Kisukari

Imepitiwa/Imerekebishwa Mar 2023 | Imebadilishwa Nov 2023

Ugonjwa wa kisukari ni nini?

Kisukari ni ugonjwa ambao viwango vya sukari kwenye damu yako (glukosi) ni vya juu sana.

Mtu hupata ugonjwa wa kisukari pale mwili wako unapokosa kudhibiti sukari kwenye damu inavyostahili.

  • Kuna aina 2 za kisukari, aina ya 1 na aina ya 2

  • Watu walio na aina ya 1 ya kisukari sharti watumie insulini (aina ya 1 wakati mwingine huitwa kisukari-kinachohitaji matumizi ya insulini)

  • Baadhi ya watu walio na aina ya 2 ya kisukari sharti watumie insulini, lakini wengi wanaweza kumeza tembe tu na kubadilisha lishe yao

  • Aina zote mbili za kisukari zinaweza kusababisha matatizo makubwa ya muda mrefu, kama vile shambulio la moyo na kiharusi

  • Kisukari hakina tiba, lakini unaweza kukidhibiti kwa kutumia insulini au dawa nyingine na kubadilisha kile unachokula

Je, sukari iliyo kwenye damu ni nini?

Sukari iliyo kwenye damu ni:

  • Chanzo kikuu cha nguvu ya mwili wako

Sukari iliyo kwenye damu haitokani tu na sukari iliyopo kwenye vinywaji au unayoweka kwenye chakula. Sukari iliyo kwenye damu hutoka kwa aina zote za vyakula, kama vile:

  • Mkate

  • Tunda

  • Pasta

  • Viazi

Vyakula hivi na vingine vingi vina wanga. Mwili wako hugeuza wanga kuwa sukari iliyo kwenye damu.

Je, mwili wangu unadhibiti vipi sukari iliyo kwenye damu?

Mwili wako unadhibiti kiasi cha sukari kinachotoka kwenye damu yako hadi kwenye seli za mwili wako kwa kutumia:

  • Insulini

Insulini ni homoni ambayo mwili wako hutengeneza kwenye kongosho. Kongosho ni kiungo kwenye sehemu ya nyuma ya tumbo lako.

Baada ya kula, mwili wako hufyonza chakula na sukari iliyo kwenye damu yako huongezeka. Kongosho lako hutambua viwango vya juu vya sukari kwenye damu na kuanza kuzalisha insulini. Insulini huziarifu seli za mwili wako kufyonza sukari kutoka kwenye damu. Sukari iliyo kwenye damu inapofika katika kiwango kinachofaa, kongosho lako huacha kuzalisha insulini.

Nini husababisha ugonjwa wa kisukari?

Ugonjwa wa kisukari unahusisha tatizo la insulini.

Kuna aina 2 kuu za kisukari:

  • Katika kisukari cha aina ya 1, kongosho yako haitengenezi insulini kwa sababu seli zinazoitengeneza ziliharibiwa

  • Katika aina ya 2 ya kisukari, kongosho yako hutengeneza insulini nyingi lakini seli za mwili wako haziitikii insulini jinsi inavyopaswa

Kukula vyakula vya sukari hakukusababishii kupata kisukari. Hata hivyo, kula sana hadi kupata uzani kupita kiasi kunaweza kukupa aina ya 2 ya kisukari.

Kisukari cha aina ya 1 kwa kawaida hutokea kabla ya umri wa miaka 30, haswa kwa watoto na vijana.

Aina ya 2 ya kisukari inaweza kutokea katika umri wowote lakini hutokea zaidi kwa watu ambao:

  • Una uzani au unene kupita kiasi

  • Wana umri wa miaka 30 au zaidi

  • Wana asili fulani za rangi au kabila fulani (nchini Marekani: watu wenye asili ya Wamarekani Waafrika, Wamarekani Waasia, Wamarekani Wahindi, wazawa wa Alaska, na asili ya Kihispania au Walatino wa Marekani wako katika hatari kubwa)

  • Wana wanafamilia ambao wana aina ya 2 ya kisukari

Wanawake wengine hupata aina ya 2 ya kisukari wakati wa ujauzito. Hii inaitwa kisukari cha wakati wa ujauzito.

Je, dalili za kisukari ni zipi?

