Vifaa vya Kuwekwa Ndani ya Uterasi

Imepitiwa/Imerekebishwa May 2023

Nyenzo za Mada

Vifaa vya kuwekwa ndani ya uterasi (IUD) ni nini?

Kifaa cha kuwekwa ndani ya uterasi (IUD) ni aina ya mbinu ya kuzuia ujauzito. Ni kifaa kidogo cha plastiki chenye umbo la T ambacho daktari anaweza kuweka ndani ya uterasi yako ili kuzuia mimba. Uterasi yako ni mahali ambapo watoto hukaa na kukua kabla hawajazaliwa.

IUD huwekwa kwenye uterasi yako kupitia sehemu yako ya uke (tyubu yenye misuli inayounganisha uterasi yako na sehemu ya nje ya mwili wako, pia inaitwa njia ya uzazi). Uzi wa plastiki huunganishwa kwenye IUD. Uzi huo hukuwezesha kuhakikisha kuwa IUD imekaa vizuri mahali pake na humsaidia daktari wako kuitoa.

  • IUD hufanya kazi vizuri sana katika kuzuia mimba na zinaweza kudumu kwa kati ya miaka 3 na 10

  • IUD hazina athari kwenye mwili mzima

  • Ni lazima daktari aweke na aondoe IUD yako

  • Unaweza kuwa mjamzito mara moja baada ya kutoa IUD

  • IUD inaweza kubadilisha kiwango chako cha damu au maumivu ya tumbo wakati wa hedhi yako

  • Inapowekwa ndani ya siku 5 baada ya tendo la ngono, IUD ya shaba hufanya kazi kama kingamimba ya dharura

Kuelewa Vifaa Vinavyowekwa Ndani ya Uterasi

Vifaa vinavyowekwa ndani ya uterasi (IUD) huwekwa na daktari kwenye uterasi ya mwanamke kupitia sehemu ya uke. IUD hutengenezwa kwa plastiki iliyofinyangwa. Aina mbili za IUD hutoa progestin iitwayo levonorgestrel. Aina nyingine ina umbo la T na ina waya wa shaba uliofungwa kwenye sehemu ya chini kwenye mikono ya T. Uzi wa plastiki huunganishwa kwenye IUD. Uzi huo huwezesha mwanamke kuhakikisha kuwa kifaa bado kipo mahali kinapofaa na daktari anaweza kukiondoa kwa urahisi.

IUD huzuiaje kupata mimba?

IUD huzuia kupata mimba kwa:

  • Kuua mbegu za kiume

  • Kuzuia mbegu za kiume zisifikie yai lako

  • Iwapo yai litakutana na mbegu, IUD inaweza pia kuzuia yai hilo lisiambatishwe kwenye uterasi yako

  • IUD haziondoi yai lililotungishwa mimba ambalo tayari limeambatishwa kwenye uterasi yako

Ninaweza kutumia IUD za aina gani?

Kuna aina 2 za IUD:

  • IUD zilizo na homoni

  • IUD zilizo na shaba (waya wa shaba umeunganishwa kwenye kifaa) badala ya homoni

IUD iliyo na homoni

  • Hukaa kwa miaka 3 au 5, au hadi itakapotolewa na daktari

  • Hutoa homoni iitwayo progestin

  • Huenda ikafanya usipate hedhi au uone kiasi kidogo tu cha damu wakati wa hedhi

IUD ya Shaba

  • Haitoi homoni

  • Inaweza kutumiwa kama kingamimba ya dharura baada ya kushiriki tendo la ngono bila kinga

  • Hukaa kwa miaka 10, au hadi itakapotolewa na daktari

  • Inaweza kusababisha kuvuja damu nyingi na tumbo kukakamaa wakati wa hedhi yako

Ni nani anayeweza kutumia IUD?

Wanawake wanaweza kutumia IUD, ikiwa ni pamoja na wasichana wadogo na wanawake ambao hawajapata watoto.

Hupaswi kuwekwa IUD ikiwa una:

Hupaswi kuwekwa IUD ikiwa wewe ni mjamzito.

Ni yapi matatizo yanayotokana na matumizi ya IUD?

Matatizo yanayoweza kutokana na matumizi ya IUD yanajumuisa:

  • IUD kutoka yenyewe katika mwaka wa kwanza (mara nyingi hufanyika kwa wanawake wenye umri mdogo au ambao bado hawajapata watoto)

  • IUD kutoboa shimo kwenye uterasi yako inapowekwa (ni nadra)

  • Kuongezeka kwa uwezekano wa kupata maambukizi ya fupanyonga katika mwezi wa kwanza baada ya kuwekwa IUD

  • Kuongezeka kwa kiwango cha damu kuvuja na maumivu ya tumbo wakati wa hedhi (IUD za shaba pekee)

Ni yapi manufaa ya kutumia IUD?

  • Ni mbinu ya kuzuia mimba inayofanya kazi vizuri sana

  • Uwezekano mdogo wa kupata saratani kwenye uterasi yako

  • Kuvuja kiasi kidogo cha damu wakati wa hedhi yako (IUD za homoni pekee)