Nyenzo za Mada
Galaktoria ni nini?
Galaktoria ni hali ya matiti yako kuzalisha maziwa wakati ambapo hunyonyeshi mtoto mchanga. Wanaume na wanawake wote wanaweza kupata galaktoria.
Kwa kawaida galaktoria husababishwa na uvimbe kwenye tezi yako ya pituitari
Baadhi ya matatizo yanayosababisha galaktoria pia yanaweza kusababisha ugumba kwa wanaume na wanawake
Vipimo hujumuisha upigaji picha wa pituitari kwa kutumia Uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) au MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) wa ubongo, na upimaji wa homoni ya pituitari, prolaktini
Madaktari hutibu galaktoria kwa dawa na mara nyingine kwa njia ya upasuaji
Tezi ya pituitari ni kipande kidogo cha tishu cha ukubwa wa mbaazi kilichoko chini ya ubongo wako kinachozalisha homoni. Homoni ni kemikali zinazochochea seli au tishu nyingine kufanya kazi.
Je, nini husababisha galaktoria?
Prolaktini ni homoni inayotoka kwenye tezi ya pituitari ambayo hufanya matiti yako yazalishe maziwa. Kwa kawaida prolaktini huongezeka katika wanawake ambao wamejifungua hivi karibuni, hivyo wanaweza kunyonyesha watoto wao. Kiwango kikubwa cha prolaktini husababisha matiti kuzalisha maziwa hata pale ambapo huna ujauzito. Prolaktini inaweza pia kufanya matiti ya mwanaume yazalishe maziwa.
Sababu iliyozoeleka zaidi inayosababisha galaktoria kwa wanaume na wanawake ni:
Uvimbe kwenye tezi yako ya pituitari ambao husababisha tezi kutengeneza prolaktini nyingi
Sababu nyingine za kuwa na prolaktini nyingi ni pamoja na
Dawa fulani (baadhi ya dawa za shinikizo la damu na dawa za kuzuia mimba)
Tezi dundumio isiyofanya kazi vizuri (dundumio lisiloamilifu)
Ugonjwa wa ini
Baadhi ya saratani za mapafu
Kuwa na prolaktini nyingi pia kunaweza kuathiri uwezo wa kujamiiana na uzazi kwa wanaume na wanawake.
Zipi ni dalili za galaktoria?
Kwa wanawake:
Matiti yako kuzalisha maziwa pasipo kutarajia
Kukosa hedhi, au kupata hedhi mara chache
Ukavu kwenye uke kwa sababu ya viwango vidogo vya estrojeni
Wakati mwingine, kuwa na nywele nyingi mwilini kupita kiasi (hiriztizimu)
Kwa wanaume:
Matiti yako kuzalisha maziwa
Kupoteza hamu ya kujamiiana
Kwa wanaume na wanawake, uvimbe mkubwa unaweza kugandamiza neva kwenye ubongo na kusababisha maumivu ya kichwa au upofu kiasi.
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina galaktoria?
Madaktari hufahamu kuwa una galaktoria kwa sababu matiti yako yanazalisha maziwa bila sababu. Ili kufahamu chanzo cha galaktoria, watafanya vipimo kama vile:
Kipimo cha damu ili kupima kiwango cha prolaktini
Uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) au MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) ya ubongo
Je, madaktari wanatibu vipi galaktoria?
Madaktari hutibu galaktoria kwa kutumia:
Dawa ili kuzuia tezi yako ya pituitari kutengeneza prolaktini
Upasuaji ili kuondoa uvimbe, kama unao na iwapo dawa imeshindwa kufanya kazi
Tiba ya mionzi, iwapo dawa na upasuaji vimeshindwa kufanya kazi
Ikiwa dalili zako si kali sana na hazikupi wasiwasi, madaktari wanaweza wasitibu galaktoria yako. Unaweza kuhitaji kutumia estrogeni kwa kiwango cha chini cha estrogeni, na madaktari watafanya ufuatiliaji wa uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) au MRI (picha za resonance ya sumaku) kila mwaka ili kuhakikisha uvimbe wa tezi ya pituitari haukui zaidi.