Ugonjwa wa Baridi Yabisi ya Idiopathiki wa Watoto (JIA)

Imepitiwa/Imerekebishwa Feb 2023

Ugonjwa wa baridi yabisi ni kikundi cha magonjwa ambayo hufanya viungo vyako kuuma, kuvimba, na kugeuka nyekundu Kuna aina nyingi za ugonjwa wa baridi yabisi.

Ugonjwa wa baridi yabisi ya idiopathiki wa watoto (JIA) ni nini?

Ugonjwa wa baridi yabisi ya idiopathiki wa watoto ni aina nadra ya ugonjwa wa baridi yabisi ambao watoto hupata na ambao hauna kisababishi kinachojulikana.

Ugonjwa wa baridi yabisi ya idiopathiki wa watoto hutokea wakati mfumo wa kingamwili huvamia viungo. Unafanana na ugonjwa wa baridi yabisi ya rumatoidi kwa watu wazima.

  • Viungo vichache au vingi vinakuwa na uchungu na kufura

  • Sehemu zingine za mwili zinaweza kuathiriwa

  • Dalili zinaweza kuja na kupotea

  • Madaktari wanaweza kubaini ikiwa mtoto ana JIA kulingana na dalili, eksirei na vipimo vya damu

  • Matibabu yanaweza kujumuisha madawa na mazoezi

Kuna aina 6 za JIA, zinazotofautiana kwa viungo vinavyoathirika, idadi ya viungo vinavyoathirika, na ikiwa mtoto wako ana dalili zingine.

Je, JIA husababishwa na nini?

JIA ni ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili. Mfumo wa kingamwili ni sehemu ya mfumo wa ulinzi mwilini mwako, ambao hukukinga dhidi ya ugonjwa na maambukizi. Katika ugonjwa wa mfumo wa kingamwili kwenda kinyume na mwili, mfumo wako wa kinga hushambulia sehemu za mwili wako kwa bahati mbaya—katika JIA, mfumo wa kinga wa mtoto hushambulia viungo na wakati mwingine sehemu zingine za mwili wa mtoto. Madaktari hawajui ni nini haswa husababisha mfumo wa kingamwili wa mtoto wako kushambulia viungo.

Je, dalili za JIA ni gani?

Dalili zinaweza kuja na kupotea. Dalili zingine zinahusisha viungo. Dalili zingine zinahusisha sehemu zingine zote za mwili. Watoto walio na JIA hawana dalili zinazofanana. Baadhi wana dalili chache hafifu, wengine wana dalili nyingi kali.

Dalili za viungo zinaweza kuhusisha viungo vichache au vingi, na zinajumuisha:

  • Uchungu na uvimbe

  • Viungo kuwa na joto unapogusa

  • Viungo vigumu, haswa asubuhi

Dalili zinazoathiri sehemu zingine za mwili zinaweza kujumuisha:

  • Homa

  • Uoni hafifu, na macho mekundu ambayo huwa chungu kwa nadra na changamoto ya kuangalia mwanga mkali

  • Upele wa sehemu ya ngozi wenye madoa ambao hauwashi

  • Katika aina kali zaidi ya JIA, vinundu vya limfu vilivyovimba, wengu, na ini

  • Wakati mwingine maumivu na muwasho (uvimbe) wa utando wa mapafu na moyo

Je, matatizo yanayoambatana na JIA ni yapi?

Huenda watoto walio na JIA kali wasikue kwa kawaida:

  • Mkono mmoja au mguu unaweza kuwa mrefu au mfupi kuliko ule mwingine

  • Iwapo JIA itaathiri mfupa wa taya, kidevu cha mtoto wako kinaweza kuonekana mdogo mno

Je, madaktari wanawezaje kubaini ikiwa mtoto wangu ana JIA?

Hakuna vipimo mahususi vya JIA. Huenda daktari ataangalia:

  • Dalili za mtoto wako

  • Vipimo fulani vya damu

  • Eksirei

Hata ikiwa mtoto wako hana dalili za macho, daktari wa macho anapaswa kuchunguza macho ya mtoto wako ili kuangalia kufura kwa sehemu za jicho.

Je, madaktari hutibu vipi JIA?

Hakuna tiba ya JIA, lakini matibabu yanaweza kufanya mtoto ahisi vizuri zaidi. Baadhi ya dawa mpya za ugonjwa wa baridi yabisi zinaweza pia kusaidia kuzuia matatizo, kama vile ulemavu wa viungo na ukuaji dhaifu.

Madaktari hutibu JIA kwa kutumia:

  • Dawa zinazopunguza maumivu na kuvimba

  • Wakati mwingine, wanadunga sindano zenye dawa kwenye kiungo

  • Dawa za vitone za macho ikiwa macho ya mtoto wako yameathiriwa

Huenda madaktari pia wakapendekeza:

  • Tiba maungo na mazoezi

  • Wakati mwingine, kuweka vibanzi ili kuweka wima viungo vya mtoto wako

  • Uchunguzi wa macho mara kadhaa kwa mwaka