Nini maana ya kuwa na kinga?
Una kinga dhidi ya maambukizi wakati kinga ya asili ya mwili wako imejifunza jinsi ya kupambana nayo. Unaweza kupata kinga ya kiasili baada ya kuathiriwa na vijidudu kama vile bakteria au virusi. Au unaweza kupata kinga dhidi ya maambukizi fulani kwa sababu ulipewa chanjo dhidi yake. Ndiyo maana kupata chanjo wakati mwingine huitwa "kupata kinga."
Chanjo ni nini?
Chanjo ni njia ya kuandaa mwili wako kukabiliana na maambukizi fulani. Chanjo huwezesha mfumo wa kingamwili wa mwili wako jinsi ya kupigana na magonjwa fulani. Tofauti na dawa chanjo haikabiliani na maambukizi baada ya wewe kuugua. Badala yake, chanjo hukusaidia kuepuka kuugua au, ikiwa utaambukizwa, zinaweza kukusaidia kupambana na maambukizo ili usiumwe.
Kila chanjo huzuia aina moja tu ya maambukizi. Kwa mfano, chanjo ya mafua huzuia mafua pekee. Huenda baadhi ya chanjo zikatolewa mara kadhaa ili ziweze kufanya kazi kikamilifu. Kwa sababu chanjo kwa kawaida hutolewa kwa kudungwa (sindano), mara nyingi chanjo kadhaa huchanganywa kwenye sindano moja ili kupunguza idadi ya kudungwa.
Je, chanjo hufanya kazi?
Ndiyo, chanjo hupunguza hatari ya kupata maambukizi. Watu ambao hawapati chanjo wana uwezekano mkubwa wa kuugua au kufariki kutokana na baadhi ya maambukizi kuliko watu wanaopata chanjo. Hata hivyo, hakuna chanjo inayofanya kazi kwa asilimia 100 kila wakati. Baadhi ya watu ambao wamepata chanjo ya maambukizi fulani bado wanaweza kuugua kutokana na maambukizi hayo, lakini chanjo hiyo inaweza kuwawezesha kupambana na maambukizi ili wasigonjeke sana. Pia, maambukizi mengi makubwa, kama vile VVU na maambukizi mengine ya zinaa hayana chanjo.
Awali, maelfu ya watoto walifariki kila mwaka kutokana na magonjwa ambayo kwa sasa yanazuilika kwa chanjo. Mamia ya maelfu waliugua sana. Kwa sababu ya chanjo:
Je, chanjo ni salama?
Ndiyo, chanjo inachukuliwa kuwa salama kabisa. Watu wachache hupata madhara, lakini madhara hayo mara nyingi huwa mepesi tu. Na magonjwa ambayo chanjo huzuia ni hatari zaidi kuliko madhara ya chanjo.
Kabla ya chanjo kutumika, hufanyiwa majaribio ya kiusalama
Mara nyingi, madhara huwa madogo, kama vile maumivu ulipodungwa sindano, upele, au homa kiasi
Mara chache, chanjo husababisha athari mbaya zaidi, ya ghafla ya mzio (inayoitwa mmenyuko wa anafailaktiki), kama vile uvimbe wa ulimi na koo na ugumu wa kupumua.
Baadhi ya chanjo (kama vile chanjo za mafua) hutengenezwa kwa dutu kutoka kwa mayai. Chanjo zinazotengenezwa kwa kutumia mayai zina uwezekano mkubwa wa kusababisha mmenyuko wa mzio. Madaktari watakuuliza kama una mzio wa mayai kabla ya kukupa chanjo kama hizo.
Je, chanjo husababisha tawahudi?
La, hakuna uhusiano uliobainishwa kati ya chanjo na usonji.
Tafiti nyingi ambazo zimefanywa na madaktari kutoka kote ulimwenguni hazijabaini uhusiano wowote kati ya chanjo na usonji
Watoto wanaopata chanjo hawana uwezekano mkubwa wa kupata tawahudi kuliko watoto ambao hawapati chanjo
Angalia Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC): Usonji na Chanjo.
Nani hupata chanjo na lini?
Watoto wakubwa na wachanga kwa kawaida hupata chanjo kulingana na ratiba iliyopendekezwa ya chanjo ya utotoni wanapokuwa katika hatari ya kwanza ya ugonjwa, jambo ambalo hupunguza uwezekano wa kuambukizwa (angalia CDC: Ratiba ya chanjo ya watoto na vijana wa balehe kulingana na umri)
Watu wazima wanaweza kuhitaji chanjo fulani kulingana na historia yao ya afya, kazi, na eneo (angalia CDC: Ratiba ya chanjo ya watu wazima kulingana na umri)
Wasafiri wanaweza kuhitaji chanjo fulani kabla ya kwenda mahali ambapo yana magonjwa yasiyopatikana kwa kawaida katika nchi zao (angalia CDC: Afya ya Wasafiri)
Muulize daktari wako ili kujua ni chanjo gani unahitaji na wakati wa kuzipata.
Ninaweza kupata wapi maelezo zaidi kuhusu chanjo?
Tovuti zifuatazo hutoa maelezo ya ziada kuhusu chanjo:
CDC: Maswali yanayoulizwa sana na wazazi na walezi kuhusu usalama wa chanjo
CDC: Chanjo kwa Watoto Wako: Taarifa za chanjo zinazotolewa kulingana na umri
Mfumo wa Kuripoti Matukio Mabaya ya Chanjo (VAERS): Wapi na jinsi ya kuripoti athari za chanjo
Hospitali ya watoto ya Philadelphia: Kituo cha Elimu ya Chanjo
Kituo cha Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (ECDC): Ratiba za chanjo katika nchi zote za EU/EEA