Kisukari ni ugonjwa ambao viwango vyako vya sukari kwenye damu (glukosi) kuwa juu sana.
Je, ketoasidosisi ya kisukari (DKA) ni nini?
Ketoasidosisi ya kisukari ni tatizo kubwa la kisukari. Mara nyingi huitwa DKA.
Ukiwa na DKA, kiwango cha sukari kwenye damu yako hupanda, asidi inayoitwa ketoni hujaa katika damu yako, unapoteza majimaji mengi, na utendakazi wa mwili wako haufanyi kazi vizuri. Unahitaji matibabu mara moja.
Watu wenye kisukari cha aina ya 1 wana uwezekano mkubwa wa kuwa na DKA
DKA inaweza kuwa dalili ya kwanza kuwa una kisukari
Matibabu hujumuisha majimaji na insulini inayodungiwa kwenye mshipa wa damu
Bila matibabu, DKA inaweza kusababisha kupoteza fahamu na kifo
Je, DKA husababishwa na nini?
Mwili wako unahitaji insulini ili kutumia sukari iliyo kwenye damu kwa ajili ya kupata nguvu. Ikiwa huna insulini ya kutosha (kwa mfano, kwa sababu una kisukari cha aina ya 1 ambacho hakijatibiwa), kiwango cha sukari kwenye damu yako hupanda sana kwa sababu sukari haiwezi kuingia kwenye seli zako. Badala yake mwili wako huchoma mafuta kwa ajili ya kupata nguvu za mwili. Mafuta yaliyochomwa huenda kwenye ini yako na kugeuzwa kuwa asidi inayoitwa ketoni. Ketoni hujaa kwenye damu na mkojo wako.
Kiwango cha juu cha ketoni katika damu yako kinaweza kukufanya kuwa mgonjwa sana.
Ikiwa una kisukari, kuna uwezekano mkubwa wa wewe kupata DKA ikiwa:
Utaacha kutumia insuliniyako
Utaacha kufuata lishe yako kwa kuwa insulini unayotumia haitoshi
Utakuwa mgonjwa, na mwili wako uko chini ya mkazo
Vichocheo vya kawaida vya DKA ni pamoja na:
Maambukizi, kama vile nimonia au maambukizi ya njia ya mkojo
Kuvimba kwa kongosho (uvimbe wa ghafla wa kongosho)
Dawa fulani
Kunywa pombe kupita kiasi au kutumia dawa za kulevya za mitaani
Je, dalili za DKA ni zipi?
Dalili zinajumuisha:
Kiu isiyo ya kawaida
Kukojoa sana kuliko kawaida
Kupoteza uzani bila sababu dhahiri
Kuhisi mgonjwa kwenye tumbo lako au kutapika
Kuhisi udhaifu na uchovu
Maumivu ya tumbo
Kuvuta pumzi nzito, kwa haraka
Harufu ya mdomo iliyo na harufu kama ya matunda (kama vile kiondoa rangi za kucha)
DKA inaweza kupelekea kupoteza fahamu au kifo ikiwa haitatibiwa.
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina DKA?
Madaktari hufanya:
Vipimo vya damu ili kuchunguza sukari kwenye damu yako, viwango vya ketoni katika damu yako, na viwango vya baadhi ya elektroliti (madini, kama vile sodiamu na potasiamu, ambayo husaidia katika utendaji kazi mwingi muhimu mwilini)
Ili kupata matatizo ambayo yanaweza kuwa yanasababisha DKA yako, madaktari wanaweza kufanya vipimo kama vile:
Vipimo vya mkojo
ECG (elektrokadiogramu, kipimo kinachopima mikondo ya umeme ya moyo wako na kuzirekodi kwenye karatasi)
Je, madaktari wanatibu vipi DKA?
DKA ni dharura ya kimatibabu. Utahitaji kwenda hospitalini na huenda ukahitaji kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Madaktari hutibu DKA kwa:
Majimaji na elektroliti kwenye mshipa wako wa damu
Kuweka Insulini kwenye mshipa wako wa damu
Vipimo vya damu kila baada ya saa chache ili kuangalia viwango vya sukari, ketoni na elektroliti ili kuhakikisha kuwa vinarejea katika hali ya kawaida
Madaktari pia hutibu tatizo lingine lolote lililosababisha DKA.