Ugonjwa wa Lyme

Imepitiwa/Imerekebishwa Jul 2023

Je, ugonjwa wa Lyme ni nini?

Ugonjwa wa Lyme ni aina fulani ya ugonjwa ambao unaupata baada ya kung'atwa na kupe wenye maambukizi. Unaitwa ugonjwa wa Lyme kwa sababu kwa mara ya kwanza uligudulika huko Lyme, Connecticut.

Aina ya kupe anayeitwa kupe wa kulungu husambaza ugonjwa wa Lyme. Kupe wa kulungu hupata bakteria anayesababisha ugonjwa wa Lyme pale anaponyonya damu ya panya mwenye maambukizi. (Huitwa kupe wa kulungu, kwa sababu kupe hawa hula kupitia kunyonya damu ya kulungu).

  • Una uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa Lyme ikiwa unaishi na kwenda kwenye maeneo yenye miti mingi

  • Kwa kawaida, unapata doa kubwa, jekundu katika sehemu uliyong'atwa na kupe

  • Kwa taratibu doa hukua na kupata pete nyekundu zinazolizunguka kama vile alama ya shabaha au jicho la fahali

  • Pia, ugonjwa wa Lyme unaweza kukufanya upate homa, misuli kuuma, na kuvimba vifundo

  • Ikiwa hutopata matibabu, unaweza kupata matatizo ya muda mrefu kwenye ubongo, neva na vifundo vyako

  • Madaktari hutibu ugonjwa wa Lyme kwa kutumia dawa za kuua bakteria

Je, nini husababisha ugonjwa wa Lyme?

Bakteria wa Borrelia burgdorferi ndiye husababisha ugonjwa wa Lyme. Uking'atwa na kupe wa kulungu, hupati ugonjwa wa Lyme mara moja. Kwa kawaida kupe wa kulingu anapaswa kujipachika kwako kwa anagalau siku moja na nusu.

Kupe wa kulungu ni wadogo kuliko kupe wa mbwa ambao mara nyingi huwakuta kwenye wanyama wako vipenzi.

Kupe kulungu

Je, zipi ni dalili za ugonjwa wa Lyme?

Dalili za ugonjwa wa Lyme zinategemea na hatua ambayo ugonjwa umefikia.

Dalili za mapema zinajumuisha:

  • Kwa kawaida, doa kubwa, jekundu lililovimba mahali ambapo kupe amekung'ata

  • Doa jekundu huongezeka, na kuwa wazi katika sehemu ya kati, na hupata pete nyekundu ambazo hulizunguka (ukurutu wa jicho la fahali)

  • Doa haliwashi wala kuuma, lakini linaweza kuwa na hali ya joto

  • Kwa kawaida doa hupote lenyewe ndani ya wiki 3 hadi 4

Baadhi ya watu wenye ugonjwa wa Lyme huwa hawapati doa au upele/ukurutu kabisa.

Kisha bakteria huanza kusambaa kwenye mwili wako na unaweza kupata dalili kama:

  • Kuhisi uchovu kwa wiki kadhaa

  • Homa, mzizimo na maumivu ya kichwa

  • Shingo iliyokaza na misuli kuuma

  • Vifundo kuuma na kuvimba

  • Wakati mwingine, madoa mengine madogo, mekundu kwenye mwili wako

  • Maumivu ya kichwa na shingo iliyokaza (homa ya uti wa mgongo)

  • Udhaifu katika upande mmoja wa uso wako (Kupooza uso kwa ghafla)

Dalili za baadaye hutokea iwapo hautapatiwa matibabu. Miezi au miaka kadhaa baada ya maambukizi, unaweza kupata dalili kama:

  • Ugonjwa wa baridi yabisi, ukiambatana na kuvimba, maumivu, na kukakamaa kwa vifundo vyako, hasa kwenye magoti

  • Wakati mwingine, ganzi au maumivu ya kuchoma kwenye mgongo, miguu na mikono yako

  • Wakati mwingine matatizo ya hali, kuzungumza, kumbukumbu na usingizi

Je, mdaktari wanawezaje kujua ikiwa nina ugonjwa wa Lyme?

Madaktari hugundua ugonjwa wa Lyme kutegemea:

  • Dalili zako

  • Ikiwa unaishi au ulitembelea eneo ambalo ugonjwa wa Lyme unapatikana sana

  • Kipimo cha damu

Mara nyingi kipimo cha damu huwa hakionyeshi uwepo wa ugonjwa wa Lyme pale unapoumwa kwa mara ya kwanza. Mara nyingi madaktari wanapaswa kurudia kipimo baada ya wiki kadhaa.

Je, madaktari hutibu vipi ugonjwa wa Lyme?

Madaktari hutibu ugonjwa wa Lyme mapema iwezekanavyo ili kuzuia matatizo zaidi. Madaktari watatumia:

  • Dawa za kuua bakteria

  • Dawa za kununua duka la dawa, kama vile ibuprofeni au aspirini, ikiwa una maumivu ya viungo

Je, ninawezaje kuzuia ugonjwa wa Lyme?

Unaweza kuzuia ugonjwa wa Lyme kwa kujaribu kuzuia kung'atwa na kupe:

  • Baki kwenye njia ya miguu na njia pale unapotembea katika maeneo yenye miti mingi na usijisugue kwenye vichaka na magugu

  • Usikae kwenye ardhi au kwenye kuta za mawe

  • Vaa mashati ya mikono mirefu ya rangi isiyokolea na suruali ndefu iliyochomekwa kwenye buti au soksi zako.

  • Puliza vinyunyuzio vya wadudu kwenye ngozi na nguo zako

  • Kagua mwili wako kwa umakini, hasa sehemu zenye nywele, hasa baada ya kutoka katika eneo lenye miti mingi

  • Ondoa kupe yoyote ambaye umemkuta akitambaa kwenye mwili wako mara moja

Iwapo utang'atwa na kupe wa kulungu:

  • Mvute kupe huyo na kumwondoa kwa kutumia kibanio kwa kukamata kichwa chake au mdomo, na si mwili wake (hutakiwi kuminya mwili wake)

  • Usitumie jeli yenye petroli, pombe, au kiberiti kujaribu kuondoa kupe

  • Daktari wako anaweza kukupatia dawa ya kuua bakteria mara moja au anaweza kutazama sehemu ulipong'atwa ili kuona kama umepata dalili za ugonjwa wa Lyme