Mabadiliko ya Fibrosisti ya Matiti

Imepitiwa/Imerekebishwa Oct 2023

Ni nini maana ya mabadiliko ya fibrosisti?

Mabadiliko ya fibrosisti ni mkusanyiko wa dalili za matiti unaojumuisha maumivu, uvimbe wenye majimaji (vifuko vidogo vilivyojaa majimaji), na ugumu kwa jumla kwenye matiti yako. Mabadiliko ya fibrosisti kwenye matiti si ugonjwa mmoja.

  • Mabadiliko ya fibrosisti hayasababishi saratani ya matiti

  • Dalili zinaweza kuwa mbaya zaidi katika siku zilizo kabla ya hedhi yako

  • Mabadiliko ya fibrosisti hutoweka baada ya ukomo wa hedhi (unapoacha kupata hedhi)

  • Madaktari wanaweza kufanya vipimo ili kuhakikisha kuwa mabadiliko yako ya fibrosisti si kansa

Una uwezekano mkubwa wa kupata mabadiliko ya fibrosisti ikiwa:

  • Umeanza kupata hedhi (vipindi vya hedhi) katika umri mdogo

  • Umepata mtoto wako wa kwanza katika umri wa miaka 30 au zaidi

  • Hujawahi kupata mtoto

Ni zipi dalili za mabadiliko ya fibrosisti?

  • Uvimbe kwenye matiti yako

  • Wakati mwingine hisia mbaya, ikiwemo uzito, maumivu unapoguswa au maumivu yanayochoma

Madaktari wanatibu vipi mabadiliko ya fibrosisti?

Huenda daktari:

  • Akushauri uvalie sidiria laini, inayokutosha vyema, kama vile sidiria ya wanamichezo

  • Kukuelekeza utumie dawa za maumivu, kama vile acetaminophen

  • Kutoa majimaji yaliyo kwenye uvimbe

  • Kukupatia dawa, kama vile danazol (aina ya homoni za kiume) au tamoxifen (dawa inayozuia estrojeni), ikiwa dalili zako ni kali

Ikiwa una uvimbe mmoja tu au ikiwa unasikika kuwa tofauti na uvimbe mwingine, daktari anaweza:

  • Kuchukua sampuli ya tishu kutoka kwenye uvimbe wa matiti yako na kuiangalia chini ya hadubini (uondoaji wa kipande cha tishu kwa uchunguzi) ili kuhakikisha kuwa si kansa

  • Kufanya upasuaji ili kuuondoa