Saratani ya Matiti

Imepitiwa/Imerekebishwa Oct 2023

Saratani ni wakati seli zinakua kwa njia isiyo ya kawaida. Seli za saratani hazifanani wala kufanya kazi kama seli za kawaida na huzidi kuwa nyingi kupita kiasi. Seli za saratani zinaweza kushambulia na kuharibu tishu nzuri zilizo karibu. Wakati mwingine, seli za saratani husafirishwa kwenye sehemu za mwili zilizo mbali na kukua hapo. Saratani iliyoenea kwenye sehemu nyingine ya mwili huitwa kansa enezi. Saratani inaweza kuanza kwenye tishu yoyote ya mwili wako.

Saratani ya matiti ni nini?

Saratani ya matiti ni wakati seli zilizo kwenye matiti yako zimepata kansa Saratani ya matiti mara nyingi hutokea kwenye tezi zinazotengeneza maziwa au kwenye vifereji vya maziwa (tyubu zinazobeba maziwa kutoka kwenye tezi zako za kutengeneza maziwa hadi kwenye chuchu zako).

  • Saratani ya matiti huua wanawake zaidi kuliko saratani nyingine yoyote kando na saratani ya mapafu

  • Wanaume pia wanaweza kupata saratani ya matiti

  • Kujua jinsi matiti yako yalivyo kwa kuonekana na kuhisi kunaweza kukusaidia kugundua saratani ya matiti mapema—zungumza na daktari wako iwapo mojawapo ya matiti yako yanaonekana au yanahisi tofauti

  • Ikiwa mama, dada, au binti yako ana saratani ya matiti, huenda ukawa na uwezekano zaidi wa kuugua saratani ya matiti—zungumza na daktari wako ili ujue wakati unapostahili kufanyiwa uchunguzi (kupimwa)

  • Mamogramu, ambayo ni eksirei ya matiti, ni kipimo cha kawaida cha uchunguzi cha kuangalia iwapo kuna saratani ya matiti kwa wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 40 au walio katika hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti

  • Matibabu huhusisha upasuaji na mara nyingi hujumuisha tiba ya mionzi, tibakemikali, na dawa za kuzuia homoni

Je, nini husababisha saratani ya matiti?

Madaktari hawajui ni kwa nini haswa baadhi ya wanawake huungua saratani ya matiti. Hata hivyo, kuna mambo kadhaa hatarishi. Una uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti iwapo:

  • Una jeni ya BRCA1 au BRCA2, inayosababisha saratani ya matiti

  • Una umri wa zaidi ya miaka 50

  • Umewahi kuugua saratani ya matiti hapo awali

  • Mama, dada, au binti yako aliugua saratani ya matiti

Wanawake ambao hawana sifa hizi hatarishi wanaweza pia kuugua saratani ya matiti.

Dalili za saratani ya matiti ni zipi?

Dalili ya kwanza kwa kawaida ni:

  • Uvimbe usio na maumivu kwenye titi lako

Ikiwa kansa yako imekua:

  • Uvimbe huwa mkubwa na huenda ukahisi kana kwamba ni mgumu na umekwama mahali

  • Ngozi iliyo juu ya sehemu ya uvimbe inaweza kuwa na joto, nyekundu na ifure

  • Ngozi iliyo juu ya sehemu ya uvimbe inaweza kuonekana kana kwamba imebonyea na kufanana na ngozi ya chungwa

Ikiwa saratani ya matiti imeenea kwenye sehemu zingine za mwili, ishara ya kwanza huenda ikawa tatizo kwenye sehemu hiyo ya mwili, kama vile tatizo la kupumua au mfupa dhaifu wenye maumivu.

Madaktari wanawezaje kujua iwapo nina saratani ya matiti?

Ikiwa huna dalili

Kwa sababu saratani ya matiti hutokea sana, madaktari hufanya vipimo vya saratani ya matiti kwa wanawake ambao hawana dalili zozote. Vipimo hivi huitwa vipimo vya uchunguzi.

Wanawake wote wanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti. Kwa wanawake wengi, madaktari huanza uchunguzi katika umri wa miaka 40 au 50. Vipimo vya uchunguzi hufanywa kila baada ya mwaka au kila baada ya miaka 2 hadi kufikia umri wa miaka 75.

