Polipu ya utumbo mpana na rektamu

Imepitiwa/Imerekebishwa Jan 2023

Polipu ya utumbo mpana na rektamu ni nini?

Polipu ni bonge laini, la mviringo lililomea katika nafasi tupu kwenye mwili wako. Kwa mfano, unaweza kuwa na polipu kwenye pua yako au kwenye nyuzi za sauti.

Koloni yako ni utumbo wako mpana. Rektamu yako ni mfuko ulio mwisho wa utumbo mpana ambako kinyesi huhifadhiwa hadi unapokwenda msalani. Mara nyingi polipu humea kwenye koloni yako (utumbo mpana) au kwenye rektamu.

Kutambua Utumbo Mpana

  • Unaweza kuwa na polipu moja au idadi kubwa ya polipu

  • Polipu za utumbo mpana mara nyingi si hatarishi, lakini baadhi ni zenye saratani au zinaweza kugeuka kuwa zenye saratani

  • Hali fulani za kurithi katika familia zinaweza kusababisha polipu

  • Polipu inaweza kumea kwenye shina (shina jembamba ambalo linaunganisha polipu kwenye ukuta wa utumbo)

  • Jinsi polipu inavyokuwa kubwa, ndivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuwa ni yenye saratani

  • Polipu inaweza kusababisha kuvuja damu kutoka kwenye rektamu yako

  • Madaktari hukagua uwepo wa polipu kwa kutumia kolonoskopia

  • Madaktari hutibu polipu kwa kuziondoa

Polipu ambazo mwanzo zinakuwa si hatarishi zinaweza kukua na kuwa saratani ya utumbo mpana, na ndio maana madaktari huziondoa wakati wa kolonoskopia.

Polipu za utumbo mpana na rektamu husababishwa na nini?

Mara nyingi, madaktari hawajui kile kinachosababisha polipu kumea. Lakini baadhi ya hali za kurithi katika familia zinaweza kusababisha polipu, kama vile:

  • Adenomatasi poliposisi ya familia (ugonjwa ambao ni wa kurithi katika familia na husababisha saratani ya utumbo mpana)

  • Ugonjwa wa Peutz-Jeghers (ugonjwa ambao husababisha polipu kwenye tumbo na utumbo wako na madoa ya bluu na meusi kwenye uso, mikono, na miguu yako)

Hata hivyo, hali hizi ni za nadra sana. Mara nyingi, polipu hutokea pasipo sababu ya kueleweka.

Zipi ni dalili za polipu ya utumbo mpana au rektamu?

Polipu nyingi hazisababishi dalili. Dalili zinazofahamika zaidi ni kuvuja damu kwenye rektamu. Polipu kubwa inaweza kusababisha:

  • Kukakamaa

  • Maumivu ya tumbo

  • Matatizo ya utumbo, kama vile kuziba

  • Kuharisha

Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina polipu ya utumbo mpana au rektamu?

Madaktari hugundua polipu kwa kutumia sigmoidoskopia au kolonoskopia (tazama endoskopia). Kwa vipimo hivi viwili, daktari hufunga kamera ndogo kwenye bomba jepesi na kulipitisha kwenye tundu la haja kubwa ili atazame ndani ya rektamu na utumbo mpana.

Je, madaktari hutibu vipi polipu za utumbo mpana na rektamu?

Madaktari huondoa polipu wakati wa sigmoidoskopia au kolonoskopia. Ndani ya bomba la kutazama kuna kifaa kinachoweza kurudi ndani ambacho kinaweza kung'oa polipu. Wakati mwingine, upasuaji unahitajika. Ikiwa polipu ni yenye saratani, madaktari watafanya vipimo vingine ili kujua ina uwezekano wa kuwa ilisambaa kiasi gani. Unaweza kuhitaji upasuaji wa kuondoa sehemu ya utumbo wako.