Kutanuka kwa Tezi ya Pituitari

Imepitiwa/Imerekebishwa Jan 2023

Tezi ya pituitari ni kipande cha tishu chenye ukubwa wa kunde kinachopatikana chini ya ubongo. Tezi ni viungo vinavyotengeneza na kutoa homoni kwenye damu. Homoni ni kemikali zinazochochea seli au tishu nyingine kufanya kazi. Tezi ya pituitari hutoa homoni nyingi tofauti. Kila homoni ya pituitari inadhibiti tezi tofauti na kazi ya mwili.

Kufikia Tezi ya Pituitari

Kutanuka kwa tezi ya pituitari ni nini?

Kutanuka kwa tezi ya pituitari hutokea pale tezi ya pituitari ya kawaida inapoongezeka ukubwa kutokana na sababu fulani. Kubadilika kwa ukubwa wake kunaweza kusababisha tezi ya pituitari itengeneze homoni fulani kwa kiasi kingi au kidogo sana.

Pituitari kubwa inaweza pia kusukuma neva ambazo zinaunganisha macho yako kwa ubongo wako na kusababisha matatizo ya kuona.

Je, nini husababisha kutanuka kwa tezi ya pituitari?

Sababu zinazosababisha tezi ya pituitari kuwa kubwa ni pamoja na:

  • Uvimbe wa pituitari (sababu iliyozoeleka sana)

  • Damu kuvuja ndani ya tezi ya pituitari

  • Sakroidosisi

  • Magonjwa mengine au maambukizi, kama vile kifua kikuu

Zipi ni dalili za kutanuka kwa tezi ya pituitari?

Dalili za tezi kubwa ya pituitari ni pamoja na:

  • Maumivu ya kichwa

  • Kupoteza uwezo wa kuona, mara nyingi kwenye macho yote na kwenye sehemu ya juu, nje ya upeo wako wa kuona

Madaktari wanawezaje kujua ikiwa tezi yangu ya pituitari imetanuka?

Madaktari hupima uwepo wa tezi kubwa ya pituitari kwa kutumia:

  • Uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) au MRI (picha inayoonyesha sehemu ya ndani ya mwili wako) ya kichwa

  • Vipimo vya damu vya viwango vya homoni

Je, madaktari wanatibu vipi tezi ya pituitari iliyotanuka?

Madaktari hutibu tatizo lililosababisha tezi yako ya pituitari kuwa kubwa. Ikiwa una uvimbe, kwa kawaida wataondoa uvimbe huo kwa njia ya upasuaji. Wakati mwingine utapaswa kutumia homoni za kurudishia baada ya upasuaji.