Dalili za kisukari cha aina ya 1 mara nyingi huanza ghafla. Huenda yafuatayo yakatokea:

  • Kukojoa sana

  • Kuhisi kiu sana na kunywa maji kwa wingi

  • Kuwa na maumivu ya tumbo (hasa kwa watoto)

  • Kula zaidi kuliko kawaida lakini bado unapunguza uzani

  • Kuwa na uoni hafifu

  • Kuhisi usingizi au mgonjwa kwa tumbo lako

Wakati mwingine tatizo hatari linaloitwa ketoasidosisi ya kisukari hutokea. Huanza kwa ghafla na inaweza kuwa ishara ya kwanza ya ugonjwa wa kisukari kwa watoto. Ikiwa una ketoasidosisi ya kisukari, unaweza:

  • Kuwa na pumzi inayonuka kama matunda na kama kiondoa rangi ya kucha

  • Kuvuta pumzi nzito na kwa haraka

  • Unajihisi mgonjwa kwa tumbo lako na unatapika

  • Unajihisi udhaifu na kuchoka mwili mzima

Dalili za aina ya 2 ya kisukari zinaweza kuanza polepole. Huenda usiwe na dalili kwa miaka mingi. Unapokuwa na dalili, unaweza kugundua kuwa:

  • Unakojoa mara kwa mara na una mkojo mwingi

  • Unakunywa maji mengi zaidi

Dalili hizi huwa mbaya zaidi kadri wiki au miezi invyoendelea. Unaweza pia:

  • Kuhisi dhaifu sana na uchovu kila mahali

  • Kuwa na uoni hafifu

  • Kukosa maji mwilini (kutokuwa na maji ya kutosha mwilini mwako)

Je, matatizo ya kisukari ni yepi?

Ikiwa viwango vya sukari kwenye damu yako vitabaki juu kwa muda mrefu, vinaweza kusababisha matatizo mengi. Matatizo mengi hutokea kwa sababu kisukari husababisha mishipa ya damu kuziba. Mishipa ya damu iliyoziba hairuhusu damu ya kutosha kuingia kwenye viungo vyako. Kwa hivyo, unaweza kuwa na:

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina kisukari?

Madaktari watapima damu yako ili kuchunguza:

  • Viwango vya sukari kwenye damu

Kwa kawaida madaktari hupima kiwango cha sukari kwenye damu yako kama kitu cha kwanza asubuhi kabla hujala kitu chochote. Hiyo inaitwa kiwango cha sukari kwenye damu baada ya kutokula usiku kucha. Madaktari wanahitaji kupima kiwango cha sukari kwenye damu baada ya kutokula usiku kucha kwa sababu wakati mwingine wa siku sukari yako inapanda na kushuka kulingana na kiasi unachokula.

Viwango vya sukari kwenye damu baada ya kutokula usiku kucha:

  • Chini ya 100 ni vya kawaida

  • 100 hadi 125, uko katika hatari ya kisukari

  • 126 au zaidi, una kisukari

Kipimo kingine ambacho madaktari wanaweza kufanya ni:

  • Hemoglobini ya A1C

Himoglobini ni dutu iliyo ndani ya seli nyekundu za damu yako. Inabeba oksijeni katika damu yako. Sukari katika damu yako hushikamana na himoglobini na kutengeneza himoglobini ya A1C.

  • Kadiri sukari yako ya damu inavyoongezeka, ndivyo himoglobini ya A1C inavyoongezeka

Kwa kuwa himoglobini ya A1C hudumu kwa muda mrefu, kiasi chake katika damu yako hubadilika polepole. Kwa hivyo kiwango chako cha himoglobini ya A1C huonyesha daktari wako viwango vya sukari kwenye damu yako katika kipindi cha miezi 2 hadi 3 iliyopita. Watu walio na kiwango cha himoglobini ya A1C kilicho zaidi ya asilimia 6.5 wana kisukari.

Je, kisukari hutibiwa vipi?

Hakuna tiba ya kisukari. Lengo la matibabu ni kuhakikisha kuwa viwango vya sukari kwenye damu vinakaribia vya kawaida.

  • Kadiri unavyodhibiti viwango vyako vya sukari iliyo kwenye damu, ndivyo uwezekano wa kuwa na matatizo unavyopungua

Matibabu ya kisukari yanahusisha:

  • Lishe inayofaa

  • Mazoezi

  • Kupunguza uzani ikiwa wewe una uzani kupita kiasi

  • Dawa

  • Kupima viwango vyako vya sukari kwenye damu mara kwa mara

Ikiwa una kisukari, jifunze mengi kukihusu kadri uwezavyo. Zungumza na muuguzi aliyepokea mafunzo ya elimu ya kisukari. Muuguzi anaweza kukusaidia kuelewa kile unapaswa kula, kiasi cha shughuli za kujihusisha nazo, jinsi ya kupima viwango vyako vya sukari kwenye damu, na jinsi ya kurekebisha insulini yako (ikiwa inahitajika).

Je, ninapaswa kula nini?

