Idadi ya Chini ya Seli Nyeupe za Damu

(Neutropenia: Limfopenia)

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2023

Seli nyeupe za damu ni sehemu ya ulinzi wa mfumo wa kingamaradhi wa mwili wako dhidi ya maambukizi na saratani. Mwili wako una aina mbalimbali za seli nyeupe za damu. Seli nyingi nyeupe za damu zinaundwa ndani ya uboho wa mifupa yako.

Je, idadi ndogo ya seli nyeupe za damu ni nini?

Idadi ndogo ya seli nyeupe za damu ni idadi ya chini isivyo kawaida ya aina moja au zaidi ya seli nyeupe za damu.

  • Idadi ndogo ya seli nyeupe za damu hukuweka katika hatari kubwa ya kupata maambukizi

  • Baadhi ya maambukizi yanaweza kuwa ya kutishia maisha

  • Idadi ndogo ya seli nyeupe za damu inaweza kuwa ni athari hasi ya dawa, hasa dawa za tibakemikali

  • Wakati mwingine idadi ndogo ya seli nyeupe za damu husababishwa na maambukizi au saratani

  • Madaktari wanaweza kufanya vipimo vya damu na vipimo vya uboho wa mifupa ili kujua ni kwanini una idadi ndogo ya seli nyeupe za damu

  • Madaktari wanaweza kukupatia dawa ili kuongeza idadi ya seli nyeupe za damu na dawa za kuua bakteria ikiwa una homa au dalili za maambukizi

Je, nini husababisha idadi ndogo ya seli nyeupe za damu?

Kuna sababu nyingi zinazosababisha idadi ndogo ya seli nyeupe za damu:

  • Dawa: Dawa nyingi, hasa dawa za tibakemikali

  • Maambukizi: VVU, na maambukizi mengine mengi ya virusi, na maambukizi makali ya bakteria mwilini (sepsisi)

  • Saratani inayoanzia kwenye uboho wa mifupa, kama vile lukemia, limfoma na maeloma

  • Saratani iliyoenea kwenye uboho wa mifupa, kama vile kutoka kwenye saratani ya matiti au saratani ya tezi dume

  • Matatizo mengine ya uboho wa mifupa, kama vile magonjwa yenye kuathiri uzalisahji wa chembe hai za damu

  • Tiba ya mionzi ambayo inajumuisha uboho wa mifupa

Zipi ni dalili za idadi ndogo ya seli nyeupe za damu?

Idadi ndogo ya seli nyeupe za damu haina dalili maalum. Unapata dalili kwa sababu unapata maambukizi kila mara. Wakati mwingine maambukizi ni yale yasiyo ya kawaida ambayo watu wengi hawapati.

Dalili za maambukizi zinaweza kuanza ghafla au taratibu na zinaweza kujumuisha:

  • Homa

  • Upele

  • Vinundu vya limfu vilivyovimba

  • Vidonda vinavyouma mdomoni mwako na kwenye tundu la haja kubwa (uwazi unaopatikana mwishoni mwa njia ya mmeng'enyo wa chakula ambapo kinyesi hutoka nje)

Madaktari watajuaje ikiwa nina idadi ndogo ya seli nyeupe za damu?

Madaktari wanaweza kufahamu kuwa una idadi ndogo ya seli nyeupe za damu kwa kufanya hesabu kamili ya damu (CBC) ya kila mara. Ikiwa unapatiwa matibabu au una ugonjwa ambao unaweza kushusha idadi ya seli zako nyeupe za damu, madaktari watakagua CBC yako kila mara.

Wakati mwingine, sababu iko wazi, kama vile ikiwa unapatiwa tibakemikali au tiba ya mionzi kwa ajili ya saratani.

Ikiwa sababu haiko wazi, madaktari wanaweza kufanya:

  • Vipimo vya damu, mkojo, na kupiga picha wakitafuta maambukizi

  • Uondoaji wa kipande cha uboho wa mifupa (kuondoa uboho kiasi kwa kutumia sindano ili kuufanyia vipimo)

Je, madaktari hutibu vipi idadi ndogo ya seli nyeupe za damu?

Madaktari hutibu idadi ndogo ya seli nyeupe za damu kwa kutumia:

  • Dawa za kuua bakteria ili kutibu maambukizi yoyote

  • Dawa za kuhamasisha mwili wako kuunda zaidi seli nyeupe za damu

  • Matibabu ya magonjwa yoyote ambayo yanaweza kuwa yanasababisha idadi kuwa ndogo