Mzio wa Msimu

Imepitiwa/Imerekebishwa Dec 2022

Mizio ya msimu ni nini?

Mzio hutokea pale ambapo mfumo wa kingamwili humenyuka kutokana na kitu kisicho na madhara, kama vile chakula, mimea, au dawa. Mizio ya msimu ni mizio ambayo hutokea tu kwenye msimu wa mwaka ambapo dutu fulani inayokupa mzio (kizio) iko hewani. Wakati mwingine mizio ya msimu huitwa "homa ya nyasi." Nyasi, chavua, au ukungu ni vizio vya kawaida vinavyosababisha mizio ya msimu.

Mizio ya msimu inaweza kutokea katika msimu wa mchipuko, joto, au vuli, kulingana na kile kinachokupa mzio.

  • Mizio ya msimu ni utendanaji wa mwili wako kwa chavua, nyasi, au ukungu hewani

  • Kwa kawaida husababisha kutokwa na makamasi na kuwasha kwa pua na macho

  • Dawa inaweza kusaidia kupunguza ukali wa dalili zako

Ni nini husababisha mizio ya msimu?

Mizio ya msimu mara nyingi husababishwa na:

  • Chavua

  • Nyasi na magugu

  • Vijimbegu vya ukungu

Kiasi na aina ya chavua, nyasi na vizio vingine hewani hubadilika kulingana na mahali unapoishi.

Dalili za mizio ya msimu ni zipi?

  • Macho mekundu yanayowasha na yenye machozi

  • Kuziba kwa pua au kutokwa na kamasi

  • Kupiga chafya

Dalili zako hutokea na kutoweka kulingana na msimu.

Daktari wangu anawezaje kujua kama nina mizio ya msimu?

Daktari wako anaweza kujua kama una mizio ya msimu kwa kuuliza maswali kuhusu dalili zako na kama hutokea katika misimu fulani. Hii inaweza pia kusaidia madaktari kujua ni kizio gani husababisha dalili zako.

Vipimo vya ngozi vinaweza kusaidia madaktari kujua ni kizio gani kinachosababisha mzio wako.

Madaktari hutibu vipi dalili za mizio ya msimu?

Daktari wako atakuagiza utibu mizio yako kwa:

  • Dawa za homoni za kunyunyiza puani kuzuia uvimbe

  • Antihistamini

  • Dawa za kuzuia kufungana

  • Matone ya macho

Ikiwa dawa hizi hazisaidii na dalili zako ni kali, daktari anaweza kupendekeza:

  • Dozi za mzio (kupunguza hisi)

Katika kupunguza hisi, daktari hukudunga sindano ya dutu ambazo una mzio nayo. Mwanzoni, sindano zina dawa kidogo sana. Kiasi hicho ni kidogo mno kusababisha athari kali. Kisha daktari anakupa dozi zilizo na dawa zaidi. Kwa kufanya hivyo, mwili wako unaweza kuzoea dutu hiyo na usipate mmenyuko wa mzio. Huenda sindano za kuzuia mizio zisifanye kazi kila wakati. Na zinapofanya kazi, huenda ukahitaji kuendelea kujidunga.