Shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2023

Ni nini maana ya shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal?

Mshipa wa portal ni mshipa mkubwa wa damu unaoleta damu kutoka kwenye matumbo yako kwenda kwenye ini lako.

Haipatensheni ni neno la kimatibabu linalomaanisha shinikizo la juu la damu

Kwa hivyo shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal ni shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wako wa lango.

  • Watu wengi hupata shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal kutokana na kirosisi (ugonjwa wa ini ambapo tishu za kovu huchukua nafasi ya tishu ya kawaida ya ini)

  • Shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal ni hatari kwa sababu linaweza kusababisha kuvuja damu kwenye tumbo na umio lako (tyubu inayounganisha koo na tumbo yako)

  • Dawa zinaweza kupunguza shinikizo la damu kwenye mshipa wako wa portal

  • Utahitaji matibabu ya dharura iwapo unavuja damu kwenye tumbo na umio lako

Usambazaji wa Damu kwenye Ini

Ni nini husababisha shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal?

Shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal husababishwa na:

Kirosisi ni hali ya kuwepo kwa makovu mabaya kwenye ini. Makovu hayo huzuia damu isiingie kwenye ini na kuongeza shinikizo katika mishipa ya damu inayokwenda kwenye ini. Unaweza kupata kirosisi kutokana na magonjwa sugu ya ini kama vile hepatitisi C ya muda mrefu na ugonjwa wa ini unaohusishwa na unywaji pombe.

Je, ni yapi matatizo yatokanayo na shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal?

Tatizo kuu ni:

  • Kuvuja Damu

Shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa lango hulazimisha damu kuingia kwenye mishipa mingine ya damu. Mishipa hii mingine ya damu inajumuisha ile iliyo kwenye sehemu ya tumbo na umio lako (tyubu inayobeba chakula kwenda kwenye tumbo yako). Mishipa hii ya damu hufura kutokana na damu nyingi, hali inayoweza kuifanya ivuje damu kwa urahisi. Kuvuja damu kwenye mishipa hii kunaweza kuwa hatari na hata kusababisha maafa.

Je, ni zipi dalili za shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal?

Shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal halisababishi dalili kivyake, lakini athari zake zinaweza kusabbaisha dalili:

  • Kuvimba na kuhisi kana kwamba tumbo limekazwa kutokana na majimaji yaliyojaa humo (ugonjwa wa tumbo kujaa maji)

  • Mishipa iliyovimba kwenye tumbo lako

Shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal linaposababisha kuvuja damu kutoka kwenye tumbo na umio lako, huenda ukapata dalili zifuatazo:

  • Kutapika damu au vitu vyeusi vinavyofanana na machicha ya kahawa

  • Kinyesi (haja kubwa) cheusi kinachofanana na lami

  • Kuvuja damu kwenye tundu la haja kubwa (sehemu ambayo kinyesi hutokea)

Huenda pia ukawa na dalili za ini kushindwa kufanya kazi kama vile:

Madaktari wanawezaje kujua kama nina shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal?

Madaktari husuku kuwa una shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal ikiwa una:

  • Ugonjwa wa ini, hususan ikiwa ugonjwa wa ini ulisababisha kirosisi

  • Mishipa iliyovimba kwenye tumbo lako

Hakuna vipimo vyovyote mahususi vya shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal, lakini madaktari wanaweza kufanya vipimo kwenye ini lako, ikiwa ni pamoja na:

Ikiwa unavuja damu, madaktari wataangalia kupitia koo yako kwa kutumia tyubu inayopindika (endoskopi). Endoskopi itawawezesha kuona sehemu halisi ya umio na tumbo lako ambapo damu inavuja. Kisha wataweza kutibu tatizo hilo la kuvuja damu.

Je, madaktari wanatibu vipi shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal?

Kuvuja damu kwenye mishipa ya tumbo na umio ni dharura ya kimatibabu. Madaktari hutibu hali hii ya kuvuja damu kwa:

  • Kukupa dawa za kupunguza uvujaji wa damu

  • Kukuongezea damu

  • Kufunga mishipa inayovuja damu kwa kutumia kanda za elastiki au klipu (kwa kutumia endoskopi)

Ili kuzuia kuvuja damu kwenye mishipa ya tumbo na umio, madaktari hutumia:

  • Dawa za kupunguza shinikizo la damu

  • Uwekaji wa tyubu kwenye ini ili kuunganisha mshipa wa portal na mshipa wa ini (uunganishaji wa kukwepa) ambao hupunguza shinikizo kwenye mshipa wa portal ini

  • Upasuaji wa kupunguza shinikizo kwenye mshipa wa portal kwa kuelekeza damu kwingine ili isipitie kwenye ini (uunganishaji wa kukwepa ini)

  • Kama chaguo la mwisho, upandikizaji wa ini (upasuaji wa kuondoa ini linalofeli na kuweka jingine lenye afya kutoka kwa mtu aliyechanga)