Ni nini maana ya majimaji ya chuchu?
Majimaji ya chuchu ni kiowevu kinachotoka kwenye mojawapo wa chuchu zako au zote mbili.
Majimaji haya yanaweza kuwa na rangi kama ya mawingu, nyeupe, yenye damu, au majimaji yasiyo na rangi yoyote
Majimaji ya chuchu ni kitu cha kawaida kwa wanawake—kwa mfano, mwishoni mwa ujauzito au wakati wa kunyonyesha
Majimaji ya chuchu si kitu cha kawaida kwa wavulana na wanaume
Je, ni nini husababisha majimaji ya chuchu?
Visababishi vikuu vya majimaji ya chuchu ni:
Uvimbe tulivu kwenye kifereji chako cha maziwa (uvimbe wa aina hii si kansa)
Vifereji vya maziwa ambavyo vimekuwa vikubwa na kujazwa na majimaji
Mabadiliko ya fibrosisti (hali inayojumuisha maumivu ya matiti, uvimbe wa majimaji kwenye matiti, na uvimbe mwingine wa matiti ambao si kansa)
Maambukizi ya matiti ambayo yana usaha
Visababishi visivyo vya kawaida vya majimaji ya chuchu ni:
Viwango vya juu vya homoni iitwayo prolaktini
Prolaktini ni homoni inayoambia mwili wako utengeneze maziwa ya mama baada ya kupata mtoto. Hata hivyo, prolaktini inaweza kuzalishwa na matatizo fulani ya afya, kama vile matatizo ya tezi dudumio au ini, na dawa fulani.
Ninapaswa kumwona daktari wakati gani kuhusiana na majimaji ya chuchu?
Nenda kwa daktari ndani ya siku 1 au 2 ikiwa una majimaji ya chuchu na dalili za maambukizi:
Wekundu
Kuvimba
Kutoka usaha (kiowevu cha rangi ya kijivu, kijani, manjano au kahawia ambacho ni kizito na kimeshikana)
Mwone daktari ndani ya wiki moja hivi ikiwa una majimaji ya chuchu na:
Yanatoka yenyewe—wakati chuchu yako haijafinywa
Una umri wa miaka 40 au zaidi
Yanatoka kwenye titi moja tu
Majimaji yana damu au rangi ya waridi
Una uvimbe unaoweza kuugusa kwenye titi lako
Wewe ni mwanaume
Je, nitarajie nini ninapokwenda kumwona daktari wangu?
Daktari atakuuliza maswali kuhusu dalili na afya yako. Watafanya uchunguzi, ikijumuisha tathmini ya titi.
Ili kufahamu chanzo cha majimaji yako ya chuchu, madaktari wanaweza kufanya vipimo vingine, kama vile:
Vipimo vya damu ili kuona viwango vyako vya homoni
Kuangalia sampuli ya majimaji yako kwenye hadubini
Kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti (uchunguzi kwa kutumia mawimbi ya sauti kutayarisha picha ya mwendo ya sehemu za ndani za mwili wako) kwa titi lako
Mamogramu (eksirei ya matiti yako) ili kuchunguza iwapo kuna kansa
Madaktari wanatibu vipi tatizo la majimaji ya chuchu?
Madaktari watatibu chanzo cha majimaji yako ya chuchu.
Ikiwa una uvimbe usio na kansa unaosababisha majimaji ya chuchu kutoka kwenye titi moja, madaktari wanaweza kutoa kifereji hicho cha maziwa kwenye titi hilo.