Ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasisi

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Ugonjwa wa baridi yabisi ni magonjwa ambayo husababisha viungo kupata maumivu, kuvimba na kuwa vyekundu. Kuna aina nyingi za ugonjwa wa baridi yabisi.

Ni nini maana ya ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis?

Ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis ni aina ya ugonjwa wa baridi yabisi unaoathiri baadhi ya watu walio na psoriasis. Psoriasis ni tatizo la ngozi linalosababisha kutokea kwa upele mwekundu unaochunuka na kucha nene zenye mashimo.

  • Ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis unaweza kuathiri kiungo chochote, lakini kwa kawaida unaanza kwenye uti wa mgongo, mikono, na miguu

  • Madaktari huangalia dalili zako ili kubaini iwapo una ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis

  • Wakati mwingine dawa zinaweza kusaidia

Je, nini husababisha ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis?

Ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis hutokea wakati mfumo wa kingamaradhi wa mwili wako (ogani na seli zinazopambana na maambukizi) unashambulia viungo vyako na tishu zilizo karibu. Madaktari hawajui hasa kwa nini hali hii hutokea.

Kuna uwezekano zaidi kwamba utapata ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis ikiwa mtu katika familia yako ana ugonjwa huo.

Ni zipi dalili za ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis?

Unaweza kuwa na dalili moja au zaidi kati ya zifuatazo:

  • Viungo vya ncha za vidole vyako vya mikono na miguu kuvimba (kufura, wekundu, na kuwa na joto)

  • Maumivu kwenye sehemu ya nyuma ya kifundo cha mguu (Achilles tendinitis) au wayo wa mguu (plantar fasciitis)

  • Maumivu ya mgongo

  • Maumivu kwenye nyonga na magoti yako

  • Viungo vilivyovimba kwa muda mrefu vinaweza kuharibika umbo

Psoriasis husababisha upele. Upele unaweza kutokea kabla au baada ya maumivu ya viungo. Huenda usigundue kuwa una upele iwapo umefichwa kwenye ngozi ya kichwa, kitovu, au mikunjo ya ngozi yako. Dalili za ngozi na viungo wakati mwingine hutokea na kutoweka kwa pamoja, lakini mara nyingi ama dalili za ngozi au za viungo huwa mbaya zaidi.

Madaktari wanawezaje kujua iwapo nina ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis?

Madaktari wanaweza kujua iwapo una ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis kulingana na dalili zako na historia ya familia na kwa kufanya uchunguzi. Daktari pia atakupima:

  • Eksirei ili kuona jinsi viungo vyako vimeharibika

  • Vipimo vya damu vya kuhakikisha kuwa huna aina nyinginezo za ugonjwa wa baridi yabisi

  • Wakati mwingine vipimo vya kuangalia majimaji ya kiungo, ikiwa kiungo kimevimba

Madaktari hutibu vipi ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis?

Madaktari watapendekeza dawa za kudhibiti upele na kupunguza uvimbe kwenye viungo vyako. Dawa zinazoweza kusaidia ugonjwa wa baridi yabisi ya psoriasis zinajumuisha:

  • Acetaminophen na dawa za kupunguza uvimbe zisizo na steroidi (NSAID) kwa kinywa au krimu zinazoweza kupakwa kwenye ngozi katika sehemu za viungo vinavyouma

  • Sindano za kotikosteroidi kwenye kiungo

  • Sindano za dawa zinazozuia mfumo wa kingamwili usishambulie viungo na pia kusaidia kumaliza upele wa psoriasis

Madaktari wanaweza kupendekeza tiba ya mazoezi ya mwili na mazoezi ili kuhakikisha kuwa unaweza kusogeza viungo vyako.

Matibabu mengine yasipofanya kazi, huenda daktari akakupendekezea upasuaji wa kubadilisha kiungo kilichoharibika vibaya.