Mwili wako hauwezi kujibu mabadiliko ya kiwango cha sukari kwenye damu yako, kwa hivyo ni muhimu:

  • Kula chakula na vitafunio wakati mahususi kila siku

  • Kula kiasi sawa cha chakula kila siku

  • Kupunguza wanga (kama vile mkate) na vyakula vya mafuta katika kila mlo

  • Kula mboga zaidi na wanga ambazo huyeyuka polepole, kama zilizopo kwa matunda, nafaka ambazo hazijakobolewa, na vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi

  • Punguza vyakula vilivyosindikwa, kama vile peremende, biskuti, donati na vitumbua vyenye sukari

  • Epuka vinywaji vyenye sukari, vikijumuisha soda, chai tamu ya barafu, lemonedi, vinywaji vya matunda na vinywaji vya spoti

  • Punguza vileo hadi 1 kwa siku ikiwa wewe ni mwanamke na 2 kwa siku ikiwa wewe ni mwanamume

Je, ninapaswa kujihusisha na shughuli za kiasi gani?

Unapaswa kujaribu kufanya mazoezi kila siku.

  • Kufanya mazoezi kunaweza kukusaidia kupata au kubaki katika uzani mzuri na kudhibiti viwango vyako vya sukari

  • Zungumza na daktari au muuguzi wako ili kufahamu kiasi cha mazoezi unayopaswa kufanya na aina ya shughuli zinazokufaa

  • Kwa kuwa kiwango cha sukari kwenye damu yako hupungua unapofanya mazoezi, huenda ukahitaji kula vitafunio au kujipa kiasi kidogo cha insulini kabla ya mazoezi marefu

Je, ninapaswa kupunguza uzani?

Ikiwa una aina ya 2 ya kisukari, ni muhimu sana kujaribu kupunguza uzani ikiwa una uzani wa kupita kiasi.

  • Kupunguza uzani kutasaidia kudhibiti sukari kwenye damu yako

Wakati mwingine, ukipunguza uzani wa kutosha huenda usihitaji kunywa dawa.

Ikiwa una kisukari cha aina ya 1, kupunguza uzani hakusaidii katika viwango vya sukari kwenye damu yako. Lakini uzani wa kupita kiasi sio afya kwa mtu yeyote.

Je, ninapaswa kupima kiwango changu cha sukari kwenye damu?

Unapaswa kupima kiwango cha sukari kwenye damu yako kwa sababu kiwango cha sukari kwenye damu hubadilika kila wakati kulingana na:

  • Unachokula

  • Shughuli unazofanya

  • Kiwango chako cha msongo wa mawazo

  • Ikiwa una maambukizi

  • Dawa unazotumia

  • Wakati wa siku

Ikiwa viwango vyako vya sukari kwenye damu vimebadilika sana, unawezahitaji kubadilisha lishe yako au dawa unayotumia.

Daktari wako atakuambia wakati na mara utakazopima kiwango cha sukari kwenye damu yako. Ikiwa una kisukari cha aina ya 1, kwa kawaida unahitaji kupima sukari kwenye damu yako mara kadhaa kwa siku. Ikiwa una aina ya 2 ya kisukari, unaweza kupima mara chache.

Mara nyingi utapima kiwango cha sukari kwenye damu yako kwa:

  • Kudunga ncha ya kidole chako kwa kifaa kidogo chenye ncha kali kiitwacho lanseti ili kupata tone la damu

  • Kuweka tone la damu kwenye kipande kidogo cha kipimo cha plastiki

  • Kuweka kipande cha kupima kwenye mashine ndogo inayosoma viwango vya sukari kwenye damu

Andika viwango vyako vya sukari kwenye damu kila wakati unapopima ili uweze kushiriki vipimo hivyo na daktari wako. Daktari wako atatumia vipimo hivyo kukuelezea ikiwa unapaswa kubadilisha dawa au lishe yako. Ikiwa hutapima kiwango cha sukari kwenye damu yako, kinaweza kuongezeka sana na hakuna mtu atakayejua.

Baadhi ya watu hutumia kifaa cha kufuatilia glukosi kila wakati—hiki hutumia kihisi kidogo kinachowekwa chini ya ngozi yako ambacho kinaonyesha matokeo ya viwango vya sukari kwenye damu yako kila baada ya dakika chache kwenye skrini ya kifaa kidogo cha mkanda kinachovaliwa kama simu ya mkononi.

Madaktari wanaweza kupima pia kiasi cha himoglobini ya A1C katika damu yako kila baada ya miezi 3 hadi 6. Hii inawawezesha kuona jinsi viwango vya sukari kwenye damu vimedhibitiwa kwa wakati.

Je, ninahitaji dawa?

  • Ikiwa una kisukari cha aina ya 1, utahitaji insulini (kupitia sindano au kipulizio)—unaweza kujifunza jinsi ya kubadilisha kiasi cha insulini kulingana na vipimo vya viwango vyako vya sukari kwenye damu

  • Ikiwa una aina ya 2 ya kisukari, utahitaji kunywa dawa, lakini pia unaweza kuhitaji insulini

Je, ninaweza kupata wapi maelezo zaidi kuhusu kisukari?