Je, mtoto kuzaliwa mfu ni nini?
Mtoto kuzaliwa mfu ni wakati unapokuwa mjamzito kwa wiki 20 au zaidi na kijusi chako (mtoto) kinakufa kabla ya kuzaliwa
Mtoto kuzaliwa mfu ni sawa na kuharibika kwa mimba, isipokuwa kuharibika kwa mimba hutokea kabla ya wiki 20 na mtoto kuzaliwa mfu hutokea baada ya wiki 20
Je, ni nini husababisha mtoto kuzaliwa mfu?
Sio visa vyote vya watoto kuzaliwa wafu husababishwa na tatizo moja. Madaktari hufanya vipimo ili kubaini chanzo cha mtoto kuzaliwa mfu. Mara nyingi, hawapati chanzo chochote. Wakati mwingine wanapata tatizo la kondo la nyuma (kiungo kinacholisha kijusi), kijusi, au mwili wako.
Matatizo na kondo la nyuma
Kondo ya uzazi inapotenguka kutoka kwa uterasi mapema sana (kutenguka kwa kondo ya uzazi)
Maambukizi ya ndani na karibu na kondo la nyuma (maambukizi ya ndani ya maji ya amnioti)
Matatizo ambayo husababisha damu kidogo kufika kwa kijusi (jambo ambalo linamaanisha kuwa mtoto anapata oksijeni na virutubisho kidogo)
Kuvuja Damu
Matatizo ya kijusi
Jeni au kromosomu zisizo za kawaida
Kasoro ya kuzaliwa
Maambukizi
Matatizo katika mwili wako
Ugonjwa wa kisukari ambao haujatibiwa
Shinikizo la juu la damu linalotokea wakati wa ujauzito (preeklampsia)
Matumizi ya dawa za kulevya, kama vile kokeini, pombe au tumbaku
Majeraha
Tatizo la damu kuganda
Tatizo kwenye tezi dundumio yako
Je, dalili za mtoto kuzaliwa mfu ni zipi?
Mara nyingi, baada ya kijusi kufa, unapata uchungu wa uzazi. Wakati wa uchungu wa uzazi, daktari wako ataona kuwa kijusi kimekufa.
Wakati mwingine kijusi hufa lakini haupati uchungu wa uzazi. Huenda usiwe na dalili kwa muda. Wakati mwingine dalili hujitokeza wazi:
Hauhisi kijusi kikisogea au kupiga teke
Kuvuja damu kwenye uke wako
Kukakamaa
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina mtoto atakayezaliwa mfu?
Mpigie simu daktari wako mara moja ikiwa una dalili za kujifungua mtoto mfu. Daktari atafanya vipimo ili kuchunguza afya ya kijusi, kama vile kipimo cha picha kutumia mawimbi ya sauti (picha za sehemu tofauti za sehemu ya ndani ya uterasi yako).
Madaktari hufanya nini ikiwa nimejifungua mtoto mfu?
Ikiwa umejifungua kijusi na kondo la nyuma kutoka, hutahitaji matibabu yoyote.
Ikiwa kijusi au kondo la nyuma bado liko kwenye mwili wako, linahitajika kutolewa nje. Daktari wako anaweza:
Kutumia dawa ambayo inaweza kuanzisha uchungu wa uzazi
Kuondoa kijusi na kondo la uzazi kwa kutumia vyombo vya upasuaji vinavyowekwa kwenye uterasi yako (tumbo la uzazi) kupitia uke wako (njia ya uzazi)
Ikiwa madaktari wanahitaji kufanya upasuaji, watakupa dawa ya nusukaputi (dawa ya kukufanya ulale).
Ni jambo la kawaida kuhisi huzuni, hasira, na hatia baada ya kujifungua mtoto mfu.
Zungumza na mtu mwingine ukiwa na huzuni na masikitiko kwa kupoteza ujauzito wako
Ikiwa una wasiwasi kuhusu kujifungua mtoto mfu mwingine, zungumza na daktari ambaye anaweza kujadili vipimo vinavyoweza kufanywa ikiwa vinahitajika
Kumbuka kuwa wanawake wengi waliojifungua watoto wafu hupata ujauzito tena na kuzaa watoto wenye afya nzuri