Ugonjwa wa Alzheimer

Imepitiwa/Imerekebishwa Dec 2022

Je, ugonjwa wa Alzheimer ni nini?

Ugonjwa wa Alzheimer ni aina ya tatizo la kupungua kwa utambuzi ambao kwa kawaida huathiri watu wenye umri wa zaidi ya miaka 65. Tatizo la kupungua kwa utambuzi ni tatizo la ubongo ambalo hufanya isiwe rahisi kukumbuka, kufikiria, kuelewa lugha, na kujifunza.

Matatizo ya ubongo huzidi kuwa mabaya zaidi kadri mtu anavyozidi kuzeeka. Watu wenye ugonjwa wa Alzheimer hatimaye huhitaji usaidizi kutoka kwa watu wengine ili kufanya shughuli za kila siku.

  • Ubongo wa kila mtu hubadilika kulingana na umri, lakini ugonjwa wa Alzheimer huathiri tishu za ubongo

  • Ugonjwa wa Alzheimer unaweza kutokea zaidi kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 65, wanawake, na wale ambao wana jamaa aliyeathiriwa na ugonjwa huo

  • Mwanzoni, mtu husahau matukio ya hivi karibuni, na polepole, baada ya muda, kumbukumbu inazidi kuwa mbaya

  • Wengi wa watu huishi kwa takriban miaka 7 baada ya utambuzi wa ugonjwa wa Alzheimer

  • Madaktari hushuku ugonjwa wa Alzheimer kulingana na dalili, uchunguzi, na vipimo vingine

  • Dawa zinaweza kusaidia kuboresha kumbukumbu kwa baadhi ya watu

Je, ugonjwa wa Alzheimer husababishwa na nini?

Ugonjwa wa Alzheimer unaonekana kusababishwa na dutu zisizo za kawaida ambazo hujilimbikiza kwenye ubongo. Dutu hizi huathiri seli za ubongo na hatimaye kuziua. Kadiri seli za ubongo zinavyokufa, ndivyo utendaji wa ubongo unavyozidi kuwa mbaya. Madaktari hawajui kwa hakika kile kinachosababisha dutu zisizo za kawaida kujilimbikiza kwenye ubongo. Matatizo yanaonekana kuwa ya kurithi.

Je, dalili za ugonjwa wa Alzheimer ni zipi?

Ugonjwa wa Alzheimer husababisha dalili nyingi ambazo ni sawa na dalili zingine za matatizo ya kupungua kwa utambuzi Hata hivyo, watu walio na ugonjwa wa Alzheimer wanaweza kuwa na wakati mgumu sana kukumbuka matukio ya hivi karibuni.

Ugonjwa wa Alzheimer husababisha matatizo kama vile:

  • Kumbukumbu

  • Kutumia lugha

  • Sifa ya mtu

  • Shida ya kuwaza kwa makini

Matatizo haya hufanya iwe vigumu kufanya kazi za kawaida za kila siku, kama vile ununuzi, kuandaa chakula, na kutumia pesa ifaavyo. Huenda pia mtu akawa na hulka zisizo za kawaida.

Dalili za mapema za ugonjwa wa Alzheimer:

  • Kusahau mambo yaliyotokea muda usiokuwa mrefu

  • Kuhisi Unyogovu, hofu, wasiwasi, au kuwa na hisia chache

  • Kuwa na changamoto katika kufanya maamuzi

  • Kuwa na changamoto katika kupata neno sahihi la kusema

  • Kuchanganywa na mambo unayoyaona na kusikia

  • Kupata changamoto ya kuendesha gari

  • Matatizo ya kupatwa na usingizi au kulala

Dalili za baadaye za ugonjwa wa Alzheimer:

  • Changamoto ya kukumbuka matukio ya zamani

  • Kutowatambua watu na vitu vingine unavyofahamu

  • Kutangatanga/Kuzurura

  • Kukasirika kwa urahisi hadi kufikia hatua ambapo mtu anaweza kuwashambulia na kuwapiga wengine

  • Kutokua na ufahamu wa wakati au mahali

  • Kuhitaji usaidizi katika kufanya shughuli za kila siku, kama vile kula, kuvaa, na kuoga

  • Kushindwa kuzuia mkojo

Hatimaye, watu wenye ugonjwa wa Alzheimer hupoteza karibu utendaji wote wa ubongo. Kutoweza kutoka kitandani au kujisogeza. Hatimaye, hawawezi hata kumeza chakula walichotiwa mdomoni.

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa mtu ana ugonjwa wa Alzheimer?

Madaktari wanashuku ugonjwa wa Alzheimer kulingana na:

Madaktari wanaweza kufanya vipimo vingine, kama vile vipimo vya damu na picha za akili ili kuchunguza ndani ya ubongo. Vipimo vya picha vinaweza kuwa tomografia ya kompyuta (CT) au upigaji picha kwa mvumo wa sumaku (MRI). Vipimo hivi humsaidia daktari kuona ikiwa kuna hali zingine zozote zinazoweza kutibika kama vile kuweweseka. Madaktari wanaweza pia kufyonza majimaji ya uti wa mgongo ili kutafuta dutu isiyo ya kawaida inayohusishwa na ugonjwa wa Alzheimer.

Je, madaktari hutibuje ugonjwa wa Alzheimer?

Madaktari watafanya:

  • Kumpa mgonjwa dawa za kusaidia kurejesha kumbukumbu

  • Kuhakikisha kuwa mtu huyo yuko salama na ana usaidizi anaohitaji ili kufanya shughuli za kila siku

Watu walio na ugonjwa wa Alzheimer wanafanya vyema zaidi katika mazingira yenye furaha na utulivu. Kuwashauri watunzaji wafuate ratiba za kawaida za kula, kulala, na shughuli kunaweza kusaidia.

Kuwashughulikia walezi

Kuwatunza watu walio na aina yoyote ya tatizo la kupungua kwa utambuzi, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa Alzheimer, ni kazi inayochosha na yenye mahitaji mengi. Huenda walezi wakafadhaika na kuchoka, na mara nyingi kutoshughulikia afya ya mwili na akili. Ni muhimu kwa walezi:

  • Kujifunza jinsi ya kukidhi mahitaji ya watu wenye tatizo la kupungua kwa utambuzi na cha kutarajia kutoka kwao

  • Kutafuta usaidizi inapohitajika, kama vile utunzaji wa mchana, kutembelewa na wauguzi nyumbani, usaidizi wa kutunza nyumba, usaidizi kutoka kwa mtu unayeishi naye, ushauri nasaha na vikundi vya kusaidiana

  • Kujitengea muda, ikiwemo kutangamana na marafiki na kufanya mambo yanayowavutia na shughuli wanazofurahia

Je, ninawezaje kuzuia ugonjwa wa Alzheimer?

Madaktari wanadhani kuwa mambo haya yanaweza kusaidia kuzuia ugonjwa wa Alzheimer:

  • Kuhakikisha kuwa una viwango vya kawaida vya lehemu kwa kula lishe yenye mafuta kidogo na kutumia dawa zinazohitajika

  • Kuhakikisha kuwa shinikizo la damu liko katika kiwango cha kawaida

  • Kufanya mazoezi

  • Kudumisha shughuli za kiakili kama vile kufanya mafumbo ya maneno, kusoma gazeti na kujifunza stadi mpya

  • Kunywa chini ya vinywaji 3 vya pombe kwa siku—lakini mara baada ya kutambuliwa kwa ugonjwa wa Alzheimer, ni bora kutokunywa pombe kabisa kwa sababu inaweza kuzidisha dalili