Uchunguzi unaotumia kemikali nunurishi ni nini?
Uchunguzi huu unatumia kemikali iliyo na elementi nunurishi. Madaktari hukupa kipimo kidogo cha elementi hiyo nunurishi. Elementi hiyo hujikusanya katika sehemu maalum ya mwili na kutoa miali inayotambuliwa na mashine ya kuchunguza iliyowekwa juu ya sehemu hiyo. Mashine ya kuchunguza hupiga picha ya mahali miali ilipo na nguvu za miali hiyo. Hali hii huwasaidia madaktari kuona kinachoendelea kwenye tishu wanayopima.
Madaktari wanaweza kukupa elementi nunurishi kama:
Sindano
Kitu cha kumeza
Gesi ya kupumua ndani
Elementi tofauti nunurishi huenda kwenye sehemu tofauti za mwili. Madaktari huchagua elementi nunurisi watakayotumia kulingana na sehemu ya mwili wanayotaka kupiga picha. Uchunguzi wa elementi nunurishi unaweza kuwasaidia madaktari kupata matatizo katika sehemu nyingi za mwili wako:
Tezi dundumio
Ini
Kibofu nyongo
Mapafu
Njia ya mkojo
Mifupa
Ubongo
Mishipa fulani ya damu
Ninaweza kuhitaji uchunguzi wa elementi nunurishi kwa sababu gani?
Madktari hutumia upimaji huu kubaini matatizo kama vile:
Kuzibwa kwa mtiririko wa damu inayokwenda moyoni
Saratani iliyoenea kwenye mifupa au ini lako
Uvimbe (kuviba na maumivu) au maambukizi ndani ya ogani
Kuvuja damu, kama vile kwenye utumbo wako
Wakati mwingine, madaktari watatumia upimaji huo kuona iwapo sehemu fulani ya mwili wako inafanya kazi vizuri. Kwa mfano, madaktari wanaweza kuona iwapo moyo wako unafanya kazi vizuri wakati unapiga damu kwa nguvu kwa kufanya upimaji unapotembea au unapokimbia kwenye kinu cha kuendesha kwa miguu. Ikiwa ulipata shambulio la moyo, madaktari wanaweza kufanya kipimo hiki ili waone jinsi moyo wako unavyopata nafuu.
Kitu gani hufanyika wakati wa uchunguzi wa elementi nunurishi?
Kabla ya kupimwa
Huenda ukaombwa usile au usinywe kwa saa kadhaa kabla ya uchunguzi
Madaktari hudunga elementi nunurishi kwenye mshipa lakini wakati mwingine unaweza kuimeza au kuipumua
Utasubiri dakika kadhaa au hadi saa kadhaa wakati elementi nunurishi inasafirishwa mwilini mwako
Wakati wa uchunguzi
Utalala tuli juu ya meza huku mashine ya uchunguzi ikipiga picha, kwa kawaida huchukua kama dakika 15
Wakati mwingine utahitaji kufanyiwa uchunguzi mwingine baada ya kusubiri kwa muda zaidi, pengine baada ya saa kadhaa
Baada ya uchunguzi
Madaktari watakushauri unywe maji mengi au vioevu vingine ili kusaidia kuosha elementi nunurishi kutoka mwilini mwako.
Uchunguzi unaotumia elementi nunurishi una madhara gani?
Mionzi
Uchunguzi unaotumia elementi nunurishi hukuweka hatarini ya miali zaidi kuliko eksirei moja. Madaktari hujaribu kupunguza mara ambazo unawekwa kwenye mionzi katika maisha yako yote. Kupata mionzi kwa wingi kunaweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani.
Ikiwa wewe ni mjamzito au unashuku kuwa una ujauzito, waambie madaktari kabla ya kufanyiwa uchunguzi unaotumia elementi nunurishi.
Elementi nunurishi husalia mwilini kwa siku kadhaa. Ukisafiri kwa ndege ndani ya siku chache baada ya kufanyiwa uchunguzi huu, huenda ving'ora vya kuashiria vifaa nunurishi vikalia. Pata barua ya daktari ya kuonyesha katika uwanja wa ndege.
Matatizo mengine
Upimaji unaweza kuchukua muda mrefu, hadi saa kadhaa
Picha zinazotokana na uchunguzi wa elementi nunurishi hazina maelezo ya kina kama picha kutoka vipimo vingine vya picha, kama vile, eksirei, changanuzi za CT (tomografia ya kompyuta), au MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku)