Spondiliti Inayofungana

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Ugonjwa wa baridi yabisi ni magonjwa ambayo husababisha viungo kupata maumivu, kuvimba na kuwa vyekundu. Kuna aina nyingi za ugonjwa wa baridi yabisi.

Ni nini maana ya spondiliti inayofungana?

Spondiliti inayofungana ni aina ya ugonjwa wa baridi yabisi unaofanya uti wako wa mgongo ukaze na usababishe maumivu.

  • Spondiliti inayofungana, kando na kuathiri uti wako wa mgongo, pia husababisha kufura, kukakamaa, na maumivu kwenye viungo vyako vikubwa, vidole vya mikono na vya miguu

  • Wakati mwingine inaweza kuathiri sehemu zingine za mwili wako, ikiwa ni pamoja na macho, mapafu, na mishipa fulani ya damu

  • Madaktari wanaweza kujua iwapo una spondiliti inayofungana kulingana na dalili na eksirei

  • Dawa zinaweza kusaidia kupunguza maumizu yako na kukakamaa

Spondiliti inayofungana hutokea kwa wanaume mara 3 zaidi kuliko inavyotokea kwa wanawake. Inaanza kwa watu walio na umri wa kati ya miaka 20 na 40.

Je, nini husababisha spondiliti inayofungana?

Madaktari hawajui haswa kinachosababisha spondiliti inayofungana.

Kuna uwezekano zaidi kwamba utapata ugonjwa wa spondiliti inayofungana ikiwa kuna mtu katika familia yako aliye na ugonjwa huo.

Je, ni zipi dalili za spondiliti inayofungana?

Dalili za kawaida ni:

  • Maumivu ya mgongo yanayozidi wakati wa usiku na asubuhi

  • Kukakamaa kwa mgongo asubuhi kunakopungua ukishaanza kushughulisha mwili

Wakati mwingine, ugonjwa wa baridi yabisi hautokei kwenye mgongo wako mwanzoni, na unaanza kwa maumivu kwenye nyonga, magoti, au mabega yako.

Pamoja na maumivu ya mgongo na viungo, kwa ujumla huenda ukajihisi mgonjwa na kuonyesha dalili kama vile:

  • Homa kiasi

  • Kuhisi uchovu mwingi

  • Kukosa hamu ya kula na kupoteza uzani

Baada ya muda, iwapo tatizo la mgongo litazidi, huenda ukapata:

  • Mkao wa kuinama wa kudumu

  • Uti wa mgongo ulionyooka na kukaza

  • Shinikizo kwenye neva zinazotoka kwenye uti wako wa mgongo, hali inayosababisha kufa ganzi, kuwashwa, maumivu na udhaifu kwenye miguu yako

Unaweza pia kupata matatizo yasiyohusiana na mgongo au viungo vyako. Kwa mfano, huenda:

  • Macho kuwa mekundu, kuwasha na wakati mwingine kutoona vizuri (kuvimba kwa uvea)

  • Matatizo ya moyo yanayosababisha maumivu ya kifua, kushindwa kupumua au mdundo usio wa kawaida wa moyo

  • Matatizo ya mapafu yanayosababisha kikohozi na ugumu wa kupumua

Watu wengi walio na spondiliti inayofungana hupata ulemavu wa aina fulani lakini bado wanaweza kuendelea na maisha ya kawaida. Baadhi ya watu, kama wale walio na uti uliokaza zaidi, huwa na ulemavu mbaya zaidi.

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina spondiliti inayofungana?

Madaktari wanaweza kujua iwapo una spondiliti inayofungana kulingana na dalili zako na historia ya familia na kwa kufanya uchunguzi. Daktari pia atakupima:

  • Eksirei ili kuona jinsi viungo vyako vimeharibika

  • Vipimo vya damu

Je, madaktari hutibu vipi ugonjwa wa spondiliti inayofungana?

Madaktari watakupatia dawa za kudhibiti uvimbe zisizo za steroidi (NSAIDs), dawa zingine, na matibabu ili:

  • Kusaidia kupunguza maumivu ya mgongo na viungo

  • Kuhakikisha kuwa unaweza kusogeza viungo vyako

  • Kukomesha au kurekebisha mabadiliko ya uti wako wa mgongo

  • Kukusaidia udumishe mkao unaofaa na uwe na misuli thabiti ya mgongo

  • Kuzuia madhara kwenye ogani zako zingine

Ikiwa una ugonjwa mkali zaidi wa spondiliti inayofungana, madaktari wanaweza kukupatia dawa za kibayolojia. Dawa hizi hufanya kazi kwenye mfumo wako wa kingamwili ili kupunguza uvimbe.

Ikiwa una matatizo ya macho, madaktari wanaweza kupendekeza matone ya macho.

Pamoja na hayo, madaktari wanaweza kupendekeza:

  • Tiba ya mazoezi na mazoezi ya kila siku ili kuimarisha misuli yako na kuzuia uwezekano wa kuinama na kujitweza

  • Kuacha au kuepuka kuvuta sigara

  • Kwa nadra, upasuaji wa kurekebisha nyonga, iwapo nyonga zako zitapata mkao ulioinama