Figo Kushindwa Kufanya Kazi kwa Ghafla

(Jeraha Kali la Figo)

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2023

Figo zako ni viungo 2 vyenye umbo la maharagwe vinavyotoa mkojo. Zina ukubwa unaotoshana na ngumi yako na ziko nyuma ya tumbo lako, karibu na uti wa mgongo wako. Figo husawazisha viwango vya maji na madini mwilini na kuchuja uchafu kwenye damu.

Je, figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla ni nini?

Tatizo kali ni tatizo ambalo limeanza na labda halitadumu kwa muda mrefu sana. Kwa hivyo, figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla ni wakati figo moja au zote mbili zinaacha kufanya kazi kwa siku au wiki chache. Ikiwa figo zako zitaacha kufanya kazi kwa muda mrefu, utakuwa na ugonjwa sugu wa figo.

Madaktari sasa hutumia neno "jeraha kali la figo" kurejelea hali ya figo kushidwa kufanya kazi kwa ghafla. Lakini figo kushindwa kufanya kazi bado ndilo neno ambalo watu wengi wanalijua.

  • Uharibifu wa figo moja hausababishi matatizo makubwa mradi tu figo yako nyingine inafanya kazi—figo zako zote mbili zinahitaji kuacha kufanya kazi ili uwe na matatizo makubwa

  • Unaweza kuwa na uvimbe kwenye miguu, vifundo vya miguu, au usoni, kujihisi mgonjwa na mchovu, kuwashwa na mwili mzima, matatizo ya kupumua, au kukojoa (kukojoa) kidogo kuliko ya kawaida

  • Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla kunaweza kusababisha matatizo makubwa, kama vile moyo kushindwa kufanya kazi

  • Huenda ukahitaji huduma ya kusafisha damu

The Urinary Tract

Je, hali ya figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla husababishwa na nini?

Hali mbaya ya figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla inaweza kusababishwa na:

  • Kuingia kwa damu kidogo kwenye figo

  • Kitu ambacho huzuia mkojo kutoka kwenye figo zako

  • Magonjwa fulani ya figo

  • Dawa au sumu fulani

Figo zako zinahitaji damu nyingi. Huenda figo zako zisipate damu ya kutosha ikiwa unavuja damu nyingi, umepungukiwa na maji sana, au moyo wako hausukumi damu ya kutosha.

Ikiwa saratani au ugonjwa wa mawe kwenye figo huzuia mtiririko wa mkojo, shinikizo huongezeka kwenye figo. Ikiwa shinikizo linaendelea kuwa juu kwa muda mrefu, figo zako zitaharibika.

Dawa nyingi na vitu vingine vinaweza kuharibu figo zako, kwa mfano:

  • Baadhi ya dawa za kuua bakteria

  • Dawa zinazotumika kuleta utofautishaji katika eksirei

Dawa zinazotumika kuleta utofautishaji katika eksirei ni vioevu vinavyowekwa kwenye mshipa ambavyo hurahisisha mishipa ya damu na viungo kuonekana kwenye eksirei.

Mara nyingi, madaktari hawawezi kupata chanzo cha figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla.

Je, dalili za figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla ni zipi?

Dalili zako zinategemea:

  • Figo yako imejeruhiwa kwa kiasi gani

  • Kile kilichosababisha figo zako kushindwa kufanya kazi kwa ghafla

  • Kasi ya kuongezeka kwa matatizo yako ya figo

Kwanza, unaweza kuwa na dalili zinazojumuisha:

  • Kuongeza uzani

  • Kuvimba kwa miguu na vifundo vyako

  • Kuvimba kwa uso na mikono yako

  • Kukojoa kidogo au kutokojoa kabisa—watu wazima wengi wenye afya nzuri hukojoa kati ya vikombe 3 na lita 2 za mkojo kwa siku.

Dalili za baadaye:

  • Kuhisi kichefuchefu, uchovu, na kupungua kwa hamu ya kula

  • Tatizo la kuwa makini

  • Kuwashwa au vipele

Unaweza pia kuwa na dalili za tatizo lililosababisha figo yako kushindwa kufanya kazi.

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina tatizo la figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla?

Daktari wako atafanya:

Je, madaktari hutibu vipi tatizo la figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla?

Madaktari hutibu tatizo linalosababisha figo yako kushindwa kufanya kazi kwa ghafla. Daktari wako anaweza pia:

  • Kukuagiza kula mlo maalumu ambao unapunguza kiasi cha maji, chumvi, fosforasi, na potasiamu unayokula

  • Kukuagiza ujipime uzani kila siku ili kujua ikiwa unahifadhi maji mwilini

  • Kukupa dawa za kusawazisha viwango vya potasiamu au fosforasi katika damu yako

  • Kukupatia huduma ya kusafisha damu ili kusaidia kuondoa uchafu na maji ya ziada kutoka kwenye damu yako

Baadhi ya majeraha ya figo ni mabaya na yanaweza kuhatarisha maisha, na yanahitaji kutibiwa katika kitengo maalum cha huduma hospitalini. Unaweza kuhitaji upasuaji, kwa mfano, ikiwa figo zako na mtiririko wa mkojo umezuiliwa.