Nyenzo za Mada
Je, homa ya nyongo ya manjano ni nini?
Homa ya nyongo ya manjano ni wakati ngozi yako na sehemu nyeupe za macho yako zimegeuka kuwa za manjano.
Homa ya nyongo ya manjano husababishwa na kukusanyika kwa dutu iitwayo bilirubini
Bilirubini ni dutu ya manjano ambayo mwili wako hutengeneza wakati unavunja seli nyekundu za damu zilizozeeka au kuharibika. Ini lako huchakata bilirubini hiyo ili kuiondoa mwilini mwako. Linaondoa bilirubini kwa kuichanganya kwenye nyongo, juisi ya kumeng'enya chakula, na kuiweka kwenye matumbo yako.
Homa ya nyongo ya manjano inaweza kutokea tatizo likitokea kwenye ini lako au katika tyubu zinazobeba nyongo kuelekea kwenye matumbo. Bilirubini hukusanyika mwilini mwako na kukufanya ugeuke kuwa manjano.
Ikiwa unaugua homa ya nyongo ya manjano, mwone daktari haraka uwezavyo—homa ya nyongo ya manjano inaweza kuwa dalili ya tatizo kubwa kama vile uharibifu wa ini
Hepatitisi kutokana na virusi ni kisababishi cha homa ya nyongo ya manjano kinachotokea sana, hususan kwa watu wenye umri mdogo ambao wana afya nzuri
Baadhi ya watu wanaougua homa ya nyongo ya manjano huwashwa mwili mzima—dawa zinaweza kusaidia kupunguza mwasho
DKT P. MARAZZI/MAKTABA YA PICHA ZA KISAYANSI
Homa ya nyongo ya manjano haisababishi dalili kubwa kivyake, lakini inaweza kuwa dalili ya matatizo mengine. Homa ya nyongo ya manjano kwa watoto waliozaliwa hivi karibuni ni tofauti na inaweza kusababisha matatizo makubwa kwa watoto.
Ni nini husababisha homa ya nyongo ya manjano?
Homa ya nyongo ya manjano inaweza kutokea iwapo:
Seli nyingi mno nyekundu za damu zimevunjwa mara moja
Ini lako limeharibika na haliwezi kuchakata bilirubini ipasavyo
Kitu kimeziba mifereji yako ya nyongo (neli zinazobeba nyongo kutoka kwenye ini lako kwenda kwenye matumbo wako.)
Visababishi vinavyotokea sana vya uharibifu wa ini vinajumuisha hepatitisi, ugonjwa wa ini unaohusishwa na unywaji wa pombe, na wakati mwingine baadhi ya dawa.
Sababu za kawaida za kuziba kwa mifereji ya nyongo zinajumuisha mawe ya nyongo na uvimbe.
Kwa watu wazee, homa ya nyongo ya manjano husababiswa na mifereji ya nyongo iliyozibwa, na uzibaji huo mara nyingi husababishwa na kansa. Madaktari hushuku kuwa watu wazee walio na homa ya nyongo ya manjano wana kansa ikiwa pia:
Kupungua uzani
Hawana maumivu ya tumbo
Wana uvimbe tumboni
Je, ni zipi dalili za homa ya nyongo ya manjano?
Ngozi kubadilika kuwa ya njano
Macho kuwa na rangi ya njano (sehemu ambayo kwa kawaida huwa nyeupe)
Kuwashwa mwili mzima
Mkojo mweusi na kinyesi chenye rangi nyepesi
Baadhi ya magonjwa yanayosababisha homa ya nyongo ya manjano pia yanaweza kusababisha:
Maumivu ya tumbo
Uchovu
Je, napaswa kumwona daktari lini?
Mwone daktari haraka uwezavyo ikiwa una homa ya nyongo ya manjano pamoja na dalili hizi za tahadhari:
Maumivu makali na ulaini wa tumbo
Mabadiliko katika utendakazi wa akili, kama vile uchovu, woga, au kuchanganyikiwa
Damu kwenye kinyesi chako au kuwa kama lami, kinyesi cheusi
Kutapika damu
Homa
Kuvilia au kuvuja damu kwa urahisi, hali ambayo wakati mwingie husababisha upele wa rangi iliyo kati ya nyekundu na zambarau wenye madoa madogo au makubwa
Kwa watu wazee, dalili za tahadhari zinaweza kuwa ndogo au zisizotambulika kwa urahisi.
Watu wasiopata dalili za tahadhari ambao wanafikiri kuwa huenda wanaugua homa ya nyongo ya manjano wanapaswa kuona daktari ndani ya siku chache.
Je, nitarajie nini ninapokwenda kumwona daktari wangu?
Madaktari watakuuliza maswali kuhusu dalili zako na historia ya afya yako na wafanye uchunguzi wa mwili. Majibu kutoka kwenye historia yako na matokeo ya uchunguzi wa mwili yatawasaidia kubaini sababu ya homa yako ya nyongo ya manjano. Wataagiza vipimo vifanywe panapohitajika.
Je, nitahitaji vipimo gani?
Daktari anaweza kufanya vipimo kama vile:
Vipimo vya damu vya kuangalia ini lako na kuona iwapo limeharibika
Upimaji wa picha kama vile kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti, uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta), au MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku)
Wakati mwingine, uondoaji wa kipande cha tishu ya ini kwa uchunguzi au laparoskopi kwa kutegemea kinachosababisha tatizo lako la ini
Wakati mwingine, vipimo vingine vya damu ili kuangalia tatizo linalosababisha homa yako ya nyongo ya manjano
Katika uondoaji wa kipande cha tishu kwa uchunguzi, daktari ataweka sindano upande wako wa kulia ili achukue sampuli ndogo ya ini lako na kukichunguza kwenye hadubini. Katika upasuaji unaotumia laparoskopi, daktari atakata sehemu ndogo ya tumbo yako kisha aweke tyubu nyembamba ya kuangalia kupitia sehemu iliyokatwa ili kukagua ogani zako.
Je, madaktari wanatibu vipi homa ya nyongo ya manjano?
Madaktari watatibu tatizo linalosababisha.
Mwasho hupungua taratibu kadiri ini linavyopata nafuu. Ikiwa mwasho ni mkali mno, daktari wako anaweza kukupendekezea dawa inayoweza kukusaidia.
Ikiwa kisababishi ni mfereji wa nyongo uliozibwa, tyubu ya kuangalia inayoweza kupindika (endoskopi) inaweza kutumiwa kuufungua.