Vipimo vya uchunguzi wa saratani ya matiti vinajummuisha:

Mamogramu ni eksirei maalum ya matiti yako. Madaktari huitumia kuangalia madoa yasiyo ya kawaida ndani ya matiti yako. Hivi ndivyo mamogramu inavyofanya kazi:

  • Utavua shati na sidiria yako kisha uvae joho linalofunguka kwenye sehemu ya mbbele

  • Msanifu-ufundi ataweka titi lako juu ya bati la eksirei

  • Kifuniko cha plastiki kitabana juu ya titi lako, ili kulifanya liwe bapa kadiri iwezekanavyo

  • Msanifu-ufundi atapiga picha za eksirei za titi lako kutoka upande wa juu

  • Msanifu-ufundi anaweza kugeuza bati la eksirei na kifuniko cha plastiki ili kupata mwonekano wa upande wa titi lako

Mamogramu ni mojawapo ya njia bora zaidi za kupata saratani ya matiti mapema. Lakini si madoa yote yanayopatikana huwa saratani ya matiti. Utahitaji vipimo vingine kubaini iwapo doa lisilo la kawaida ni saratani ya matiti. Zungumza na daktari wako kuhusu wakati wa kuanza kufanyiwa vipimo vya mamogramu kulingana na umri wako na afya yako.

Tathmini ya matiti ni sehemu ya uchunguzi wa mwili wa mara kwa mara. Wakati wa uchunguzi wa matiti, madaktari hugusa kila titi kwa vidole vyao ili kujaribu kutafuta uvimbe. Pia, watatafuata nodu za limfu zilizopanuka kwenye makwapa yako na juu ya mtulinga.

Uchunguzi wa MRI unaweza kufanywa ikiwa uko katika hatari kubwa ya kuugua saratani ya matiti. MRI ni kipimo kinachotumia sehemu thabiti ya sumaku kuunda picha yenye maelezo ya kina ya ndani ya mwili wako.

Mamografia: chunguzi wa Saratani ya Matiti

Ikiwa una dalili

Ikiwa una uvimbe kwenye titi au dalili nyinginezo za saratani ya matiti, madaktari hufanya vipimo ili kuangalia iwapo una saratani ya matiti:

Kulingana na dalili na matokeo ya vipimo hivi, daktari wako anaweza:

  • Kudunga sindano kwenye uvimbe na kutoa majimaji au sampuli ya tishu

  • Kukukata ngozi ili kuchukua sehemu ya uvimbe na kuichunguza kenye hadubini (uondoaji wa kipande cha tishu kwa uchunguzi)

Baada ya kutambuliwa kuwa una saratani ya matiti

Matokeo ya uondoaji wa kipande cha tishu kwa uchunguzi yakionyesha kuwa kuna seli za kansa, madaktari hufanya vipimo ili kuona iwapo matibabu ya homoni yatasaidia kansa yako. Kwa mfano, madaktari hupima kansa ili kuona kama kuna vichocheo vya estrojeni, projesteroni, na HER2.

Madaktari pia hufanya vipimo ili kuona kama saratani imeenea. Vipimo vinajumuisha:

  • Vipimo vya damu

  • Eksirei ya kifua

  • Wakati mwinine uchunguzi wa mfupa, au uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) wa tumbo lako

Hatua za saratani ya matiti

Hatua hufafanua kiwango ambacho kansa imekua. Hatua hupewa namba kuanzia 0 hadi 4 na herufi A hadi C. Kadiri namba na herufi ya kansa yako ilivyo chini, ndivyo ulivyo na uwezekano mkubwa wa kupona.

Ili kujua hatua, madaktari huzingatia:

  • Ukubwa wa saratani

  • Iwapo imeenea kwenye sehemu za karibu kama vile nodu za limfu kwenye makwapa

  • Ikiwa kansa imeenea kwenye sehemu za mwili zilizo mbali, kama vile mapafu au mifupa

Madaktari hutibu vipi saratani ya matiti?

Madaktari hutibu saratani ya matiti kulingana na aina yake na hatua iliyofikia. Kuna aina kadhaa za matibabu ya saratani ya matiti. Wewe na daktari wako mtaamua aina ya matibabu mnayotaka kufanya.

Upasuaji

Kuna aina 2 kuu za upasuaji wa saratani ya matiti:

  • Upasuaji wa kuhifadhi titi huondoa knsa pekee na kuacha sehemu nyingine ya titi lako

  • Upasuaji wa kutoa titi huondoa titi lako lote na wakati mwingine nodu za limfu kwenye kwapa lako

Baadhi ya upasuaji wa kutoa titi huacha sehemu ya ngozi ya titi kwenye chuchu. Hali hii huifanya iwe rahisi kufanya upasuaji wa kupandikiza titi.

