Tomografia ya kompyuta (uchanganuzi wa CT) ni nini?
Uchanganuzi wa CT hutumia mashine kubwa yenye umbo la donati kubwa kuchukua eksirei kutoka pande nyingi. Kisha kompyuta huchukua eksirei na kuunda picha nyingi za ndani ya mwili wako. Kila picha inaonekana kama kipande kilichochukuliwa kutoka sehemu moja ya mwili wako. Kompyuta pia inaweza kuunda picha ya 3-D ya sehemu ya ndani ya mwili wako.
Uchanganuzi wa CT ni mzuri katika kuonyesha taarifa za ogani na tishu zingine katika ubongo, kichwa, shingo, kifua na tumbo.
Uchanganuzi wa CT hukupa mnururisho mkubwa zaidi kuliko eksirei ya kawaida
Ni kwanini ninaweza kuhitaji kufanyiwa uchanganuzi wa CT?
Madaktari hutumia uchanganuzi wa CT kwa matatizo ya aina nyingi, kama vile:
Matatizo katika ubongo na uti wa mgongo wako, kama vile kutokwa na damu, uvimbe, au kasoro za kuzaliwa
Matatizo ndani ya tumbo lako, kama vile matumbo yaliyoziba na uvimbe au maambukizi kwenye figo, ini, au mapafu yako.
Matatizo katika viungo vya uzazi vya mwanamke, kama vile uvimbe kwenye uterasi au ovari
Mishipa ya damu isiyo ya kawaida ya moyo wako au mkole (ateri kubwa iliyounganishwa na moyo wako)
Mifupa iliyovunjika, haswa kwenye nyonga, mgongo (uti wa mgongo), na fupanyonga
Misuli na kano zilizovunjika
Kitu gani hufanyika wakati wa uchunganuzi wa CT?
Kabla ya uchanganuzi
Mara nyingi, huhitaji kufanya chochote ili kujiandaa kwa uchanganuzi wa CT. Wakati mwingine, madaktari watakupa kiowevu (majimaji yenye kutofautisha) kupitia mshipa, au cha kumeza, au wakati mwingine kuingizwa kwenye tundu lako la haja kubwa. Majimaji yenye kutofautisha hufanya sehemu fulani ya mwili wako ionekane kwenye skani kwa uwazi zaidi.
Wakati wa uchunguzi
Utalala tuli huku meza ikisogezwa kupitia skana kubwa yenye umbo la donati
Huenda ukahitaji kushikilia pumzi kwa muda mfupi ili picha zisiwe na ukungu
Unaweza kusikia milio ya mvumo wakati skana inaposogezwa kuchukua eksirei kutoka pande nyingi
Uchanganuzi wa CT kwa kawaida hudumu kwa sekunde chache hadi dakika chache
Baada ya uchunguzi
Unaweza kuendelea na shughuli zako za kawaida.
Je, uchanganuzi wa CT una hatari gani?
Mionzi
Uchanganuzi wa CT hukuangazia mnururisho zaidi kuliko eksirei ya msingi. Kwa mfano, uchanganuzi wa CT ya tumbo hutumia takriban mara 300 hadi 400 ya kiasi cha mnururisho unaotumiwa na eksirei kuangalia kifua mara moja. Madaktari hujaribu kupunguza mara ambazo unawekwa kwenye mionzi. Mionzi kwa wingi inaweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani.
Kwa wajawazito na watoto, madaktari hujaribu kutumia vipimo vingine isipokuwa kama CT ndiyo njia bora zaidi ya kugundua tatizo hatari la kiafya.
Matatizo mengine
Wapo watu ambao huhisi usumbufu majimaji yenye kutofautisha yakiingia
Wengine hupata mmenyuko wa mzio kutokana na majimaji yenye kutofautisha (kama vile kupiga chafya, upele, au shida ya kupumua)
Ikiwa una matatizo ya figo, majimaji yenye kutofautisha yaweza kufanya matatizo yako ya figo kuwa mabaya zaidi