Saratani ya mapafu ni nini?
Saratani ya mapafu ni saratani ambayo huanzia kwenye mapafu yako.
Saratani ambayo inaanza kukua kwenye viungo vingine inaweza kuenea (kueneza kansa) kwenye mapafu mengine. Saratani ambazo zimeenea kwenye mapafu yako hazichukuliwi kuwa ni saratani za mapafu. Zinachukuliwa kuwa ni saratani za kiungo husika ilipoanzia, kama vile matiti, utumbo mpana au tezi dume.
Uvutaji sigara ndio sababu kuu ya saratani ya mapafu
Dalili moja wapo iliyozoeleka ni kikohozi ambacho hakiondoki, mabadiliko kwenye kikohozi ulichokuwa nacho kwa muda
Saratani ya mapafu inapatikana sana kwa watu walio na umri kati ya miaka 45 hadi 70
Eksirei za kifua zinaweza kuonyesha saratani za mapafu
Saratani ya mapafu inaongoza katika sababu za vifo vitokanavyo na saratani
Aina za saratani ya mapafu ni zipi?
Kuna aina 2 kuu za saratani ya mapafu:
Saratani ya mapafu ya seli isiyo ndogo (imeenea sana)
Saratani ya mapafu ya seli ndogo (haijaenea sana)
Aina zote mbili ni hatari lakini seli ndogo ni hatari zaidi. Kujua aina ni muhimu kwa sababu matibabu yanatofautiana.
Je, nini husababisha saratani ya mapafu?
Kisababishi kikuu cha saratani ya mapafu ni:
Uvutaji sigara, kuvuta sigara kunasababisha karibu visa 85 kati ya 100 vya saratani ya mapafu
Ikiwa utaacha kuvuta sigara hatari yako ya kupata saratani inapungua. Bado unaweza kupata saratani ya mapafu hata kama huvuti sigara.
Visababishaji vingine vya saratani ya mapafu hujumuisha:
Jeni (vinasaba unavyorithi kutoka kwa mzazi au babu/bibi)
Uchafuzi wa hewa
Kuzungukwa na watu wengine wanaovuta sigara au biri (uvutaji sigara mtumba)
Kuvuta hewa yenye dutu inayoweza kusababisha saratani (kama vile asbesto, mionzi au radoni)
Kutumia moto wenye moshi kwa kupika na kupasha joto
Asbesto ni nyuzi za madini zinazotumiwa kuhami majengo ili yahifadhi joto na vitu vingine vya kujengea. Mionzi kwa kawaida inapatikana kwa kiwango kidogo katika mazingira, lakini kukaa sana kwenye mionzi wakati wa eksirei, uchanganuzi wa CT na vipimo vingine vya picha ni tatizo. Radoni gesi yenye miale nunurishi inayotoka ardhini na inaweza kufikia viwango hatari katika sehemu za nyumba zilizojengwa chini ya ardhi
Je, dalili za saratani ya mapafu ni zipi?
Dalili huenda zisionekane kwa muda. Wakati mwingine madaktari wanaiona saratani ya mapafu bila kutarajia wanapofanya eksirei ya kifua kuangalia matatizo mengine.
Watu wanapokuwa na dalili za saratani ya mapafu, kwa kawaida:
Kukohoa
Kikohozi kinakuwa kikavu, lakini wakati mwingine kimelainika. Unaweza kukohoa matone ya damu. Kikohozi huenda kisiwe kibaya, lakini hakiondoki kama kikohozi wakati wa mafua.
Kadiri saratani inavyozidi kuwa kubwa, unaweza kuwa na dalili nyinginezo kama vile:
Kutohisi njaa
Kupunguza uzani
Kuhisi udhaifu na uchovu
Maumivu ya kifua
Saratani ya mapafu mara nyingi huwa ni hatari, hasa ikiwa haitapatikana mapema.
Je, madaktari wanawezaje kujua kuwa nina saratani ya mapafu?
Madaktari wanaweza kushuku uwepo wa saratani ya mapafu kulingana na dalili zako. Ili kuwa na uhakika kwa kawaida watachukua picha ya mapafu yako kwa kutumia:
Ikiwa picha zitaonyesha kitu kama saratani, daktari wako atachukua kipande cha tishu kwa ajili ya uchunguzi. Atachukua kipande cha tishu kutoka kwenye mapafu kupeleka kwa ajili ya vipimo. Kuna njia nyingi za kuchukua kipande cha sampuli ya tishu kwa ajili ya uchunguzi:
Bronkoskopi (iliyozoeleka sana): Daktari ataangalia mapafu yako kwa kutumia hadubiri rahisi ambayo ina zana mwishoni mwake ambazo zinaweza kuchukua kipande kidogo cha tishu
Kuchukua sampuli kwa sindano: Ikiwa madaktari hawawezi kufikia sehemu husika kwa kutumia bronkoskopi, wakati mwingine wanaweka sindano kupitia ngozi yako na kuingia kwenye kifua chako ili kuchukua sampuli
Upasuaji (nadra): Ikiwa njia hizo 2 hazitafanikiwa, madaktari wanaweza kufaya upasuaji, ili kufungua kifua chako waweze kuchukua sampuli
Kwa kuangalia sampuli ya tishu iliyochukuliwa kwa kutumia hadubini, madaktari wako wanaweza kujua iwapo una saratani. Ikiwa una saratani, wanaweza kukuambia ni aina gani.
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa saratani imeenea?
Ikiwa una saratani ya mapafu, madaktari wanafnya vipimo kuona ikiwa saratani imeenea kwenye sehemu nyingine za mwili wako. Vipimo vinaweza kujumuisha:
Ni nani anayepaswa kuchunguzwa kwa ajili ya saratani ya mapafu?
Ikiwa huna dalili zozote unapaswa kufanyiwa vipimo vya saratani ya mapafu ikiwa tu upo katika hatari ya juu. Upo katika hatari ya juu ikiwa:
Ulivuta sigara sana kwa muda mrefu NA
Una umri wa kati au mkubwa zaidi
Madaktari kwa kawaida wanafanya uchanganuzi wa CT kwenye kifua kwa watu wenye hatari ya juu. Kuwapima watu wengine hakuonekani kuwa kunaokoa maisha ya watu.
Madaktari wanatibu vipi saratani ya mapafu?
Mpango wako wa matibabu unategemea aina ya saratani yako ya mapafu, ni mbaya kiasi gani na mahali ilipo kwenye mwili wako.
Madaktari wanatibu saratani ya mapafu kwa kutumia:
Dawa zinazolenga uvimbe
Tiba ya leza (madaktari wanapotumia leza kuhafifisha au kuondoa uvimbe)
Madaktari wanatibu dalili saratani ya mapafu kwa kutumia:
Oksijeni
Dawa zinazokusaidia upumue
Dawa za maumivu
Ninawezaje kuzuia saratani ya mapafu?
Unaweza kuzuia saratani ya mapafu kwa:
Kukaa mbali na watu wanaovuta sigara
Kuepuka dutu zinazojulikana kusababisha saratani