Ugonjwa wa Parkinson ni ugonjwa unaoathiri sehemu ya ubongo wako inayodhibiti mwendo wako. Unapata mtetemo (kutetemeka), kukakamaa kwa misuli, mwendo wa taratibu, matatizo ya usawa, na ugumu wa kufikiria (kupoteza kumbukumbu).
Je, dalili zinazofanana na ugonjwa wa parkinson ni nini?
Katika hali ya Parkinson, unakuwa na dalili za ugonjwa wa Parkinson, lakini husababishwa na ugonjwa tofauti wa ubongo au na dawa au sumu fulani.
Mwanzoni, unatetemeka (mitetemo) kwenye vidole na mikono yako wakati misuli yako imetulia na kupumzika.
Unaweza pia kuwa na hali ya misuli kukaza, mwendo wa taratibu, na matatizo ya usawa.
Madaktari hutibu sababu za dalili zinazofanana na ugonjwa wa parkinson pale inapowezekana na hutumia dawa na matibabu ya kimwili
Ni nini husababisha dalili zinazofanana na ugonjwa wa Parkinson?
Visababishaji vya dalili zinazofanana na za ugonjwa wa parkison vinajumuisha:
Kuvimba kwa ubongo kunakosababishwa na maambukizi ya virusi (ensefalitisi)
Ugonjwa wa Alzheimer, guonjwa wa Lewy wa mwili kupoteza utambuzi, na matatizo mengine ambapo ubongo wako huzorota kadiri muda unavyopita.
Ugonjwa wa Wilson (ugonjwa unaosababisha mrundikano wa shaba mwilini mwako)
Majeraha ya kichwa, haswa ikiwa yanatokea mara kwa mara, kama vile kwenye mchezo wa ndondi au kandanda
Dawa fulani, kama vile baadhi ya dawa za skizofrenia na dawa za kuzuia kichefuchefu
Sumu, kama vile monoksidi ya kaboni na pombe ya methanoli
Dalili za hali ya kufanana na ugonjwa wa parkinson ni zipi?
Dalili za hali ya kufanana na ugonjwa wa parkinson zinajumuisha:
Mkono wako unatetemeka wakati misuli yako imelegea (hii ni dalili kuu, kwani mitetemeko mingine mingi ya mikono hutokea wakati misuli ya mkono inatumika)
Misuli migumu
Mwendo wa taratibu
Matatizo ya usawaziko na kutembea
Unaweza kuwa na dalili ambazo si za ugonjwa wa Parkinson, kama vile:
Kupoteza kumbukumbu mapema (katika ugonjwa wa Parkinson kupoteza kumbukumbu hutokea baadaye)
Shinikizo la chini la damu, ugumu wa kumeza, kufunga choo, na matatizo ya mkojo
Mwendo wa macho usiokuwa wa kawaida
Hisia isiyo halisi (kusikia au kuona vitu ambavyo havipo) ya mapema (katika ugonjwa wa Parkinson hisia zisizo halisi hutokea baadaye)
Matatizo ya kutumia au kuelewa lugha
Madaktari wanawezaje kujua kama nina dalili zinazofanana na za ugonjwa wa parkinson?
Madaktari watakuuliza kuhusu hali za hatari ambazo zinaweza kusababisha dalili zinazofanana na za ugonjwa wa parkison, kama vile:
Kutumia dawa fulani
Sumu kuingia mwilini
Historia ya matatizo ya ubongo kwenye familia
Majeraha ya kichwa ya mara kwa mara
Kwa kawaida, madaktari hufanya vipimo kama vile:
Tomografia ya kompyuta (uchanganuzi wa CT) au upigaji picha kwa mvumo wa sumaku (MRI)
Wakati mwingine madaktari huagiza ujaribu dawa ya ugonjwa wa Parkinson. Dawa hiyo ikifanya kazi, basi kuna uwezekano kuwa una ugonjwa wa Parkinson na si dalili zinazofanana na za ugonjwa wa Parkinson.
Je, madaktari hutibu vipi dalili zinazofanana na za ugonjwa wa parkinson?
Ikiwa kuna tatizo lingine la kiafya linalosababisha dalili zinazofanana na za ugonjwa wa parkinson, madaktari watalitibu iwapo inawezekana kufanya hivyo.
Daktari anaweza pia:
Watakuagiza ufanye tiba ya kuzoeza mwili au tiba ya kimazingira
Watakuagiza ujishughulishe, ule chakula chenye afya, na kutumia vifaa vya usaidizi (kama vile fimbo au kitembezi) ili kukusaidia kwa maisha ya kila siku