Ini ni ogani kwenye sehemu ya juu kulia ya tumbo yako. Ini hufanya vitu vingi muhimu:
Huvunjavunja kemikali na dawa
Hutengeneza kiowevu cha kumeng'enya chakula kiitwacho nyongo
Hutoa dutu nyingi muhimu, ikiwa ni pamoja na zile zinazofanya damu yako igande unapovuja damu
Ni nini maana ya ini kushindwa kufanya kazi?
Ini kushindwa kufanya kazi ni wakati ini lako limeacha kufanya kazi vizuri. Hali ya ini kushindwa kufanya kazi inaweza kuathiri jukumu moja au zaidi linalotekelezwa na ini lako.
Hali ya ini kushindwa kufanya kazi hutokea wakati sehemu kubwa ya ini lako imeharibika
Magonjwa fulani, dawa fulani na pombe inaweza kuharibu ini lako
Watu walio na ini lililoshindwa kufanya kazi wanaweza kuugua homa ya nyongo ya manjano (ngozi na macho ya manjano)
Hali ya ini kushindwa kufanya kazi inaweza kutokea kwa siku chache tu au kwa miaka kadhaa
Tatizo la ini kushindwa kufanya kazi linaweza kuwa hatari
Wakati mwingine upandikizaji wa ini huhitajika
Ni nini husababisha tatizo la ini kushindwa kufanya kazi?
Hali ya ini kushindwa kufanya kazi hutokea wakati sehemu kubwa ya ini lako imeharibika.
Ini lako linaweza kuharibiwa na magonjwa kama vile:
Hepatitisi inayotokana na virusi (kuvimba kwa ini kunakosababishwa na virusi)—inayotokea sana ni hepatitisi B
Kirosisi (ugonjwa wa ini ambapo tishu za makovu huchukua nafasi ya tishu za kawaida za ini)
Ini lako linaweza pia kuharibiwa kutokana na kutumia kiwango kikubwa cha vitu fulani:
Dawa kama vile acetaminophen, inayosababisha sumu ya acetaminophen
Pombe
Je, ni zipi dalili za ini kushindwa kufanya kazi?
Dalili za ini kushindwa kufanya kazi zinaweza kujumuisha:
Kuhisi uchovu, udhaifu au kichefuchefu
Homa ya nyongo ya manjano (ngozi na sehemu nyeupe za macho kugeuka kuwa manjano)
Kuvuja damu na kuchubuka kwa urahisi zaidi
Kuvimba kwenye eneo la tumbo kutokana na kujaa kwa majimaji (ugonjwa wa tumbo kujaa maji)
Kizunguzungu na kuchanganyikiwa (matatizo ya akili yanayohusiana na ini)
Kuongezeka kwa uwezekano wa kupata maambukizi kwa sababu ya mfumo dhaifu wa kingamwili
Harufu nzuri ya mdomo, kama ya matunda
Kutapika damu
Kinyesi (haja kubwa) chenye damu
Madaktari wanawezaje kujua iwapo nina tatizo la ini kushindwa kufanya kazi?
Madaktari huangalia:
Vipimo vya damu ili kukagua utendakazi wa ini lako na kubaini kinachosababisha ini lako kushindwa kufanya kazi
Vipimo vya mkojo, vipimo vya damu, na eksirei za kifua ili kuona iwapo tatizo la ini kushindwa kufanya kazi linaathiri sehemu zingine za mwili wako
Je, madaktari wanatibu vipi tatizo la ini kushindwa kufanya kazi?
Hakuna matibabu yanayoweza haswa kufanya ini lako lipone. Hata hivyo, madaktari watakushauri ufanye mambo ya kupunguza matatizo kwenye ini lako:
Kutokunywa pombe au dawa zinazoweza kudhuru ini lako
Kula kiwango kidogo cha nyama nyekundu, samaki, jibini na mayai
Kula protini zaidi za mboga (kama vile soya)
Kula kiasi kidogo cha chumvi (kwa kuepuka kula vyakula vyenye chumvi nyingi na kutoongeza chumvi kwenye chakula)
Ina lako likidhoofika kwa haraka, madaktari watakutibu hospitalini. Matibabu yanaweza kujumuisha:
Viowevu kupitia kwenye mshipa ili kupandisha shinikizo la damu yako
Haluli (dawa za kukusaidia kutoa kinyesi) au enema (majimaji yanayosukumwa kwenye matumbo yako kupitia kwenye tundu la haja kubwa ili kukusaidia kutoa kinyesi)—husaidia kuondoa vitu vyenye sumu (toksini) mwilini mwako
Glukosi (aina ya sukari) unayopewa kupita mshipa (IV), ikiwa kiwango cha sukari kwenye damu yako kiko chini
Kuongezewa damu au kupewa dawa za kusaidia kugandisha damu yako ikiwa unavuja damu
Tyubu ya kupumulia na mashine ya kusaidia kupumua (kifaa chenye mitambo ya kupitisha hewa) ikiwa una matatizo makubwa ya kushindwa kupumua
Upandikizaji wa ini (upasuaji wa kuondoa ini linalofeli na kuweka jingine lenye afya kutoka kwa mtu aliyechanga) unaweza kurekebisha utendakazi wa ini. Hata hivyo, upandikizaji wa ini haufai kwa kila mtu aliye na ini lililoshindwa kufanya kazi.