Mzio wa Konjunktivaitisi

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Konjunktiva ni safu angavu na nyembamba inayofunika weupe wa jicho lako na sehemu ya ndani ya kope zako. Konjunktivaitisi ni mwako (kuvimba na mwasho) kwenye konjuktiva yako.

Mzio wa konjunktivaitisi ni nini?

Mzio wa konjunktivaitisi ni athari katika konjunktiva yako unaosababishwa na kitu ambacho una mzio nacho, kama vile chavuo, ukungu au vumbi. Jicho huvimba, kuwa jekundu, na kuwasha.

Mzio wa konjunktivaitisi unaweza kusababishwa na:

  • Mzio wa msimu kwa vitu kama vile ukungu, mti, magugu, au chavuo la nyasi (kwa kawaida huwa na dalili katika masika au vuli)

  • Mzio wa mwaka mzima kwa vitu kama vile vumbi, ngozi ya wanyama, au manyoya (unakuwa na dalili mwaka mzima)

Kuna sababu nyingine za macho mekundu. Kwa mfano, konjunktivaitisi ya kuambukiza husababishwa na maambukizi ya bakteria au ya virusi. Pia, chembe ya uchafu, miwani, au vipodozi vinaweza kuwasha konjunktiva na kusababisha macho mekundu bila kuwa na mmenyuko wa mzio au maambukizi.

Sehemu za Macho

Dalili za mzio wa konjunktivaitisi ni zipi?

Utakuwa na:

  • Kuwasha na kuungua kwa macho yote mawili

  • Macho mekundu na mboni zako za macho zinaweza kuonekana kuwa na uvimbe

  • Macho yenye majimaji

  • Pua inayowasha, yenye kamasi

Hutakuwa na matatizo yoyote ya kuona.

Madaktari wanawezaje kujua kama nina mzio wa konjunktivaitisi?

Madaktari wanaweza kujua kulingana na dalili zako. Kwa kawaida, hakuna vipimo vinavyohitajika.

Madaktari wanatibuje mzio wa konjunktivaitisi?

Daktari atakuambia:

  • Tumia matone ya jicho ya kuzuia mzio

  • Epuka vitu ambavyo una mzio navyo

  • Tumia machozi bandia (matone ya macho yanayofanya kazi kama machozi halisi kulowesha jicho)

  • Wakati mwingine, tumia matone ya kotikosteroidi kama dalili ni kali

Ikiwa una dalili zingine za mzio, kama vile pua yenye kamasi, kupiga chafya, au mwasho, madaktari wanaweza kukushauri kutumia dawa ya kumeza ya antihistamini.