Atrasonografia (atrasaundi) ni nini?
Atrasonografia ni kipimo salama cha picha ambacho hutumia mawimbi ya sauti kuunda picha inayosonga ya sehemu za ndani za mwili wako. Atrasonografia haitumii miali hatari (eksirei). Atrasonografia pia huitwa kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti au sonogramu.
Atrasonografia haisababishi uchungu na ni salama kabisa, hata ukiwa mjamzito
Atrasonografia inaweza kuonyesha sehemu za mwili wako zinazosonga, kama vile moyo unaopiga
IAN HOOTON/MAKTABA YA PICHA ZA SAYANSI
Kwanini ninaweza kuhitaji kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti?
Madaktari wanaweza kutumia kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti kugundua vinyama kwenye shingo, matiti, kinena, mikono au miguu yako. Kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti kinaweza kusaidia kubaini tofauti kati ya sisti (kifuko kilichojaa majimaji) na uvimbe mgumu. Kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti kinaweza pia kuonyesha matatizo kwenye ogani katika tumbo, eneo la nyonga (fupanyonga), na kifua, kama vile:
Sehemu za moyo wako ambazo zina ukubwa au umbo lisilofaa
Vijiwe vidogo au uzibaji kwenye kibofu nyongo
Uvimbe
Ikiwa madaktari wanahitaji kuchukua sampuli ya uvimbe au kinyama kingine, wanaweza kutumia kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti ili kuwaongoza.
Ikiwa wewe ni mjamzito, madaktari watafanya kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti ili kuona jinsi mtoto wako anavyokua.
Aina maalumu za kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti kwa ajili ya matatizo ya moyo na mishipa ya damu
Kipimo cha Doppler cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti huonyesha moyo wako ukipiga na damu yako ikisafirishwa, hivyo madaktari wanaweza kuona:
Matatizo katika jinsi moyo wako unavyopiga
Matatizo yanayohusiana na njia ya mzunguko wa damu kupitia mishipa yako ya damu.
Kipimo cha Doppler ya rangi cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti huonyesha upande ambao damu yako inasafirishwa:
Kwenda kwenye ogani zako
Kwenda kwenye uvimbe au madonda ndugu mengine
Katika kichwa na shingo yako, ili kubaini uwezekano wa kupata kiharusi
Ni kitu gani hufanyika wakati wa kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti?
Kabla ya kupimwa
Ikiwa madaktari wanafanya kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti kwenye sehemu ya tumbo lako, watakuomba usile wala kunywa kwa saa kadhaa kabla ya upimaji. Hata hivyo, ikiwa wanapiga picha ya ogani za kike (au tezi kwa wanaume), huenda wakakuomba unywe maji zaidi ili ujaze kibofu cha mkojo.
Wakati wa kupimwa
Utalala juu ya meza
Madaktari huweka jeli kwenye ngozi yako juu ya sehemu ya mwili wanayotaka kuona
Watapitisha kifaa kidogo cha kushikilia kwa mkono juu ya ngozi yako
Kifaa hicho hutuma mawimbi ya sauti ndani ya mwili wako na kurekodi jinsi mawimbi hayo ya sauti yanavyorudi kutoka kwenye ogani zako za ndani
Mawimbi hayo yana sauti kali mno hivi kwamba huwezi kuyasikia
Kompyuta hubadilisha mawimbi ya sauti kuwa picha tuli au filamu ya sehemu za ndani za mwili wako
Kwenye baadhi ya vipimo, madaktari wanaweza kuweka kifaa ndani ya mwili wako—kwa mfano, ndani ya uke ili kupata picha za tumbo lako la uzazi ukiwa mjamzito, au kwenye rektamu ili kupata picha za tezi dume na kubaini iwapo kuna saratani.
Ni yapi matatizo ya kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti?
Kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti hakisababishi madhara yoyote
Kuwekwa kifaa kwenye uke au rektamu kunaweza kusababisha usumbufu
Mfupa au gesi inaweza kuziba kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti