Kupanga uzazi kuna maana ya kuzuia ujauzito (kingamimba). Unaweza kupata ujauzito licha ya kutumia njia za kupanga uzazi, lakini kutumia njia hizo ifaavyo hupunguza uwezekano wa kushika mimba.
Homoni ni viwasilishaji vya kemikali ambavyo sehemu moja ya mwili wako hutuma kwenye sehemu nyingine ya mwili. Viwasilishaji hivi hudhibiti utendakazi wa sehemu muhimu za mwili. Homoni za ngono, kama vile estrogen na progestin, husaidia kudhibiti vipindi vya hedhi na uzazi kwa mwanamke. Madaktari wanaweza kutumia homoni hizi (au aina bandia za homoni hizo) kuzuia ujauzito
Ni nini maana ya mbinu za homoni za kupana uzazi?
Mbinu za homoni za kupanga uzazi hufanya kazi kwa njia mbili:
Huzuia ovari zako zisitoe mayai
Hufanya utelezi ulio kwenye mlango wa kizazi uwe mzito ili mbegu za kiume zisipite
Ikiwa mayai hayatolewi au mbegu za kiume haziweza kuyafikia, huwezi kupata ujauzito.
Mbinu za homoni za kupanga uzazi ni pamoja na:
Dawa za kuzuia mimba
Kiraka cha ngozi
Kijipete cha kutia kwenye uke wako
Kipandikizi
Sindano
Mbinu za homoni za kupanga uzazi hufanya kazi vizuri kwa kiasi gani?
Mbinu za homoni za kupanga uzazi ni mojawapo ya mbinu zenye ufanisi zaidi za kupanga uzazi ukizitumia ipasavyo.
Uwezekano wako wa kuwa mjauzito huongezeka usipotumia tembe zako kwa usahihi, hususan ukikosa kumeza tembe wiki ya kwanza baada ya kupata hedhi.
Ni nani anayeweza kutumia mbinu za homoni za kupanga uzazi?
Wanawake wengi wanaweza kutumia mbinu za homoni za kupanga uzazi.
Hupaswi kutumia dawa za kumeza za kuzuia mimba (tembe) zilizo na estrogen na progestin ikiwa:
Una umri wa miaka 35 au zaidi na unapata maumivu ya kichwa ya kipandauso
Una maumivu ya kichwa ya kipandauso pamoja na dalili tangulizi (dalili zinazotokea kabla ya kipandauso, kama vile kuona mwangaza au kuwa na hisia zisizo za kawaida kwenye ngozi yako)
Una tatizo au umewahi kuwa na tatizo la damu iliyoganda kwenye miguu au mapafu yako
Kuwa na shinikizo la juu la damu
Umekuwa na ugonjwa wa kisukari kwa zaidi ya miaka 20 au ugonjwa wa kisukari ulioathiri figo, neva au macho yako
Una viwango vya juu vya mafuta yaitwayo trigliseridi kwenye damu yako
Una ugonjwa wa moyo
Una umri wa miaka 35 au zaidi na unavuta zaidi ya sigara 15 kwa siku
Umefanyiwa upandikizi wa ogani unaosababisha matatizo
Una ugonjwa wa ini
Umepata homa ya nyongo ya manjano (ngozi na macho ya manjano) ukitumia mbinu ya kupanga uzazi hapo awali
Umewahi kuugua au unaugua saratani ya matiti
Ikiwa umefanyiwa upasuaji wa kupunguza uzani, hupaswi kutumia kidonge, lakini unaweza kutumia kiraka cha ngozi au pete ya kuweka ukeni.
Ni zipi mbinu tofauti za kupanga uzazi za homoni?
Zungumza na daktari wako kuhusu mbinu ya homoni ya kupanga uzazi inayokufaa.
Dawa za kuzuia mimba
Dawa za kuzuia mimba zina progestin na estrogen au progestin pekee ili kukuzuia usiwe mjamzito. Tembe zilizo na progestin pekee hazifanyi kazi vizuri sana. Madaktari kawaida huwapa tu kama huwezi kupokea estrogen
Ni lazima umeze tembe moja kila siku. Ukiruka kumeza tembe, unaweza kupata mimba. Kadiri unavyoruka tembe nyingi, ndivyo uwezekano wako wa kupata mimba unavyoongezeka. Ukiacha kumeza tembe, huenda ukaweza kupata mimba mara moja au inaweza kuchukua miezi kadhaa.
Athari mbaya za kutumia dawa za kuzuia mimba ni pamoja na:
Kuvuja damu nyakati zisizotarajiwa, hususan katika miezi michache ya kwanza ya matumizi
Kuhisi kichefuchefu tumboni, kuvimba tumbo na kutapika
Maumivu kwenye matiti
Damu iliyoganda kwenye miguu au mapafu
Maumivu ya kichwa
Mfadhaiko
Sehemu zenye weusi kwenye ngozi yako (melasma)
Uwezekano mkubwa zaidi wa kuugua saratani ya mlango wa kizazi
Kuongeza uzani
Kiraka cha Ngozi
Kiraka cha ngozi cha kupanga uzazi ni kiraka chembamba kinachonata ambacho huachilia estrogen na progestin ili kukuzuia usipate mimba. Kwa kawaida, unavaa kiraka kwa siku 7 kisha unavaa kingine kipya kwa siku zingine 7. Ukishatumia viraka 3, unasubiri kwa wiki moja kabla ya kuanza tena.
Huenda ukahitaji kutumia mbinu ya ziada ya kupanga uzazi (kama vile kondomu) katika wiki ya kwanza ya kutumia kiraka
Huenda ukapata kuwa ni rahisi kukumbuka kutumia kiraka mara moja kwa wiki kuliko kumeza dawa ya kuzuia mimba kila siku
Athari mbaya zinazotokana na matumizi ya kiraka zinafanana na za tembe
Huenda kiraka kisifanye kazi vizuri sana iwapo una uzani mkubwa kupita kiasi
Huenda ukapata maumivu au mwasho kwenye ngozi yako chini ya kiraka au sehemu iliyo karibu na kiraka
Kijipete cha kutia kwenye uke wako
Kingamimba ya kijipete cha kutia kwenye uke ni kijipete kidogo cha plastiki kinachowekwa kwenye sehemu yako ya uke. Kijipete hicho huachilia estrogen na progestin ili kukuzuia usipate mimba. Kwa kawaida unaacha kijipete hicho ndani yako kwa wiki 3 kisha unakitoa kwa wiki 1. Katika wiki hiyo unaweza kupata hedhi. Baada ya wiki hiyo kuisha, unaweka kijipete kingine. Baadhi ya madaktri hukushauri uache kijipete kikae ndani kwa wiki 5 kisha ubadilishe uweke kipya.
Huenda ukahitaji kutumia mbinu ya ziada ya kupanga uzazi (kama vile kondomu) katika wiki ya kwanza ya kutumia kijipete
Huenda ukapata kuwa ni rahisi kukumbuka kutumia kijipete mara moja kila baada ya wiki 3 hadi 5 kuliko kumeza dawa ya kuzuia mimba kila siku au kuweka kiraka kila wiki
Kwa upande mwingine, kwa kuwa huwezi kuhisi kijipete, ni rahisi kusahahu kukiondoa na kukibadilisha
Athari mbaya zinazotokana na matumizi ya kijipete zinafanana na za kutumia tembe na kiraka
Kipandikizi cha kupanga uzazi
Kipandikizi cha kupanga uzazi ni kijiti kinachotoshana na kijiti cha kiberiti kinachowekwa chini ya ngozi yako na kutoa progestin ili kukuzuia usipate mimba.
Kipandikizi hufanya kazi kwa miaka 3
Mara tu kipandikizi kinapoondolewa, unaweza kupata mimba
Daktari wako ataweka kipandikizi chini ya ngozi yako kwa kutumia kifaa kama sindano na kukiondoa kwa kukata kidogo kwenye ngozi yako
Athari mbaya za kutumia vipandikizi ni pamoja na:
Kutopata hedhi
Kuvuja damu nyakati zisizotarajiwa
Maumivu ya kichwa
Kuongeza uzani
Sindano ya kupanga uzazi
Sindano ya kupanga uzazi ni sindano ya progestin inayofanya kazi kwa muda mrefu ambayo hudungwa kila baada ya miei 3 ili kukuzuia ushipate mimba.
Huenda ikachukua hadi miezi 18 kabla ya kuwa mjamzito baada ya kuacha kudungwa sindano hizo
Athari mbaya za kutumia sindano ni pamoja na:
Kuvuja damu nyakati zisizotarajiwa, hususan mwanzoni
Kutopata hedhi
Kuongeza uzani
Maumivu ya kichwa
Uzito wa mifupa uliopungua (jinsi mifupa yako ilivyo na nguvu na afya)—ingawa uzito wa mifupa hurejea katika hali ya kawaida ukiacha kudungwa sindano