Magonjwa ya Mfumo wa Kingamwili kwenda Kinyume na Mwili

Imepitiwa/Imerekebishwa Dec 2022

Ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili ni nini?

Mfumo wa kingamwili ni mfumo wa ulinzi wa mwili wako. Inasaidia kukulinda dhidi ya magonjwa na maambukizi. Mfumo wa kingamwili kwa kawaida hushambulia bakteria, virusi, na seli za saratani. Katika ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili, mfumo wako wa kinga hushambulia mwili wako wenyewe.

  • Kuna aina nyingi tofauti za magonjwa ya mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili

  • Dalili za magonjwa ya mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili ni tofauti kulingana na ugonjwa ulionao na ni sehemu gani ya mwili wako imeathirika

  • Madaktari hufanya vipimo vya damu ili kutafuta ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili

  • Madaktari hutibu magonjwa ya mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili kwa dawa zinazopunguza kasi ya mfumo wa kinga

Magonjwa ya mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili yanaweza kushambulia sehemu yoyote ya mwili wako:

Ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili husababishwa na nini?

Mfumo wako wa kingamwili hushambulia tishu zako zenye afya. Hufanyika hivi:

  • Kwa kawaida, mfumo wako wa kingamwili hulinda mwili wako kutokana na magonjwa kwa kushambulia vitu (kama vile bakteria au virusi) ambavyo ni hatari au vinavyoathiri afya.

  • Katika magonjwa ya mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili, mfumo wako wa kinga huchukulia kimakosa sehemu za mwili wako zenye afya kuwa kitu kinachoushambulia

  • Kisha mfumo wako wa kingamwili hushambulia seli au tishu zako zenye afya kama vile zingeshambulia kitu ambacho kingekufanya uwe mgonjwa

  • Hii husababisha dalili za ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili

Baadhi ya watu wana uwezekano mkubwa wa kuwa na ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili kwa sababu upo katika familia zao.

Wanawake wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili kuliko wanaume.

Zipi ni dalili za ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili?

Dalili ni tofauti kulingana na ugonjwa ulionao na sehemu ya mwili wako iliyoathirika. Hata hivyo, kwa ujumla, magonjwa ya mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili husababisha kuvimba na kuharibiika kwa tishu. Unaweza kuwa na moja au zaidi ya dalili hizi:

  • Viungo vinavyouma

  • Viungo vyekundu, vilivyovimba

  • Kuwasha

Magonjwa ya mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili yanaweza kusababisha matatizo ya kupumua, homa ya nyongo ya manjano (macho na ngozi kuwa na rangi ya manjano), udhaifu, na kuchanganyikiwa. Unaweza kupata hali ya figo kushindwa kufanya kazi.

Wakati mwingine, ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili unaweza kusababisha kifo.

Madaktari wanawezaje kujua kama nina ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili?

Ikiwa madaktari wanashuku kuwa una ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili, watakuuliza kuhusu dalili zako, kukuchunguza, na kukufanyia vipimo vya damu.

Madaktari hutibu vipi ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili?

Madaktari kwa kawaida:

  • Hukupa dawa zinazopunguza kasi ya mfumo wako wa kingamwili na mashambulizi yake kwenye mwili wako

Dawa maarufu ambazo madaktari hutumia ni kotikosteroidi, kama vile prednisone. Wakati mwingine madaktari hutumia dawa zenye nguvu zaidi ili kupunguza kasi ya mfumo wako wa kingamwili.

Ubaya wa dawa hizi ni kwamba pia hufanya iwe vigumu kwa mwili wako kupigana na maambukizi. Baadhi ya dawa pia zinaweza kuongeza hatari yako ya kupata saratani. Daktari wako atakuangalia kwa karibu ili kusaidia kukulinda dhidi ya kupata ugonjwa mwingine.

Magonjwa mengi ya mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili ni ya muda mrefu, na mara nyingi watu walio nayo huhitaji kunywa dawa maisha yao yote.