Fupanyonga ni kikundi cha mifupa katikati mwa kiuno. Mifupa hii inazunguka sehemu ya chini ya viungo vya tumbo, kama vile kibofu cha mkojo na utumbo na viungo vya kike kama vile uterasi (mfuko wa uzazi) na ovari. Maumivu kwenye viungo hivi yanahisiwa kwenye sehemu ya fupanyonga na wakati mwingine yanaitwa maumivu ya fupanyonga. Maumivu ya fupanyonga ni ya kawaida kwa wanawake lakini yanaweza kuwa makali zaidi.
Maumivu ya fupanyonga yanaweza kuwa kidogo au makali na yanaweza kufanya sehemu yako ya fupanyonga ihisi kuwa nyororo
Maumivu yanaweza kuja kwa ghafla na yanaweza kudumu au yaishe na kurudi
Wanawake wengi hupata mikakamao mara tu kabla au wakati wa hedhi yao ya kila mwezi, ambayo ni kawaida
Nenda kwa daktari mara moja ukihisi maumivu ya fupanyonga ya ghafla, makali—inaweza kuwa ni ishara ya tatizo kubwa
Je, nini husababisha maumivu ya fupanyonga?
Kisababishaji cha kawaida zaidi cha maumivu ya fupanyonga ni:
Maumivu kutokana na kupata hedhi yako ya kila mwezi (mikakamao ya hedhi)
Unaweza pia kuwa na mikakamao katikati mwa hedhi, wakati mwili wako unaachilia yai (inaitwa kufanya yai).
Visababishaji hatari zaidi vya maumivu ya fupanyonga vinajumuisha:
Ugonjwa wa kidole tumbo—maambukizi kwenye kidole tumbo chako, kiungo kidogo kilicho katikati ya utumbo mdogo na mpana
Ujauzito wa nje ya kizazi uliopasuka—ujauzito kwenye sehemu isiyofaa, kama vile kwenye mirija yako ya uzazi, ambayo inaunganisha ovari zako kwenye uterasi (mfuko wa uzazi) wako
Ovari iliyosokotwa
Kuvuja damu au kuchanika kwenye mshipa wa damu au ogani
Ikiwa una mojawapo ya visababishaji hivi, madaktari wanaweza kuhitaji kufanya upasuaji.
Visababishaji vingine vya maumivu ya fupanyonga vinajumuisha:
Matatizo kwenye ovari zako—kama vile uvimbe kwenye ovari
Matatizo kwenye mirija yako ya uzazi—kama vile maambukizi kwake
Matatizo kwenye kibofu cha mkojo—kama vile maambukizi au mawe kwenye kibofu cha mkojo
Matatizo kwenye utumbo wako mpana—kama vile kufunga choo, gastroenteraitisi, au divertikulaitisi
Ujauzito, kama vile kuharibika mimba
Saratani ya viungo mbalimbali
Ninapaswa kumwona daktari lini kwa ajili ya maumivu ya fupanyonga?
Nenda kwa daktari mara moja ikiwa una maumivu ya fupanyonga na yoyote ya ishara hizi za onyo:
Kizunguzungu, kupoteza fahamu au mshtuko (kushuka kwa kiwango hatari kwa shinikizo la damu)
Homa au mzizimo
Maumivu kali, ya ghafla haswa ikiwa unahisi ukiwa mgonjwa kwenye tumbo yako, kutapika na kutokwa na jasho sana
Nenda kwa daktari siku hio ikiwa haujawai kuwa na maumivu ya fupanyonga kabla na maumivu yanadumu na yanakuwa mabaya zaidi.
Nenda kwa daktari siku hio au ndani ya siku chache ikiwa una maumivu ya fupanyonga pamoja na kuvuja damu ukeni baada ya kuacha kupata hedhi yako ya kila mwezi (ukomo wa hedhi).
Ukiendelea kupata maumivu ya fupanyonga lakini bila ishara zingine, nenda kwa daktari wakati unaweza, lakini kuchelewa kwa siku kadhaa kwa kawaida hakuna madhara.
Ni kipi kitafanyika nikienda kwa daktari kwa ajili ya maumivu ya fupanyonga?
Madaktari watakuuliza maswali kuhusu maumivu yako na kufanya uchunguzi. Unaweza pia kufanyiwa baadhi ya vipimo:
Vipimo vya mkojo wako ili kujua kama uko mjamzito au ikiwa una UTI (maambukizi ya njia ya mkojo)
Kipimo kwa kutumia mawimbi ya sauti, kipimo cha kompyuta (tomografia ya kompyuta), au MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) (vipimo ambavyo vinaonyesha picha za sehemu ya ndani ya sehemu ya fupanyonga yako)
Ikiwa una maumivu yasiyoisha au makali zaidi na vipimo vingine havionyeshi ni kipi kinayasababisha, unaweza kuhitaji taratibu ya upasuaji inayoitwa upasuaji unaotumia laparoskopi. Kwa taratibu hii, madaktari wanakupatia dawa ya kukuweka usingizini (unusukaputi). Kisha madaktari watakata mwili wako kidogo chini tu ya tumbo na kuingiza mrija wa kutazama ili kuona tatizo ni lipi.
Madaktari wanatibu aje maumivu ya fupanyonga?
Madaktari wanatibu kisababishaji cha maumivu yako ya fupanyonga, kama wanaweza. Wanaweza kukupatia dawa ya maumivu ili kukufanya uhisi vizuri hadi wajue ni nini inasababisha maumivu yako. Lakini ni muhimu kwa madaktari kuona ni nini inasababisha maumivu yako lakini si tu kutuliza maumivu kwa kutumia dawa.