Kupoteza sehemu ya titi au titi lako lote kunaweza kufadhaisha sana. Lakini kitu cha muhimu zaidi ni kutoa kansa yote badala ya kuacha tishu za titi ambazo huenda zikawa na kansa.

Ikiwa titi lako linatakiwa kuondolewa, huenda ukafanyiwa upasuaji wa kupandikiza titi wakati huo huo au baadaye. Kuna aina 2 za upasuaji wa kupandikiza titi:

  • Madaktari wanaweza kuweka kipandikizi cha silikoni au cha maji ya chumvi

  • Madaktari wanaweza kuunda upya titi lako kwa kutumia tishu kutoka kwenye sehemu zingine za mwili, kama vile tumbo yako, mgongo au makalio

Tiba ya mionzi

Tiba ya mionzi hutumia mionzi kutoka kwenye mashine ili kupunguza uvimbe na kuharibu seli za kansa.

  • Madaktari mara nyingi hutoa tiba ya mionzi baada ya kufanya upasuaji ili kupunguza uwezekano wa kansa kurudi

  • Saratani ikirejea kwenye sehemu ya matiti baada ya upasuaji, unaweza kupata tiba zaidi ya mionzi

Tiba ya mionzi inaweza kufanya ngozi yako iwe nyekundu na ipate malengelenge, na huenda ukahisi uchovu kila mahali.

Tibakemikali

Tibakemikali hutumia dawa kuharibu seli za saratani.

  • Madaktari mara nyingi hutoa tibakemikali kabla ya upasuaji ili kupunguza kansa na kuifanya iwe rahisi kuondoa kabisa

  • Unaweza pia kupata tibakemikali baada ya upasuaji au ikiwa saratani yako imeenea

Dawa za tibakemikali zinaweza kukufanya upoteze nywele zako, utapike, uhisi kichefuchefu tumboni, au uhisi uchovu kila mahali. Huenda pia ukapata matatizo ya kupata mimba au uache kupata hedhi.

Dawa za kuzuia homoni

  • Baadhi ya seli za kansa ya matiti huchochewa kukua na estrojeni na projesteroni, ambazo ni homoni za kike zinazozalishwa mwilini

  • Dawa za kuzuia homoni huzuia homoni hizi ili zisifanye uvimbe wako uongezeke

  • Tamoxifen ni dawa inayofahamika sana inayotolewa ili kuzuia homoni ya estrojeni

  • Madaktari wakati mwingine hutumia dawa za kuzuia homoni badala ya tibakemikali

Baada ya matibabu ya saratani ya matiti

Utamwona daktari wako mara kwa mara Kwenye ziara hizi, madaktari wataangalia matiti yako, kifua, shingo, na makwapa ili kuona iwapo kansa imerudi.

Kuwa mwangalifu kwa jinsi matiti yako yanavyokaa na yanavyohisi na umjulishe daktari wako iwapo utagundua mabadiliko yoyote au una dalili yoyote kati ya hizi:

  • Maumivu

  • poteza uzani au kutohisi njaa

  • Mabadiliko katika hedhi zako

  • Kuvuja damu ukeni ambako si sehemu ya hedhi yako ya kila mwezi

  • Uoni hafifu

  • Dalili zingine zozote ambazo si za kawaida au hazitoweki

Ikiwa unapitia wakati mgumu baada ya matibabu yako, zingatia kujiunga kwenye kikundi cha usaidizi au kuzungumza na mshauri wa kisaikolojia.

Itakuwaje matibabu yasipofanya kazi?

Ikiwa una saratani ya matiti yenye makali sana, huenda ukazingatia kuelekeza mawazo yako katika kupata afueni kuliko kujaribu kuishi maisha marefu. Madaktari wanaweza kusaidia kutibu dalili zako.

Mshauri wa kisaikolojia au kiongozi wa kidini anaweza pia kukusaidia kukabiliana na hisia zako.

Ikiwa bado hujafanya hivyo, andika wosia na hati ya kisheria inayobainisha aina ya huduma unazotaka ikiwa huwezi kuwaambia madaktari wewe mwenyewe. Hati hii inaitwa maagizo ya mapema.