Nyenzo za Mada
Je, athari ya sumu ni nini?
Athari ya sumu ni maradhi yanayotokana na kumeza, kupumua, au kugusa kitu chenye sumu (sumu). Nchini Marekani, zaidi ya watu milioni 2 hupata athari ya sumu kila mwaka. Hii ni pamoja na watu ambao kwa bahati mbaya wanatumia dawa haramu zaidi ya kipimo au kujaribu kujiua. Watu wengi hawaugui sana. Hata hivyo, watu wengine huwa wagonjwa sana na wanaweza kuaga dunia.
Kwa ajili ya usalama, weka dawa na bidhaa za kusafisha kwenye vyombo vyake asili
Hifadhi dawa na bidhaa za kusafisha mahali pasipoweza kufikiwa na watoto
Athari ya simu inaweza kuwa ndogo au inayowewza kutishia maisha
Kuwa mwangalifu ili kuhakikisha kuwa unatumia dawa kama ulivyoagizwa
Muulize daktari ikiwa unaweza kutumia zaidi ya dawa moja kwa wakati mmoja bila madhara
Je, vitu gani vina sumu?
Karibu kila kitu kinaweza kuwa na madhara katika wingi wake. Hata dawa za kuagizwa na daktari na za dukani zinaweza kuwa hatari ikiwa utazidisha dozi.
Ni vigumu kuorodhesha kila kitu ambacho kinaweza kuwa na sumu. Lakini ni salama kusema kuwa ikiwa kitu hakijakusudiwa kuliwa, kunywa, kupumua, au kutumika kwenye mwili wako, basi usitumie. Hata hivyo, kuna vitu vingi katika nyumba yako ambavyo si hatari. Hili ni muhimu kujua kwa sababu mara nyingi watoto wanaonja au kula vitu wanavyopata.
Je, nani yuko katika hatari ya kuathiriwa na sumu?
Watu walio katika hatari kubwa ya kuathiriwa na sumu ni pamoja na:
Watoto wadogo, kwa sababu wana mazoea ya kuweka vitu kinywani mwao
Watu wazee, ambao wanaweza kuchanganyikiwa na kuchanganya dawa zao
Wafanyakazi ambao kazi zao zinahusisha kemikali
Watu walio na matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya, hasa wale wanaotumia dawa za opioidi kama vile oksikodoni, heroini na fentanili
Watu wanaotaka kujiua na wanaweza kunywa sumu kwa makusudi—watu wanaofanya hivi au kufikiria kuhusu hilo wanapaswa kutafuta usaidizi wa afya yao ya akili
Je, dalili za kuathiriwa na sumu ni zipi?
Dalili hutofautiana kulingana na aina na kiasi cha sumu. Dalili zinaweza pia kutofautiana kulingana na umri na afya yako. Unaweza kupata dalili mara moja. Au inaweza kuchukua masaa au siku kabla ya kuona dalili zozote.
Dalili zinazoweza kuonyesha kuwa mtu ameathiriwa na sumu:
Kutapika
Kupumua kwa shida
Kuchanganyikiwa, usingizi, au kupoteza fahamu
Maumivu ya tumbo
Baadhi ya sumu huenda zisisababishe kuonekana kwa dalili hadi ziharibu sehemu za mwili wako, kama vile figo au ini.
Je, ninapaswa kufanya nini ikiwa mtu ameathiriwa na sumu?
Ikiwa mtu anaonekana kuwa mgonjwa sana na huenda ameathiriwa na sumu, piga simu kwa usaidizi wa dharura wa matibabu (911 katika maeneo mengi ya Marekani).
Ikiwa mtu ambaye huenda alikuwa ameathiriwa na sumu hana dalili kubwa za ugonjwa, piga simu kwenye kituo cha kudhibiti sumu kwa ushauri (1-800-222-1222 nchini Marekani). Mara nyingi watu wanaweza kutibiwa nyumbani. Shirika la Afya Duniani hutoa orodha ya kimataifa ya vituo vya sumu.
Ikiwa mtu ameathiriwa na sumu:
Jaribu kujua ni sumu gani
Chunguza kiasi cha sumu alichomeza
Ikiwa sumu hiyo ni bidhaa ya kusafisha au dawa, chukua chombo chake asilia uende nacho hospitalini ili madaktari waweze kukikagua
Usijaribu kumfanya mtu huyo atapike isipokuwa ikiwa utaambiwa na daktari au kituo cha kudhibiti sumu.
Kemikali inapokumwagikia:
Vua nguo, viatu, au mapambo yoyote yaliyopata kemikali
Osha ngozi vizuri kwa sabuni na maji
Ikiwa sumu iliathiri macho yako, yasafishe kabisa kwa maji au maji ya chumvi (maji ya chumvi yasiyo na vijidudu)
Ikiwa umeathiriwa na gesi yenye sumu, nenda mahali penye hewa safi mara moja. Ikiwa unamsaidia mtu ambaye ameathiriwa na sumu na kemikali au gesi zenye sumu, hakikisha huwa hupati sumu hiyo mwenyewe. Wataalamu walio na vifaa vya kinga pekee ndio ambao wanapaswa kwenda katika eneo lenye kemikali au gesi zenye sumu.
Je, madaktari wanawezaje kujua kuwa nimeathiriwa na sumu?
Madaktari watashuku sumu kulingana na dalili zako na maelezo yako ya kile kilichotokea.
Madaktari watauliza maswali ili kujua aina ya sumu na kiasi ulichomeza.
Je, madaktari hutibu vipi mtu aliyeathiriwa na sumu?
Watu wengi walioathiriwa na sumu watapona. Watu wengine wanaweza kuhitaji kutibiwa hospitalini.
Baada ya muda, mwili wako huondoa kiasi kikubwa cha sumu peke yake. Kwa kutegemea aina ya sumu, madaktari wanaweza:
Kukupa dawa ili kurejesha hali ya kawaida ya mapigo ya moyo na shinikizo la damu
Kukuweka kwenye mashine ya kukusaidia kupumua (respirator) ili kukusaidia kupumua
Kukupa makaa hai, ambayo yanaweza kuzuia sumu uliyomeza kuingia kwenye damu yako
Kukupa dawa inayofanya kazi dhidi ya sumu maalum (dawa ya kupunguza athari za sumu)
Kutumia kichujio maalum ili kuondoa sumu kutoka kwa damu yako (utaratibu unaoitwa hemodialisisi)
Sumu chache pekee ndizo zina dawa ya kupunguza athari yake. Naloxone ni dawa ya kupunguza athari ya dawa za opioidi (kama vile heroini). Inaweza kuokoa maisha ya mtu ambaye amezidisha dozi ya dawa za opioidi.
Je, ninawezaje kuzuia kuathiriwa na sumu?
Weka dawa katika vyombo vyao vya asili ili kuzuia kuchanganyika
Weka bidhaa za kusafisha nyumbani, dawa, na vitu vingine vinavyoweza kuwa sumu mahali ambapo watoto hawawezi kufikia
Kamwe usiweke bidhaa zenye sumu kwenye vikombe au chupa zinazotumika kunywa
Fuata maagizo ya dawa na bidhaa za nyumbani
Tupa dawa zilizoisha muda wake wa matumizi au zisizohitajika kwa kuzificha kwenye takataka za paka au nyenzo zingine zisizovutia, au piga simu kwa duka lako la dawa kwa ushauri juu ya utupaji