Maambukizi ya Ghafla ya Homa ya Ini

Imepitiwa/Imerekebishwa May 2023

Ni nini maana ya maambukizi ya ghafla ya homa ya ini?

Maambukizi ya ghafla ya homa ya ini ni uvimbe (kufura) kwenye ini ambao huja kwa haraka na kutoweka kwa haraka. Maambukizi ya ghafla ya homa ya ini wakati mwingine huwa homa ya ini inayodumu kwa muda mrefu. Homa ya ini ya aina hii hudumu kwa muda mrefu.

  • Maambukizi ya ghafla ya homa ya ini mara nyingi husababishwa na virusi.

  • Dalili zako zinaweza kuwa ndogo zinazofanana na za homa ya mafua au dalili kali na za kutishia maisha

  • Madaktari hufanya vipimo vya damu ili kubaini iwapo una maambukizi ya ghafla ya homa ya ini na virusi vilivyoisababisha

  • Unaweza kupata chanjo (sindano) za kuzuia baadhi ya aina za homa ya ini inayosababishwa na virusi

  • Shughuli fulani, kama vile kuweka chale au kutoboa sehemu za mwili, kutumia kwa pamoja sindano za kudungia dawa za kulevya, au kuwa na wenzi wengi wa ngono, huongeza hatari yako ya kuugua homa ya ini

Ni nini husababisha homa ya ini ya ghafla?

  • Kuna aina 5 za virusi vya hepatitisi ambavyo vinaweza kusababisha maambukizi ya ghafla ya homa ya ini na zinajulikana kama A, B, C, D na E

  • Virusi vya Hepatitisi A ndivyo vinavyotokea sana kama kisababishi cha maambukizi ya ghafla ya homa ya ini

  • Kisababishi cha pili kinachotokea sana ni Hepatitisi B

Virusi tofauti vya hepatitisi huenezwa kwa njia tofauti:

  • Hepatitisi A: kupitia chakula au maji yaliyochafuliwa na kinyesi (haja kubwa) kutoka kwa watu walioambukizwa

  • Hepatitis B: kupitia kugusana na damu au majimaji ya mwili ya watu walioambukizwa, kwa mfano, kwa kushiriki tendo la ngono au kutumia sindano kwa pamoja (kudungia dawa za kulevya au kuweka chale)—pia, mwanamke mjamzito anaweza kuambukiza mtoto wake virusi vya hepatitisi B

  • Hepatitis C: kupitia kugusana na damu ya watu walioambukizwa, kwa mfano, kwa kutumia sindano kwa pamoja—kushiriki tendo la ngono hakusambazi virusi vya hepatitisi C

  • Hepatitisi D: Sawa na hepatitisi B

  • Hepatitisi E: Sawa na hepatitisi A

Ni dalili zipi za maambukizi ya ghafla ya homa ya ini?

Huenda usionyeshe dalili zozote au huenda ukaonyesha dalili kama vile:

  • Kutohisi njaa kama kawaida

  • Homa, kutapika, au kuhisi kichefuchefu tumboni

  • Maumivu kwenye sehemu ya juu kulia ya tumbo yako, ambapo ini lako linapatikana

  • Ngozi na sehemu nyeupe za macho yako kugeuka kuwa manjano (homa ya nyongo ya manjano)

  • Mkojo mweusi

  • Kuchukia sigara, ikiwa unavuta

Dalili nyingi kwa kawida huwa zinatoweka ndani ya siku 3 hadi 10 na unaanza kujisikia vizuri. Hali ya ngozi na macho yako kuwa ya manjano inaweza kudumu kwa wiki 2 hadi 4.

Matatizo ya hepatitisi kali ni yapi?

Watu wengi wanakuwa hawana matatizo lakini wakati mwingine:

Madaktari wanawezaje kujua kuwa nina hepatitisi kali?

Madaktari watafanya:

  • Vipimo vya damu ili kuona jinsi ini lako linavyofanya kazi na kuangalia ikiwa una virusi vya hepatitisi

  • Mara kwa mara, wataondoa kipande cha tishu ya ini lako kwa ajili ya uchunguzi kwa kuchukua sampuli yake kwa sindano ili kuichunguza chini ya hadubini

Je, madaktari wanatibu vipi hepatitisi kali?

Ikiwa una hepatitisi kiasi ya virusi kali:

  • Pengine utapona ndani ya wiki 4 hadi 8 bila matibabu maalumu

  • Daktari wako atakuwambia usinywe pombe au kutumia dawa fulani hadi uwe mwenye afya

Ikiwa una hepatitisi ya virusi kali sana, huenda ukahitaji:

  • Kuhudumiwa hospitalini

  • Dawa zinazosaidia kuua virusi

  • Kwa nadra, kubadilisha ini

Je, ninawezaje kuzuia hepatitisi kali?

Unaweza kuchomwa sindano (chanjo) ili kuzuia maambukizi ya hepatitisi A au B. Watu nchini China pia wanapata chanjo ya hepatitisi E.

Ikiwa umegusana na mtu mwenye hepatitisi A au B na hujapata chanjo, unaweza kuchoma sindano (chanjo au globulini ya kinga) ambayo inasaidia kuzuia maambukizi hayo.

Unaweza pia kusaidia kuzuia hepatitisi kali ya virusi ikiwa:

  • Unanawa sana mikono yako kabla hujagusa chakula

  • Hushiri miswaki, nyembe na vitu vingine ambavyo vinaweza kuwa na damu ya watu wengine

  • Unafanya ngono salama, kama vile kutumia kondomu

  • Punguza idadi ya watu ambao unafanya nao ngono

  • Usishiriki sindano za kudunga dawa