Ni nini maana ya maambukizi ya virusi vya ukimwi (HIV)?
Maambukizi ya virusi vya ukimwi (HIV) ni aina ya virusi vinavyoitwa retrovirus. Yanasababisha UKIMWI (ukosefu wa kinga mwilini), ambao ni ugonjwa wa kutishia maisha.
UKIMWI huitwa virusi vya ukosefu wa kinga mwilini kwa sababu unaleta udhaifu (ukosefu) kwenye mfumo wako wa kingamaradhi. Mfumo wako wa kingamwili husaidia kukukinga dhidi ya maambukizi na kansa.
Maambukizi ya virusi vya ukimwi hufanya mfumo wa kingamaradhi wa mwili wako uwe dhaifu kwa sababu yanaua aina fulani za seli nyeupe za damu ziitwazo limfosaiti za CD4. Bila limfosaiti za CD4 za kutosha, una uwezekano mkubwa zaidi wa kupata maambukizi na kansa mbalimbali.
Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi hudhoofisha kinga za mwili wako dhidi ya maambukizi na kansa fulani
Hakuna tiba ya kuponya VVU, lakini dawa za VVU huleta tofauti kubwa katika kupunguza nguvu za virusi
Bila matibabu, VVU husababisha UKIMWI
Kuanza dawa za VVU haraka iwezekanavyo kunaweza kusaidia kuepuka matatizo yanayohusishwa na UKIMWI
Watu hawafi kutokana na VVU vyenyewe, mbali kutokana na changamoto za maambukizi na kanda wanazopata
Kushiriki ngono kwa njia salama, kutotumia sindano pamoja, na kutogusa damu ya wengine hukusaidia kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
Ni nini maana ya upungufu wa kinga mwilini (UKIMWI)?
UKIMWI ni upungufi wa kinga mwilini unaosababishwa na VVU. Si kila mtu aliye na maambukizi ya VVU hupata UKIMWI Unapata UKIMWI wakati una maambukizi ya VVU pamoja na mojawapo ya:
Idadi ndogo sana ya limfosaiti za CD4
Maambukizi na kansa fulani
Kuna maambukizi na kansa nyingi zinazobainisha UKIMWI. Baadhi ya zinazotokea sana ni pamoja na:
Maambukizi ya kuvu ya umio ("umio ya chakula" inayounganisha koo na tumbo yako), ubongo, au mapafu
Kaposi sarcoma, kansa inayosababisha madoa yasiyo na maumivu yenye rangi nyekundu na zambarau kwenye ngozi au ndani ya mdomo wako
Limfoma isiyo ya Hodgkin na aina nyingine fulani za saratani
Maambukizi fulani ambayo mfumo wa kingamaradhi wenye afya unaweza kupambana nayo lakini mfumo dhaifu hauwezi, kama vile nimonia inayotokana na kuvu, toksoplasmosisi, na kirusi cha sitomegalo
Watu walio na UKIMWI mara nyingi hupoteza uzani sana—hali hii inaitwa "kudhoofika kutokana na UKIMWI."
Je, nini husababisha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi?
Virusi vya HIV vinaposhambulia limfosaiti ya CD4, inatengeneza nakala nyingi za virusi hivyo kabla ya kuua seli ya CD4 na kuachilia nakala hizo za virusi. Kisha nakala hizo huvamia limfosaiti zingine za CD4, ambazo nazo hutengeneza nakala zaidi. Utaratibu huu huendelea hadi kunapokuwa na mabilioni ya VVU mwilini mwako.
Unaweza kuambukizwa VVU kwa kugusana na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa, hususan:
Damu
Manii
Majimaji ya uke
Maziwa ya mama
Ni nadra kumbukizwa kutokana na machozi, mkojo, au mate ya mtu. Majimaji haya hubeba virusi hivyo lakini kwa viwango vidogo.
Unaweza kupata VVU kwa kushiriki ngono bila kinga na mtu aliyeambukizwa
Unaweza kupata VVU kwa kushiriki sindano na mtu aliyeambukizwa
Watoto wanaweza kupata VVU kutoka kwa mama zao walioambukizwa, wakati wa ujauzito, kujifungua, na kunyonyesha
Lakini huwezi kupata VVU kwa kumgusa, kumshika au kumkaribia mtu aliye na VVU
Dalili za VVU ni zipi?
Watu wengi hawapati dalili mara moja. Ndani ya wiki 1 hadi 4 baada ya kupata VVU, unaweza kupata dalili kama vile:
Homa
Upele
Uvimbe kwenye shingo, makwapa, au kwenye kinena chako—uvimbe huo ni vinundu vya limfu vilivyovimba, ogani ndogo zenye umbo la haragwe zinazosaidia mwili wako kupambana na maambukizi
Kuhisi udhaifu na uchovu
Dalili hizo hudumu kwa siku 3 hadi 14. Baada ya dalili hizi kuisha, huenda ukapata dalili chache au usipate dalili zozote kwa miaka mingi.
