Je, hipoglisemia ni nini?
Hipoglisemiai wakati kiwango cha sukari kwenye damu yako kinapopungua sana. Sukari iliyo kwenye damu ndiyo chanzo kikuu cha nishati ya mwili wako, kwa hivyo kiwango cha chini cha sukari kwenye damu husababisha matatizo.
Hipoglisemia husababisha njaa, kutokwa na jasho, kutetemeka, na udhaifu, na hufanya iwe vigumu kufikiria vizuri
Ikiwa una kisukari, kuna uwezekano mkubwa wa wewe kupata hipoglisemia—inaweza kutokea ikiwa unatumia dawa nyingi, huli chakula cha kutosha, au unafanya mazoezi kupita kiasi
Ili kutibu hipoglisemia, kula au kunywa kitu chenye sukari (kama juisi au peremende) ili kupandisha kiwango cha sukari kwenye damu yako
Je, hipoglisemia husababishwa na nini?
Mara nyingi, hipoglisemia ni:
Tatizo la dawa zinazotumika kutibu kisukari, hasa ikiwa huli kiasi kinachofaa kwa wakati ufaao
Ikiwa huna kisukari, kuna uwezekano wa kutopata hipoglisemia. Hata hivyo, wakati mwingine unaweza kupata Hipoglisemia ikiwa:
Una uvimbe kwenye kongosho
Una matatizo makubwa ya kiafya, kama vile figo kushindwa kufanya kazi, moyo kushindwa kufanya kazi, saratani, au mshtuko (shinikizo la damu la damu kushuka kwa kiwango hatarishi)
Kunywa pombe kupita kiasi
Una matatizo ya ini kama vile sirosisi
Je, dalili za hipoglisemia ni gani?
Mwanzoni, unaweza kuwa na dalili zifuatazo:
Kutokwa jasho
Kutetemeka
Kuhisi kuzunguzungu
Njaa
Baadaye, ikiwa una hipoglisemia kali, unaweza kuwa na dalili hizi:
Kizunguzungu
Kuchanganyikiwa na kutatizika kuwa makini
Kuzungumza kwa shida
Kuzirai
Wakati mwingine, hipoglisemia hufanya ionekane kama umelewa.
Ikiwa haitatibiwa, hipoglisemia kali inaweza kusababisha matukio ya kifafa, kupoteza fahamu na kuharibika kwa ubongo.
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina hipoglisemia?
Madaktari hutambua hipoglisemia kulingana na kiwango chako cha sukari kwenye damu unapokuwa na dalili.
Je, madaktari hutibu vipi hipoglisemia?
Madaktari watakuambia utibu dalili zako nyumbani. Ikiwa una dalili, kula au kunywa vitu vyenye sukari, kama vile:
Peremende
Tembe za glukosi (sukari)
Kinywaji chenye sukari, kama vile glasi ya juisi ya matunda
Madaktari watatibu chanzo cha hipoglisemia yako:
Ikiwa dawa inasababisha hipoglisemia, madaktari watabadilisha kiasi unachotumia
Ikiwa una uvimbe kwenye kongosho, madaktari watafanya upasuaji ili kuondoa uvimbe huo
Ikiwa una kisukari au uko katika hatari ya kupata hipoglisemia, daktari wako anaweza kukushauri:
Kubeba glukagoni nawe endapo kutakuwa na dharura (glukagoni ni sindano ambayo hupandisha haraka kiwango cha sukari kwenye damu yako haraka)
Kula milo midogo siku nzima badala ya milo 3 mikubwa
Kupunguza wanga unayokula
Kubeba au kuvaa kitambulisho cha kimatibabu ili kuwafahamisha madaktari wengine kuwa una kisukari endapo kutakuwa dharura ya matibabu