Viungo ni sehemu katika mwili wako ambapo mifupa miwili huungana, kama vile vifundo vya mikono, viwiko, mabega, nyonga, magoti na vifundo vya miguu.
Viungo pia vinapatikana sehemu ambazo huenda usifikirie, kama vile katikati ya mifupa mingi iliyo kwenye miguu, mikono, fupanyonga, na uti.
Maumivu makali kwa zaidi ya kiungo kimoja (aghalabu zaidi ya viungo 5) kwa kawaida yanasababishwa na tatizo la muda mrefu la viungo
Baadhi ya magonjwa yanayosababisha maumivu ya viungo yanaweza pia kusababisha upele, homa, maumivu ya macho, au vidonda mdomoni
Ni vitu gani husababisha maumivu kwenye viungo vingi?
Visababishi vya maumivu kwenye viungo vingi kwa kawaida ni tofauti na vile vya maumivu kwenye kiungo kimoja.
Maumivu kwenye viungo vingi husababishwa na:
Ugonjwa wa baridi yabisi
Ugonjwa wa baridi yabisi ni mwako wa viungo unaosababisha kuvimba, maumivu, na kukakamaa kwa viungo. Visababishi vya ugonjwa wa baridi yabisi ni tofauti kulingana na iwapo viungo vilianza kuumia ghafla (kwa muda mfupi) au umekuwa na maumivu kwa muda mrefu (ya kudumu).
Ugonjwa wa baridi yabisi unaotokea ghafla (kwa muda mfupi) katika zaidi ya kiungo kimoja mara nyingi husababishwa na:
Maambukizi kutokana na virusi
Kuanza kwa tatizo la viungo au kulipuka kwa tatizo la viungo lililokuwepo kwa muda mrefu (kama vile ugonjwa wa baridi yabisi ya rumatoidi)
Sababu zisizotokea sana ni pamoja na:
Ugonjwa wa baridi yabisi unaodumu kwa muda mrefu katika zaidi ya kiungo kimoja husababishwa na:
Matatizo ya kuvimba, kama vile ugonjwa wa baridi yabisi ya rumatoidi, ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis, au ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kushambulia tishu na ogani
Ugonjwa wa viungo vya mwili, ambao ndio kisababishi kinachotokea sana kwa watu wazee
Ugonjwa wa baridi yabisi ya idiopathiki wa watoto (kwa watoto)
Matatizo yanayotokea sana nje ya viungo ambayo husababisha maumivu kwenye viungo ni pamoja na:
Je, ninapaswa kumwona daktari wakati gani kuhusiana na maumivu ya viungo vingi?
Mwone daktari mara moja ikiwa una maumivu kwenye zaidi ya kiungo kimoja na dalili yoyote ya tahadhari kati ya zifuatazo:
Wekundu, joto na kuvimba kwenye viungo
Upele mpya, madoa, au sehemu za zambarau kwenye ngozi
Vidonda kwenye mdomo, pua, au sehemu zako za siri
Maumivu ya kifua, kupumua kwa shida au kikohozi kipya au kikali
Maumivu tumboni mwako
Homa, kutokwa na jasho au mzizimo
Wekundu au maumivu ya macho
Mpigie daktari simu ikiwa una maumivu katika viungo vingi lakini huna dalili za tahadhari.
Je, nitarajie nini ninapokwenda kumwona daktari wangu?
Kabla ya kukupima, daktari wako atakuuliza kuhusu dalili zako na historia ya afya yako.
Dalili fulani zinaweza kumsaidia daktari kuamua kinachosababisha maumivu yako ya viungo. Dalili hizi ni pamoja na iwapo maumivu:
Yapo kwenye kiungo sawa cha pande zote mbili za mwili wako (kwa mfano, magoti yote mawili au mikono yote miwili)
Yanahama kutoka kiungo kimoja hadi kingine
Yapo kwenye uti wa mgongo na/au fupanyonga
Daktari anaweza kufanya vipimo kama vile:
Vipimo vya majimaji ya kiungo—madaktari hutoa majimaji kutoka kwenye kiungo chako kimoja kwa kutumia sindano kisha wanayatuma ili yakapimwe
Vipimo vya damu
Upimaji wa picha, kwa kawaida huwa eksirei, lakini wakati mwingine uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) au MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku)
Madaktari wanatibu vipi maumivu kwenye viungo vingi?
Madaktari watatibu tatizo linalosababisha maumivu yako ya viungo. Kwa mfano, ikiwa una tatizo la kingamwili kwenda kinyume na mwili (wakati mfumo wa kinga wa mwili wako unasababisha mwili ushambulie tishu zake), huenda ukahitaji dawa za kutuliza mfumo wako wa kingamwili.
Madaktari wanaweza pia kukutibu maumivu ya viungo kwa:
Dawa za kupunguza uvimbe zisizo za steroidi (NSAID) au asetaminofeni
Kitambaa au kombeo
Kuwekelea kitu chenye joto au baridi
Mazoezi (kama vile kutembea au kuendesha baiskeli) husaidia kuhakikisha kuwa viungo havijakakamaa na kwamba misuli yako ina nguvu ikiwa una ugonjwa wa baridi yabisi uliodumu kwa muda mrefu.