Je, surua ni nini?
Surua ni maambukizi ya virusi. Surua ulikuwa ugonjwa wa kawaida sana kwa watoto nchini Marekani. Surua sasa ni nadra nchini Marekani kwa sababu imezuiwa na chanjo za kawaida za utotoni. Katika sehemu za dunia ambapo watoto wachache huchanjwa, surua bado ni jambo la kawaida.
Surua husababishwa na virusi ambavyo huenea haraka miongoni mwa watu ambao hawajachanjwa
Dalili ni pamoja na homa, kutokwa na kamasi mapuani, kikohozi, macho mekundu, na upele
Kwa kawaida surua si tatizo kubwa kwa watoto wenye afya nzuri, lakini mara chache inaweza kusababisha uharibifu wa ubongo au kifo
Chanjo ya surua inaweza kuwalinda watoto dhidi ya kuugua surua
Je, surua husababishwa na nini?
Surua husababishwa na virusi. Watoto wenye afya nzuri ambao hawajapata chanjo wanaweza kupata surua kwa kupumua tu virusi baada ya mtu aliye na surua kukohoa au kupiga chafya karibu nao.
Je, dalili za surua ni zipi?
Dalili za kwanza huanza siku 7 hadi 14 baada ya maambukizi:
Homa
Pua zinazotoa kamasi
Kikohozi kikavu, kifupi na cha mara kwa mara
Macho mekundu
Wakti mwingine mtu huathiriwa na mwangaza mkali
Alama ndogo nyekundu zenye sehemu nyeupe au bluu-nyeupe ndani ya mdomo
Maumivu kooni
Takriban siku 3 hadi 5 baadaye, mtoto wako anaweza kuwa na:
Vipele vinavyowasha—vipele huanza chini na mbele ya masikio, au kwenye shingo, na kisha kuenea kwa mwili wote
Homa inayozidi 104° F (selsiasi 40°)
Maambukizi ya macho (jicho la rangi ya waridi, pia huitwa macho mekundu)
Picha kwa hisani ya Maktaba ya Picha za Afya kwa Umma ya Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa.
Je, surua husababisha matatizo gani?
Katika watoto wenye afya, surua sio tatizo kubwa sana. Hata hivyo, wakati mwingine surua husababisha shida kubwa za kiafya, kama vile:
Maambukizi ya mapafu (nimonia)
Kuvuja damu kupita kiasi (thrombosaitopenia)
Maambukizi ya ubongo (kuvimba kwa ubongo), ambao u naweza kusababisha maumivu ya kichwa, kifafa, na kukosa fahamu takriban siku 2 hadi 14 baada ya upele na inaweza kusababisha uharibifu wa ubongo au kifo
Nchini Marekani, takriban mtoto 1 hadi 2 kati ya watoto 1000 walio na surua hufa. Pia, miaka mingi baada ya kuwa na surua, baadhi ya watu hupata tatizo la nadra la ubongo liitwalo ugonjwa wa Dawson (SSPE), ambalo husababisha uharibifu wa ubongo na kifo.
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa mtoto wangu ana surua?
Madaktari watafanya uchunguzi wa kimwili. Watatafuta:
Upele wa surua
Madoadoa ndogo nyekundu yenye sehemu ya katikati iliyo bluu au bluu-nyeupe mdomoni (Madoadoa yanayotambuliwa kabla ya kuanza kwa upele au madoadoa ya Koplik)
Madaktari watafanya vipimo vya damu ili kujua kwa uhakika ikiwa mtoto wako ana surua. Ikiwa mtoto wako atapatikana na surua, madaktari watawaambia maafisa wa afya ya umma, ambao watajaribu kuzuia ugonjwa wa surua kuenea kwa watu wengi sana katika eneo lako.
Picha kwa hisani ya Maktaba ya Picha ya Afya ya Umma ya Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa.
Je, madaktari wanatibu surua vipi?
Hakuna matibabu ambayo yanaweza kutibu ugonjwa wa surua. Mwache mtoto wako apumzike virusi vinapoendelea kufanya kazi yake.
Ili kumsaidia mtoto wako, unaweza:
Kumpa dawa za kupunguza homa (kama vile acetaminophen au ibuprofeni)
Muepushe mtoto wako na baridi na awe sawa
Ili kupunguza uwezekano wa matatizo kutokana na surua, madaktari wanaweza kumpa mtoto wako vitamini A
Je, ninawezaje kuzuia ugonjwa wa surua?
Hakikisha kuwa mtoto wako amepata chanjo ya surua.
Kwa jumla, watoto hupata chanjo 2 za surua, wakiwa na umri wa miezi 12 hadi 15 na wakiwa na umri wa miaka 4 hadi 6
Watoto walio na umri wa miezi 6 wanaweza kupata chanjo yao ya kwanza ikihitajika, kama vile wakati wa mlipuko wa surua au kabla ya kusafiri nje ya Marekani
Chanjo ya surua ni sehemu ya chanjo ya MMR, ambayo ni chanjo ambayo husaidia pia kukinga dhidi ya matumbwitumbwi na rubela
Chanjo ya surua haisababishi usonji
Baadhi ya watu wanaweza kupata joto la kidogo na upele baada ya kupata chanjo
Watu fulani hawapaswi kupata chanjo ya MMR, ikiwa ni pamoja na wanawake wajawazito na watu ambao ni wagonjwa sana au wana mfumo dhaifu wa kingamwili