kondo la nyuma lililopandikizwa chini

Imepitiwa/Imerekebishwa May 2023

Je, kondo ni nini?

  • Kondo ni kiungo ambacho hukua upande wa ndani wa sehemu ya juu ya uterasi (mfuko wa uzazi) ukiwa mjamzito.

  • Lina mishipa mingi mikubwa ya damu inayobeba oksijeni na virutubisho kutoka kwako kwenda kwa kijusi (mtoto)

  • Mishipa ya damu ya kondo huunda kiunga mwana ili kuunganisha kondo na kijusi

  • Takriban dakika 15 baada ya kujifungua mtoto, kondo hutenganishwa na uterasi yako na hutoka kupitia uke wako

  • Ndiyo maana pia linaitwa "kondo la nyuma"

Je, tatizo la kondo la nyuma kujipandikiza kwenye sehemu ya chini ya uterasi ni nini?

  • Tatizo la kondo la nyuma kujishikiza kwenye sehemu ya chini ya uterasi ni wakati kondo la nyuma linapojishikiza chini sana kwenye uterasi yako, juu au karibu na mlango wako wa kizazi

Shingo ya kizazi ni sehemu ya chini ya uterasi yako. Una mwanya ambao kwa kawaida hufungika ukiwa mjamzito. Mtoto wako anapokuwa tayari kuzaliwa, mlango wa kizazi hufunguka (hupanuka) ili kumruhusu mtoto wako kutoka nje. Ikiwa una kondo la nyuma lililopo chini, kondo la nyuma huziba njia ya mtoto.

  • Mara nyingi tatizo la kondo la nyuma kujishikiza kwenye sehemu ya chini ya uterasi hupungua lenyewe kabla ya kujifungua

  • Ikiwa tatizo halitapungua kabla ya kujifungua, mtoto wako anaweza kuchana kondo la nyuma wakati anapopita kwenye mlango wa kizazi hadi kwenye njia ya uzazi (uke), na kusababisha kutokwa na damu nyingi sana

  • Ikiwa una tatizo la kondo la nyuma kujishikiza kwenye sehemu ya chini ya uterasi, usifanye ngono hadi mtoto wako atakapozaliwa—kufanya ngono wakati una kondo lililo chini kunaweza kusababisha kutokwa na damu

Matatizo ya Kondo la nyuma

Kwa kawaida, kondo linapatikana sehemu ya juu ya uterasi, na hujipachika kwenye ukuta wa uterasi baada ya mtoto kuzaliwa. Kondo hubeba oksijeni na virutubisho kutoka kwa mama hadi kwa kijusi.

Wakati wa kondo kujitenganisha na mfuko wa uzazi (abruptio placentae), kondo linajitenganisha na ukuta wa uterasi kabla ya wakati unaofaa, hali inasyosababisha uterasi kuvuja damu na kupunguza kiasi cha oksijeni na virutubisho vinavyomfikia mtoto hupungua. Wanawake walio na tatizo hili hulazwa hospitalini, na huenda mtoto akazaliwa mapema.

Kondo linapojipachika upande wa chini, huwa juu ya shingo ya kizazi, upande wa chini wa uterasi. Kondo kujipachika upande wa chini kunaweza kusababisha mama kuvuja damu ghafla bila maumivu yoyote, baada ya wiki 20 za ujauzito. Huenda mama akavuja damu nyingi. Kawaida mtoto huzaliwa kwa njia ya upasuaji.

Je, dalili za tatizo la kondo la nyuma kujishikiza kwenye sehemu ya chini ya uterasi ni zipi?

  • Kutokwa na damu kwa ghafla, bila uchungu, nyekundu angavu katika kipindi cha mwisho cha ujauzito

  • Mpigie simu daktari wako mara moja ikiwa wewe ni mjamzito na unatokwa na damu ukeni—maisha yako na ya mtoto wako yanaweza kuwa hatarini

Madaktari wanawezaje kujua kama nina kondo iliyopo chini?

  • Madaktari hushuku uwepo wa tatizo la kondo la nyuma kujishikiza kwenye sehemu ya chini ya uterasi ikiwa unatokwa na damu kwenye uke ambapo huanza baada ya wiki 20 za ujauzito

  • Watafanya kipimo cha picha kutumia mawimbi ya sauti ili kujua kwa hakika—kipimo hiki kinatumia mawimbi ya sauti kupiga picha za sehemu tofauti za ndani za uterasi yako.

  • Wakati wa uchunguzi wa kipimo cha picha cha kutumia mawimbi ya sauti, watachunguza pia ili kuhakikisha kuwa kondo lako la nyuma halijajiondoa kenye uterasi yako mapema (kutenguka kwa kondo la nyuma)

Je, madaktari wanatibuje tatizo la kondo la nyuma kujishikiza kwenye sehemu ya chini ya uterasi?

Ikiwa madaktari wanafikiri kuwa mapafu ya mtoto wako yamekua vya kutosha kuweza kuzaliwa akiwa salama (kwa kawaida baada ya wiki 36 za ujauzito), watafanya:

Madaktari hujaribu kufanya Upasuaji wa kupasua tumbo la uzazi kabla ya kupata uchungu wa uzazi. Kupata uchungu wa uzazi kunaweza kuchochea kuvuja damu.

Ikiwa unatokwa na damu kabla ya wiki 36 za ujauzito:

  • Madaktari watakuruhusu ulazwe hospitalini ukiwa umepumzika kitandani ili kuona ikiwa kutokwa na damu kutakoma

  • Madaktari watafuatilia mapigo ya moyo wa mtoto wako

  • Ikiwa kutokwa na damu kutakoma, unaweza kurudi nyumbani, lakini itabidi uwe tayari kurudi hospitali haraka ikiwa utaanza kutokwa na damu tena

  • Ikiwa kuvuja damu hakukomi au mapigo ya moyo ya mtoto wako si ya kawaida, watafanya Upasuaji wa kupasua tumbo la uzazi

Ikiwa madaktari wanafikiri unahitaji kujifungua mapema, wanaweza kuchukua sampuli ya majimaji yanayomzunguka mtoto wako (maji ya amnioti). Madaktari wanaweza kupima majimaji ili kujua ikiwa mapafu ya mtoto wako yamekua vya kutosha ili uweze kujifungua.