Mfumo wa kingamwili ni mfumo wa ulinzi wa mwili wako. Inasaidia kukulinda dhidi ya magonjwa na maambukizi. Mfumo wa kingamwili kwa kawaida hutendana na kushambulia bakteria, virusi, na seli za saratani. Mzio hutokea pale ambapo mfumo wa kingamwili humenyuka kutokana na kitu kisicho na madhara, kama vile chakula, mimea, au dawa.
Je, mmenyuko wa mzio ni nini?
Mmenyuko wa mzio ni kile kinachotokea unapogusa, kula, au kupumua kitu ambacho husababisha mzio. Mmenyuko wa mzio unaweza kuwa mdogo au mbaya.
Athari ndogo husumbua na kuudhi
Athari kali zinaweza kutishia maisha
Ni nini husababisha mmenyuko wa mzio?
Madaktari hawana uhakika kwa nini baadhi ya watu huwa na mzio kwa kitu fulani ilhali wengine hawana.
Mzio hupatikana katika familia
Yale ambayp ulipatana nayo na kula ulipokuwa mtoto yanaweza kuathiri iwapo utapata mizio
Vitu ambavyo kwa kawaida huchochea mmenyuko wa mzio ni pamoja na:
Vumbi kwenye nyumba
Magamba ya wanyama
Chavua (ya miti, nyasi, magugu)
Ukungu
Vyakula fulani
Dawa fulani
Dalili za mmenyuko wa mzio ni zipi?
Mmenyuko mdogo wa mzio unaweza kusababisha:
Macho yenye majimaji na kuwasha
Pua zinazotoa makamasi na kupiga chafya
Kuwashwa ngozi, wakati mwingine na upele (mabaka ya ngozi)
Mmenyuko mkali wa mzio (anafilaksisi) unaweza kusababisha:
Kuvimba macho, midomo, ulimi na koo
Kuforota na kuishiwa pumzi
Kukakamaa, kujihisi mgonjwa kwenye tumbo lako, na kutapika
Kizunguzungu na kuzirai kwa sababu ya kushuka kwa shinikizo la damu
Kifo
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina mmenyuko wa mzio?
Kwa kawaida madaktari wanaweza kujua kulingana na dalili zako na kwa kukuchunguza. Hata hivyo, inaweza kuwa vigumu kwa madaktari kujua ni nini hasa una mzio nao. Wanaweza kufanya vipimo vya ngozi au vipimo vya damu ili kujua.
Madaktari hutibu vipi mmenyuko wa mzio?
Kwa athari ndogo, daktari wako anaweza kukupa:
Dawa za homoni za kunyunyiza puani kuzuia uvimbe
Antihistamini
Dawa za kuzuia kufungana
Matone ya macho
Kwa athari kali, unaweza kuhitaji:
Chanjo ya epinefrini
Antihistamini na kotikosteroidi zinazodungiwa kwenye mshipa (IV)
Dawa na viowevu zinazotolewa kupitia mshipa ili kupandisha shinikizo lako la damu
Dawa ya kufungua mkondo wako wa hewa na kukusaidia kupumua
Wakati mwingine, bomba la kupumua kwenye koo lako ili madaktari wakuweke kwenye kipumuaji ili kukusaidia kupumua
Ninawezaje kuzuia mmenyuko wa mzio?
Njia muhimu zaidi za kuzuia mmenyuko wa mzio:
Epuka vitu vinavyosababisha mizio
Ikiwa huwezi kuepuka vitu ambavyo una mzio navyo, muulize daktari wako kuhusu chanjo za mzio
Kuepuka kizio kunaweza kuhusisha:
Kuacha kutumia dawa fulani
Kuweka wanyama kipenzi nje ya nyumba au kuwazuia wasiingie kwenye vyumba fulani
Kutumia vichungi vya chembechembe vyenye ufanisi mkubwa (HEPA)
Kutokula chakula fulani
Kuondoa au kubadilisha vitu vinavyokusanya vumbi, kama vile fanicha laini, mazulia, na vyombo vingine
Kuweka matandiko maalum kwenye godoro na mito ili kuzuia wadudu wa vumbi
Kwa kutumia mito ya nyuzi za sanisia
Kuosha shuka, foronya na blanketi mara kwa mara kwa maji ya moto
Kusafisha nyumba mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na kutoa vumbi, kuvuta uchafu, na kudeki
Kutumia viyoyozi na viondoa unyevunyevu katika vyumba vya chini na vyumba vingine vinavyopata unyevu
Kuondoa mende
Katika chanjo za mizio, daktari hukupa chanjo za vitu ambavyo una mzio navyo. Mwanzoni, sindano zina dawa kidogo sana. Kiasi hicho ni kidogo mno kusababisha athari kali. Kisha daktari anakupa dozi zilizo na dawa zaidi. Kwa njia hiyo, mwili wako unaweza kuzoea vitu hivyo na usipate mzio. Huenda sindano za kuzuia mizio zisifanye kazi kila wakati. Na zinapofanya kazi, huenda ukahitaji kuendelea kujidunga.