Saratani ya Umio

(Uvimbe wa Umio)

Imepitiwa/Imerekebishwa Jan 2023

Umio ni bomba ambalo linaunganisha koo lako na tumbo lako.

Umio

Saratani ya umio ni nini?

Saratani ni ukuaji wa seli mwilini kwa namna isiyoweza kudhibitiwa. Seli ni elementi ndogo zinazoshikamana kuunda viungo vya mwili wako. Seli zina majukumu maalum. Viungo tofauti vimeundwa na aina tofauti za seli. Aina yoyote ya seli inaweza kuwa yenye saratani. 

Saratani ya umio ni saratani ambayo inaanzia kwenye utando wa umio lako.

  • Una uwezekano mkubwa zaidi wa kupata saratani ya umio ikiwa unatumia tumbaku na pombe, una maambukizi ya HPV, au magonjwa fulani ya umio

  • Dalili zinajumuisha matatizo ya kumeza, kupoteza uzani, na maumivu

  • Isipokuwa kama saratani itagundulika mapema, upasuaji, tibakemikali, na tiba nyingine zinaweza zikashindwa kuponya saratani yako lakini zikakusaidia kujihisi vizuri zaidi

Je, nini husababisha saratani ya umio?

Una uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya umio ikiwa:

  • Unatumia tumbaku na kunywa pombe

  • Una maambukizi ya HPV

  • Umewahi kupata saratani ya kichwa au shingo

  • Umio lako limewahi kupatiwa tiba ya mionzi ili kutibu saratani nyingine zilizokuwa karibu nalo

  • Umewahi kupata ugonjwa wa tindikali ya tumbo kurudi kwenye koo (huitwa GERD) ambao haukutibiwa kwa miaka mingi

Zipi ni dalili za saratani ya umio?

Unaweza usigundue dalili mara moja. Dalili za mapema zinajumuisha:

  • Kupata ugumu wa kumeza chakula, kwa sababu uwazi wa umio unazidi kupungua kadiri saratani inavyoongezeka

  • Kupungua uzani

  • Maumivu ya kifua, ambayo pia unaweza kuyahisi kwenye mgongo wako

Dalili za baadaye zinajumuisha:

  • Kupata shida kumeza vimiminiko na mate

  • Sauti yenye kukwaruza

  • Maumivu kwenye uti wa mgongo

  • Kwikwi

  • Kuishiwa na pumzi

Mwishowe, saratani huziba umio lako, hali ambayo hukufanya ushindwe kumeza na kusababisha mate kujaa mdomoni mwako.

Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina saratani ya umio?

Madaktari hushuku uwepo wa saratani ya umio kutokana na dalili zako. Ili kujua kwa hakika, watafanya vipimo kama vile:

Je, madaktari hutibu vipi saratani ya umio?

Ikiwa saratani ni ndogo, madaktari wanaweza kuichoma au kuikata na kuiodnoa kwa upasuaji ili kujaribu kukuponyesha.

Mara nyingi saratani haiwezi kupona, hivyo matibabu ya saratani ya umio yanaweza kusaidia kupunguza dalili kama vile maumivu na shida ya kumeza. Matibabu yanajumuisha:

  • Upasuaji ili kukata na kuondoa uvimbe

  • Tibakemikali

  • Tiba ya mionzi

  • Kutumia stent (bomba la wavu la chuma lenye kupindika) ili kufanya umio lako libaki wazi

  • Kuunguza saratani kwa kutumia leza ili kupanua uwazi

Ni muhimu kupata lishe ya kutosha. Ikiwa unaweza kumeza, unaweza kupata mchanganyiko maalum wa lishe za vimiminiko. Ikiwa huwezi kumeza, unaweza kutakiwa kulishwa kupitia bomba lililopo kwenye tumbo lako.

Kuwa na saratani ya umio kunaweza kuogofya na kufadhaisha. Daktari wako anaweza kukupatia usaidizi wa kukusaidia kukabiliana na dalili na hisia zako na kupanga siku za mwisho za maisha yako, kama vile kuandaa wosia wa kuishi.