Konjunktivaitisi ya Kuambukiza

(jicho la rangi ya waridi; jicho la waridi)

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Konjunktiva ni tishu wazi, nyembamba inayopatikana ndani ya kope zako na hufunika sehemu nyeupe ya jicho lako. Konjunktivaitisi ni mwako (kuvimba na mwasho) kwenye konjuktiva yako.

Konjunktivaitisi ya kuambukiza ni nini?

Konjunktivaitisi ya kuambukiza husababishwa na maambukizi ya aina mbalimbali za bakteria na virusi. Mara nyingi huitwa jicho la rangi ya waridi kwa sababu macho yako yanageuka ya wridi au mekundu.

  • Konjunktivaitisi ya kuambukiza husambaa kwa urahisi kutoka jicho moja hadi jingine, vilevile kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

  • Mara nyingi husababishwa na virusi

  • konjunktivaitisi ya virusi (inayosababishwa na virusi) inadumu kwa wiki 1 hadi 2 na inatoweka yenyewe

  • Ikiwa una konjunktivaitisi ya bakteria, madaktari watakupa matone ya macho yenye dawa ya kuua bakteria

  • Ili kuepuka kusambaza konjunktivaitisi kwa wengine, nawa mikono mara kwa mara na epuka kushiriki taulo, vitambaa, na matandiko

Watoto wachanga waliozaliwa hivi karibuni wanaweza kupata konjunktivaitisi ikiwa mama zao wana klamidia au kisonono. Maambukizi hupitishwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kuzaliwa. Watoto wanaweza kuwa vipofu wasipotibiwa na wanahitaji kuona daktari mara moja.

Mambo mengine mbali na maambukizi yanaweza kusababisha konjunktivaitisi. Kwa mfano, chembe ya uchafu, lenzi za mawasiliano, au vipodozi vinaweza kusababisha kuwasha na kuvimba kwa konjunktiva. Mzio wakati mwingine husababisha mzio wa konjunktivaitisi.

Dalili za konjunktivaitisi ya kuambukiza ni zipi?

Dalili kawaida huanza katika jicho moja na kisha kuenea hadi jingine. Wakati mwingine maambukizi huja wakati una homa.

Dalili za kawaida ni pamoja na:

  • Macho ya waridi au mekundu

  • Macho yenye mwasho

  • Macho yenye majimaji

Wakati mwingine, kiowevu kinachotoka kwenye macho yako ni cheupe au cha manjano kama usaha. Kinaweza kuwa kizito badala ya majimaji. Unaweza kuamka huku macho yako yakiwa yamefungika. Kuosha macho yako kwa maji ya moto kunayasaidia kufunguka kwa urahisi.

Wakati mwingine unaweza pia kugundua:

  • Mwanga unasumbua macho yako

  • Kuona kwako kumefifia kwa sababu ya kiowevu chote machoni mwako

Ikiwa imsababishwa na bakteria, kuna uwezekano kwamba:

  • Kinachotoka kwenye jicho lako kitakuwa kizito, kinanata, na cheupe au cha manjano (usaha)

  • Jicho lako linaweza kuwa limefungika unapoamka asubuhi

Watoto walio na klamidia au kisonono machoni mwao wana:

  • Usaha unaotoka kwenye jicho

  • Ukope uliovimba

Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina konjunktivaitisi ya kuambukiza?

Madaktari wanaweza kubaini kulingana na dalili zako na uchunguzi wa macho. Ikiwa madaktari wanafikiri klamidia, kisonono, au tatizo jingine linaweza kusababisha matatizo ya jicho lako, watachukua sampuli kutoka kwenye jicho lako na kufanya vipimo.

Je, madaktari wanatibu vipi konjunktivaitisi ya kuambukiza?

Ikiwa sababu ni virusi:

  • Dalili zako zitatoweka zenyewe ndani ya wiki 1 hadi 2

  • Ili kutuliza jicho linalowasha, weka kitambaa chenye joto au baridi juu yake

  • Ikiwa kuona kwako kumefifia au kunaathiriwa na mwanga, madaktari wanaweza kukupa matone ya macho ya kotikosteroidi

Ikiwa madaktari wanadhani konjunktivaitisi yako ya kuambukiza inaweza kuwa imesababishwa na bakteria, watakupatia matone au mafuta ya macho yenye dawa ya kuua bakteria.

Kwa mtoto mchanga aliyezaliwa hivi karibuni, madaktari:

  • Watampa mtoto aliyezaliwa karibuni dawa ya kuua bakteria ikiwa mtoto ana konjunktivaitisi inayosababishwa na kisonono au klamidia

  • Pia watibu wazazi wa mtoto

Ili kuzuia konjunktivaitisi, madaktari huwapa watoto waliozaliwa hivi karibuni matone ya jicho au mafuta mara tu baada ya kuzaliwa.

Ninawezaje kuzuia konjunktivaitisi ya kuambukiza kuenea?

Ikiwa una konjunktivaitisi ya kuambukiza, chukua hatua hizi ili usiieneze:

  • Nawa mikono kwa sabuni na maji au tumia dawa za kuua viini mara kwa mara na hasa kabla na baada ya kusafisha jicho au kuweka dawa kwenye jicho lako

  • Usiguse macho yako

  • Usishiriki taulo, nguo za kuogea, na matandiko na wengine

  • Kaa nyumbani kutoka shuleni au kazini kwa siku chache