Ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo (OA)

Imepitiwa/Imerekebishwa Sept 2024
Nyenzo za Mada

Ugonjwa wa baridi yabisi ni magonjwa ambayo husababisha viungo kupata maumivu, kuvimba na kuwa vyekundu. Kuna aina nyingi za ugonjwa wa baridi yabisi.

Ni nini maana ya kudhoofika kwa viungo?

Kudhoofika kwa viungo ni aina inayotokea sana ya ugonjwa wa baridi yabisi. Katika tatizo la kudhoofika kwa viungo, gegedu iliyo kwenye viungo vyako hudhoofika taratibu.

  • Tatizo la kudhoofika kwa viungo mara nyingi huanza kwa watu walio na umri wa kati ya miaka 40 na 50 na huathiri takribani kila mtu kufikia umri wa miaka 80

  • Huenda ukawa na maumivu, kuvimba na kukakamaa kwa viungo (hususani asubuhi)

  • Kuwa na uzani kupita kiasi na kufanya kazi inayotumia viungo hivyo mara kwa mara huongeza hatari yako ya kupata tatizo la kudhoofika kwa viungo ukiwa bado hujazeeka

  • Madaktari huangalia dalili zako na kufanya eksirei ili kubaini iwapo una tatizo la kudhoofika kwa viungo

  • Madaktari hutibu tatizo la kudhoofika kwa viungo kwa mazoezi, dawa, na wakati mwingine upasuaji

Je, nini husababisha ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo?

Kudhoofika kwa viungo husababishwa na mkazo kwenye kiungo. Mkazo huo hufanya giligili idhoofu kwenye kiungo. Giligili ni tishu nyororo na thabiti ya kinga iliyo mwishoni mwa mifupa katika kila kiungo. Giligili hukinga mifupa na kuiwezesha ipitane kwa mtelezo bila msuguano:

  • Giligili inapodhoofika, mifupa iliyo kwenye kiungo huanza kusuguana na kusababisha madhara

  • Kutokana na madhara kwenye gegedu na mfupa, kiungo hakiwezi tena kusogea kwa ulaini wala kufanya kazi vizuri

Una hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo iwapo:

  • Wewe ni mwanamke mzee

  • Una uzani mkubwa kupita kiasi

  • Tayari umejeruhiwa kwenye kiungo

  • Una misuli dhaifu au neva zilizoharibiwa kwenye miguu au mikono yako

  • Unafanya kazi inayoweka mkazo kwenye viungo vyako

  • Una wanafamilia wanaougua ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo

Je, dalili za ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo ni zipi?

Dalili za kawaida ni:

  • Maumivu au mchonyoto wa ndani unaozidi unapoweka mkazo kwenye kiungo (kwa mfano unaposimama)

  • Kukakamaa kwa viungo vyako baada ya kulala au kukaa tuli ambako kunatoweka baada ya takrinani dakika 30 za kutembea huku na kule

  • Viungo ambavyo havinyooki au kuinama kikamilifu

  • Viungo vinavyosaga, kuparuza, au kulia unapovisogeza

  • Viungo vya vidole vilivyofura

  • Viungo vilivyolegea visivyo thabiti

Kwa kawaida kudhoofika kwa viungo huanza kwenye kiungo kimoja au viungo vichache. Tatizo hilo huzidi polepole baada ya dalili kuanza. Watu wengi walio na tatizo la kudhoofika kwa viungo huenda wasiweze kufanya kila kitu walichofanya hapo awali.

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo?

Madaktari wanaweza kujua iwapo una ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo kulingana na dalili zako na kwa kufanya uchunguzi. Huenda daktari pia:

  • Eksirei

  • Vipimo vya damu vya kuhakikisha kuwa huna magonjwa mengine

  • Vipimo vya kuangalia majimaji ya kiungo, ikiwa kiungo kimevimba

Je, madaktari hutibu vipi ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo?

Malengo makuu ya matibabu ni:

  • Kupunguza maumivu yako

  • Kuhakikisha kuwa unaweza kunyumbulisha viungo vyako

  • Kuhakikisha kuwa viungo vyako vinafanya kazi na unaweza kutembea

Dawa, pamoja na mazoezi na tiba ya mazoezi, zinaweza kusaidia kudhibiti dalili zako.

Dawa

Madaktari wanaweza kupendekeza dawa za kudhibiti maumivu za kununua dukani, kama vile:

  • Acetaminophen

  • Dawa za kupunguza uvimbe zisizo na steroidi (NSAID) kwa kinywa

  • Krimu za NSAID zinaweza kupakwa kwenye ngozi

Madaktari wanaweza pia kupendekeza dawa zenye nguvu zaidi za kudhibiti maumivu au kudunga dawa, kama vile kotikosteroidi, kwenye kiungo chenye maumivu kilichovimba.

Mazoezi

  • Mazoezi ya kila siku ya kujinyoosha (kama vile yoga)

  • Mazoezi ya kuongeza nguvu (kama vile kuinua vitu vizito)

  • Mazoezi rahisi ya viungo vya kuongeza hewa (kama vile kutembea, kuogelea, au kuendesha baiskeli)

  • Mazoezi ya majini ili kuepuka kukaza kiungo

Matibabu mengine

  • Matibabu ya kimwili

  • Tiba ya mazoezi ya kikazi (ili kukuwezesha kufanya shughuli za kila siku)

  • Zana za usaidizi (kama vile viti vya kunyoosha mgongo, vifaa vya kuweka kwenye viatu, au fimbo za kutembelea)

  • Kushinikiza kwa vitu baridi au pedi zenye joto

  • Kukandwa

  • Kuepuka vitanda na viti vyororo kupita kiasi

Matibabu mengine yasipofanya kazi, huenda daktari akakupendekezea upasuaji wa kubadilisha kiungo kilichoharibika vibaya.