Upigaji Picha kwa Mvumo wa Sumaku (MRI)

Imepitiwa/Imerekebishwa Dec 2023

MRI ni nini?

MRI ni kipimo kinachotumia mashine yenye sumaku yenye nguvu ya kuzalisha picha za ndani ya mwili wako. Kompyuta hutengeneza mfululizo wa picha zenye maelezo. Kila picha inaonekana kama kipande kilichochukuliwa kupitia mwili wako. Kompyuta pia inaweza kuunda picha ya 3-D ya sehemu ya ndani ya mwili wako. Tofauti na vipimo vya CT (tomografia ya kompyuta) na PET (picha ya tishu inayotokana na dawa yenye mnururisho), MRI haitumii eksirei (mnururisho).

  • Kipimo cha MRI hakitumii eksirei au mnururisho na kwa kawaida ni salama kabisa

  • Kwa kawaida MRI hutoa taarifa zaidi kuliko uchanganuzi wa CT, lakini MRI huchukua muda mrefu na huchosha zaidi

  • Kwa sababu inatumia sumaku zenye nguvu, huwezi kufanyiwa MRI ikiwa una aina fulani za vitu vya chuma mwilini mwako.

  • Mashine nyingi za MRI hukuweka kwenye upenyo mwembamba, kwa hivyo watu wengine hupata wasiwasi sana (klaustrofobia) na hawawezi kufanya kipimo.

  • Baadhi ya mashine za MRI zina mwanya mkubwa ("MRI wazi") ambao hausumbui sana watu

Kwa nini ningehitaji MRI?

Madaktari wanaweza kutumia MRI badala ya uchanganuzi wa CT wakati maelezo zaidi yanahitajika ili kugundua na kuona:

  • Matatizo katika ubongo, uti wa mgongo, misuli, na ini lako

  • Matatizo katika viungo vya uzazi wa kike

  • Kuvunjika kwa mifupa ya nyonga na fupanyonga

  • Matatizo katika viungo vyako, kama vile kuchanika au kutenguka

  • Kutokwa na damu au maambukizi

Madaktari wanaweza kuchagua kipimo cha MRI badala ya uchanganuzi wa CT iwapo:

  • Umewahi kupata mmenyuko wa mzio (kama vile kupiga chafya, upele, au kuishiwa na pumzi) kutokana na majimaji yenye kutofautisha yanayotumika kwenye uchanganuzi wa CT

  • Wewe ni mjamzito (kwa sababu uchanganuzi wa CT hutoa mnururisho na MRI haitoi)

Ni kitu gani hufanyika wakati wa kipimo cha MRI?

Kabla ya kupimwa

Utotoa kila kitu kwenye mifuko yako na kuvua vito, mikanda na vitu vingine vyovyote vyenye chuma. Mara nyingi unaweza kuingia ukiwa umevaa nguo.

Wakati mwingine, madaktari huingiza kiowevu (kinachoitwa majimaji ya sumaku yenye kutofautisha) kwenye mshipa au kiungo. Majimaji yenye kutofautisha ya MRI hufanya sehemu fulani za mwili wako zionekane kwenye picha kwa uwazi zaidi.

Ikiwa una wasiwasi kuhusu kufungiwa kwenye mashine ya MRI, madaktari wanaweza kukupa dawa ya kusaidia kukutuliza.

Wakati wa kupimwa

  • Utalala tuli kwenye meza huku ikisogezwa kupitia skana kubwa yenye umbo la neli

  • Madaktari wanaweza kukuruhusu uvae vifaa vya kuzuia sauti masikioni ili kuzuia kelele kubwa zinazotolewa na skana.

  • Madaktari wanaweza kukuambia ushikilie pumzi yako wakati fulani

Uchanganuzi kwa kawaida huchukua dakika 20 hadi 60.

Baada ya kupimwa

Unaweza kuendelea na shughuli zako za kawaida.

Vipimo vya MRI vinahusishwa na matatizo gani?

Huchukua muda mrefu kuliko uchanganuzi wa CT

Uchanganuzi wa MRI huchukua muda mrefu zaidi kuliko uchanganuzi wa CT. Huwa hazitumiwi sana katika hali za dharura wakati matokeo ya haraka yanahitajika, kama vile ukiwa na jeraha mbaya au kiharusi.

Nafasi ndogo, iliyofungiwa

Skana nyingi za MRI ni ndogo na zimefungwa. Unaweza kuhisi klaustrofobia (woga wa kuwa katika nafasi ndogo iliyofungwa) wakati wa uchanganuzi, hata kama kwa kawaida huwa huogopi kuwa katika nafasi zilizofungwa. Pia, watu ambao wana mwili mkubwa sana wanaweza wasienee kwenye skana.

Baadhi ya skana za MRI zimetengenezwa kwa neli kubwa amabyo ni wazi upande mmoja (MRI wazi). Lakini picha zao sio wazi kama zile za skana za kawaida.

Matatizo ya uga wa sumaku

Ikiwa una vitu fulani vyenye chuma ndani ya mwili wako, uga wa sumaku wa MRI unaweza kuathirika. Mtaalamu wa MRI atakuuliza kuhusu vitu vyote vyenye chuma vilivyo kwenye mwili wako. Baadhi ya vyuma ni salama na vingine si salama. Mafundisanifu wana orodha yenye maelezo ya kina kuhusu vyuma vilivyo salama kwa kila mashine ya MRI. Lakini kwa ujumla, MRI ni tatizo kwenye:

  • Vifaa vya kimatibabu vinavyodhibitiwa na sumaku, kama vile kifaa cha kurekebisha mapigo ya moyo, kifaa cha kudhibiti kubana kwa misuli ya moyo, au kifaa cha upandikizaji wa uti wa sikio—MRI inaweza kufanya kifaa kisifanye kazi ipasavyo

  • Vifaa vya kimatibabu vyenye nyaya au vyuma vingine vinavyoweza kupitisha nguvu za umeme—MRI inaweza kufanya kifaa kipate joto jingi sana na kikuchome

  • Aina ya chuma kinachoweza kuvutwa na sumaku—MRI inaweza kusogeza chuma hicho ndani ya mwili wako

Baadhi ya vifaa vya kimatibabu ni salama kwenye vipimo vya MRI, ikiwa ni pamoja na meno ya kupandikiza, nyonga bandia, na vyuma vinavyotumiwa kunyoosha uti wa mgongo.

Athari kutokana na majimaji yenye kutofautisha, yanapotumiwa

Kuna uwezekano mdogo wa kupata mmenyuko wa mzio kutokana na rangi inayotumiwa wakati wa kipimo cha MRI kuliko wakati wa uchanganuzi wa CT. Hata hivyo, huenda ukapata maumivu ya kichwa, kizunguzungu, maumivu ya tumbo, maumivu au ladha isiyo ya kawaida mdomoni. Kwa nadra, unaweza kupata uharibifu wa figo. Kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa uharibifu wa figo ikiwa tayari una matatizo ya figo.