Je, mshtuko ni nini?

Mshtuko ni dharura ya kiafya inayosababishwa na viungo vyako kutopata damu na oksijeni ya kutosha. Wakati mwili wako hauwezi kufikisha damu ya kutosha kwa viungo vyako, viungo hivyo huanza kuacha kufanya kazi. Shinikizo lako la damu ni la chini sana unapopata mshtuko.

  • Unaweza kupata mshtuko kutokana na kupoteza damu nyingi, kutokuwa na maji ya kutosha katika mwili wako, au kuwa na matatizo ya moyo, maambukizi mabaya, au mimenyuko ya mizio

  • Mshtuko hukufanya uhisi dhaifu, kizunguzungu, na kuchanganyikiwa, na unaweza kuzimia

  • Madaktari hutibu chanzo cha mshtuko na kukupa maji, oksijeni, na wakati mwingine dawa za kusaidia kuongeza shinikizo la damu

  • Bila matibabu, mtu aliye katika mshtuko ataaga dunia

Watu walio katika mshtuko wanahitaji matibabu ya dharura. Ikiwa unafikiri mtu amepata mshtuko:

  • Piga simu kwa 911 kwa ajili ya gari la wagonjwa

  • Jaribu kuzuia kuvuja damu nyingi kwa kuweka shinikizo kwenye sehemu inayovuja damu kwa kutumia kitambaa

  • Mlaze mtu huyo chini, mfunike ili awe na joto huku miguu ikiwa imeuliwa juu kidogo

Je, mshtuko husababishwa na nini?

Kuna aina kadhaa za sababu za mshtuko:

  • Mwili wako hauna damu au maji ya kutosha, kwa sababu umetokwa na damu nyingi au umepungukiwa na maji mwilini

  • Moyo wako unapiga kwa udhaifu

  • Mishipa yako ya damu hutulia na kukuwa pana, jambo ambalo linaweza kutokea ikiwa una mmenyuko wa mzio, maambukizi makali, sumu, au uharibifu wa mfumo wako wa neva

Mshtuko unaweza kusababisha ogani zako (kama vile ubongo, moyo, na mapafu) kuacha kufanya kazi kwa sababu hazipati damu ya kutosha.

Je, dalili za mshtuko ni zipi?

Dalili za mshtuko ni pamoja na:

  • Udhaifu, kizunguzungu, na kuchanganyikiwa

  • Ngozi baridi, iliyopauka, inayotokwa na jasho

  • Kuzirai

  • Kuwa na kichefuchefu na kutapika

Je, madaktari wanawezaje kujua kuwa nina mshtuko?

Madaktari wanajua kuwa una mshtuko kulingana na dalili zako na shinikizo la damu. Watafanya vipimo ili kujua chanzo ikiwa hakiko wazi kulingana na dalili zako.

Je, madaktari hutibu vipi mshtuko?

Madaktari watakutibu hospitalini na kukupa:

  • Vioevu unavyotiwa mwilini (vioevu unavyotiwa kwenye mshipa wako kupitia mirija miembamba ya plastiki)

  • Kuongezewa damu ikiwa umepoteza damu nyingi

  • Wakati mwingine, dawa ya kuongeza shinikizo la damu yako

Madaktari pia hutibu chanzo cha mshtuko wako, matibabu ambayo yanaweza kujumuisha kukupa dawa zingine au kukufanyia upasuaji.