Baadaye, usipotibiwa, mfumo wa kingamaradhi wa mwili wako ambao umekuwa dhaifu hupata matatizo ya kukulinda dhidi ya maambukizi. Utakuwa na dalili tofauti kulingana na maambukizi unayopata. Kwa mfano, ikiwa una maambukizi ya mapafu, unaweza kukohoa na kupumua kwa shida. Ukiwa na maambukizi kwenye umio lako, unaweza kuhisi maumivu unapomeza. Maambukizi kwenye utumbo wako yatasababisha kuharisha na kupoteza uzani.
Madaktari wanawezaje kujua iwapo nina VVU?
Madaktari kwanza hufanya kipimo rahisi cha uchunguzi kwenye damu au mate yako. Kipimo hicho cha uchunguzi kikionyesha ishara za VVU, madaktari hufanya vipimo vingine vya damu ili kuhakikisha.
Ikiwa una maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, madaktari hupima kiwango cha VVU kilicho kwenye damu yako.
Kiwango hiki huitwa kipimo cha virusi mwilini
Kipimo cha virusi mwilini ni idadi muhimu kwako na kwa daktari wako. Kiwango cha juu cha kipimo cha virusi ni kibaya. Kinamaanisha kuwa kuna virusi vingi mwilini mwako na mfumo wa kingamaradhi wa mwili wako ni dhaifu. Kiwango cha chini cha kipimo cha virusi ni kizuri. Kinamaanisha kuwa matibabu unayopata yanafanya kazi.
Madaktari pia hufanya vipimo vya damu mara kwa mara ili kujua idadi ya seli za CD4 ulizo nazo.
Idadi hii inaitwa idadi yako ya CD4
Kiwango cha juu cha CD4 kinaamaanisha kuwa mfumo wako wa kingamwili ni thabiti. Kiwango cha chini cha CD4 kinaamaanisha kuwa mfumo wako wa kingamwili unazidi kuwa dhaifu. Kiwango cha chini cha CD4 kinaweza kumaanisha kuwa dawa zako zimeacha kufanya kazi au huzitumii. Dawa zinaweza kuacha kufanya kazi kwa sababu virusi vimeanza kukinza dawa hizo. Kiwango chako cha CD4 kikiwa chini sana, huenda ukahitajika kutumia dawa ili uzuie maambukizi.
Kufahamu kuwa una VVU ni muhimu kwa sababu kupata matibabu kunaweza kukusaidia kuishi maisha marefu, kuwa na afya, na kutoeneza virusi kwa watu wengine.
Madaktari wanatibu vipi VVU?
Madaktari hawawezi kutibu ugonjwa wako wa VVU, lakini wanaweza kutumia dawa za VVU, ziitwazo dawa za kupunguza makali ya virusi, ili kupunguza maambukizi:
Dawa za kupunguza makali ya virusi huzuia VVU visijirudufishe na kupunguza kiwango cha VVU kwenye damu yako
Kwa kawaida utatumia dawa 3 au zaidi za VVU kwa sababu dawa za VVU hufanya kazi vizuri zaidi zikitumiwa pamoja
Mara nyingi dawa kadhaa huwekwa kwenye tembe moja, kwa hivyo hutahitaji kumeza vidonge vingi
Ni lazima utumie dawa za VVU milele
Ukiacha kutumia dawa hizo, hata kwa muda mfupi, VVU vinaweza kurejea
Ukitumia dawa zako kama ulivyoagizwa na daktari, unaweza kuishi muda mrefu ukiwa na maambukizi ya VVU.
Madaktari wanaweza kukupatia dawa zingine za:
Kuzuia maambukizi mengine, kama vile maambukizi ya kuvu na nimonia
Kusaidia kukabiliana na athari mbaya, kama vile udhaifu na kupoteza uzani
Hakikisha kuwa madaktari wako wote wanajua dawa za VVU unazotumia kabla hawajakupatia dawa zingine zozote.
Ninawezaje kuzuia VVU?
Unaweza kuzuia VVU kwa kushiriki ngono kwa njia salama na kutotumia sindano pamoja.
Tumia kondomu ya mpira wakati wa tendo la ngono na uitumie kwa usahihi ili isivunjike au kumwaga shahawa
Usipake kondomu mafuta ya grisi au mafuta mengine ya kulainisha kwa sababu yanaweza kuifanya iwe dhaifu
Pimwa VVU na umwombe mwenzi wako apimwe pia kabla hamjaanza kushiriki vitendo vyovyote vya ngono
Usitumie sindano au siringji moja pamoja na mtu mwingine yeyote
Vaa glavu za mpira ikiwa kuna uwezekano kwamba utagusana na damu au majimaji mengine ya mwili wa mtu mwingine
Ikiwa wewe ni mjamzito, pimwa VVU ili daktari wako akuelekeze uanze kutumia dawa za kuzuia mtoto wako asiambukizwe
Unaweza kutumia dawa za VVU kabla ya kuathiriwa na VVU ziitwazo tiba ya kabla ya kuambukizwa (PrEP). Lakini dawa hizo ni ghali na kwa kawaida zinapendekezewa tu watu walio katika hatari kubwa ya kupata maambukizi, kama vile watu walio na mwenzi aliye na VVU.
Ikiwa tayari una VVU, unaweza kuzuia kueneza maambukizi kwa watu wengine kwa kushirki tendo la ngono kwa njia salama na kuepuka kutumia sindano pamoja.
Bado hakuna chanjo ya kuzuia maambukizi ya VVU.