Hepatitisi sugu ni nini?
Hepatitisi sugu ni uvimbe (kuvimba) wa ini ambao unadumu kwa miezi 6 au zaidi. Hepatitisi sugu kwa kawaida inatokana na hepatitisi kali lakini huenda usijue ulipata hepatitisi kali.
Kwa kawaida, hepatitisi sugu inasababishwa na virusi vya hepatitisi B au C au dawa fulani
Watu wengi hawaoneshi dalili lakini baadhi ya watu wanaweza kujihisi kuumwa kidogo, kuchoka au hawahisi njaa
Wakati mwingine, hepatitisi sugu inaweza kusababisha matatizo kadiri muda unavyokwenda, kama vile kirosisi
Hepatitisi sugu inaweza kudumu kwa miaka kadhaa
Madaktari wanaweza kutibu hepatitisi sugu kwa kutumia dawa
Je, nini kinasababisha hepatitisi sugu?
Hepatitisi sugu kwa kawaida inasababishwa na maoja wapo kati ya virusi vya hepatitisi, hasa hepatitisi B na C.
Hepatitisi sugu inaweza pia kusababishwa na:
Aina fulani za dawa, hasa ikiwa utazitumia kwa muda mrefu
Magonjwa fulani, kama vile hepatitisi ya ulevi, ugonjwa wa ini lenye mafuta, na mengineyo
Mmenyuko wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili (mwili unaposhambulia ini)
Madaktari hawajui hasi kile kinachosababisha hepatitisi sugu kwa baadhi ya watu.
Je, dalili za hepatitisi sugu ni zipi?
Karibu watu 2 kati ya 3 wenye hepatitisi sugu wanakuwa nayo taratibu na wanakuwa hawaonyeshi dalili hadi wanapokuwa na kirosisi (ini kuwa na makovu).
Unaweza kuwa na dalili kama vile:
Kujisikia kuumwa kidogo, na kutokuhisi njaa sana
Wakati mwingine, homa na maumivu kiasi kwenye eneo la juu la tumbo lako
Uvimbe kutokana na majimaji kujitengeneza kwenye eneo la tumbo lako (ugonjwa wa tumbo kujaa maji)
Mishipa misogo ya damu kama buibui kwenye ngozi yako (angioma ya buibui)
Viganja vyekundu
Kutofikiria vyema
Kutokwa damu kwa urahisi
Mwasho
Kinyeshi (haja kubwa) chenye harufu mbaya, chenye mafuta na chenye rangi nyeupe
Dalili za mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili kama vile maumivu ya viungo na kwa wanawake kukosa hedhi
Ikiwa una hepatitisi B sugu au hepatitisi C pamoja na kirosisi, unaweza kuwa na saratani ya ini.
Madaktari wanawezaje kujua kuwa nina hepatitisi sugu?
Madaktari watafanya:
Fanya vipimo vya damu
Watachukua sampuli ndogo ya ini lako ili kuichunguza kwenye hadubini (uondoaji wa kipande cha tishu kwa uchunguzi)
Je, madaktari hutibu vipi hepatitisi sugu?
Daktari wako atatibu hepatitisi sugu kwa njia tofauti kulingana na kisababishi:
Ikiwa dawa fulani ndiyo chanzo, daktari wako atakuambia uache kutumia dawa hiyo.
Ikiwa hepatitisi B, C au E ndio chanzo, daktari wako atakupa dawa ya kutibu virusi hivyo
Ikiwa unapata athari ya mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili, daktari wako atakupa kotikosteroidi kupunguza mwako kwenye ini
Ikiwa ini limeshindwa kufanya kazi, huenda ukahitaji kuwekewa ini jingine
Madaktari pia watatibu matatizo yoyote ambayo yamesababishwa na hepatitisi sugu.