Klamidia ni nini?

Klamidia ni bakteria ambayo inaweza kusababisha aina nyingi za maambukizi. Klamidia kwa kawaida ni maambukizi ya zinaa (STI). Ugonjwa wa zinaa ni maambukizi ambayo huenezwa kutoka kwa mtu hadi mwingine kupitia ngono.

Maambukizi ya zinaa ya klamidia yanaweza kuathiri sehemu zako za siri, kwa wanawake, mirija yako ya uzazi na ovari. Mirija ya uzazi huunganisha ovari (viungo vya uzazi vinavyohifadhi mayai) na uterasi.

Wakati mwingine, kufanya ngono ya kinywa na mtu ambaye ana klamidia inaweza kusababisha maambukizi ya koo na klamidia. Ngono kwa njia ya tundu la haja kubwa inaweza kusababisha maambukizi kwenye rektamu (pale ambapo kinyesi huhifadhiwa).

  • Unaweza kupata klamidia kupitia ngono ya uke, mdomo, au tundu la haja kubwa na mtu aliyeambukizwa

  • Mwanamke mjamzito anaweza kueneza klamidia kwa macho au mapafu ya mtoto wake wakati wa kuzaliwa

  • Huenda usiwe na dalili zozote hata kama umeambukizwa, au dalili zako zinaweza kuchukua wiki nyingi kukukera baada ya kuambukizwa.

  • Kwa wanaume, dalili ni pamoja na kutokwa na mshuko kutoka kwa uume na maumivu makali kwenye urethra (ncha ya uume) wakati wa kukojoa (haja ndogo)

  • Kwa wanawake, dalili zinajumuisha kuhisi haja ya kukojoa mara kwa mara, maumivu wakati wa kukojoa, na kuwa na majimaji mazito ya manjano kutoka kwenye uke wako (vitu kutoka ukeni).

  • Wanawake wasipopata matibabu wanaweza kuwa na madhara ya kudumu na kufanya iwe vigumu au isiwezekane kabisa kupata mtoto

  • Ikiwa unashiriki ngono, zungumza na daktari wako kuhusu kipimo cha uchunguzi wa klamidia

  • Madaktari hutibu klamidia kwa dawa za kuua bakteria

Mwanamke aliye na klamidia akikosa kutibiwa anaweza kupata ugonjwa wa kuchochewa kwa fupanyonga (PID). PID ni maambukizi kwenye uterasi, mirija ya uzazi au vyote kwa pamoja. PID pia inaweza kusambaa katika ovari zako na kwenye mtiririko wa damu. PID inaweza kuharibu viungo vyako vya uzazi na kufanya iwe vigumu kupata mtoto.

Mwanamume aliye na klamidia anaweza kupata epididimitisi, maambukizi ya epididimisi. Epididimisi ni bomba lililojikunja sehemu ya juu ya korodani. Ugonjwa wa epididimitisi husababisha maumivu na uvimbe ya mfuko wako wa korodani.

Dalili za klamidia ni zipi?

Wanawake

Wanawake wengi hawana dalili zozote au wanaonyesha dalili chache tu:

  • Kuhisi kama una haja ya kukojoa mara nyingi zaidi kuliko kawaida

  • Maumivu unapokojoa

  • Ute wa manjano kutoka ukeni

  • Maumivu wakati wa kufanya ngono

  • Wakati mwingine maumivu makali chini ya tumbo

Wanaume

Wanaume wengi hupata dalili:

  • Maumivu makali wakati wa kukojoa

  • Kuhisi kukojoa zaidi kuliko kawaida

  • Uchafu wa kijivu au usiokuwa na rangi (majimaji mazito) kutoka kwenye uume

  • Mdomo wa kwa uume wako kuwa mwekundu kufungika asubuhi

  • Uvimbe wenye maumivu kwenye korodani kwa pande moja au zote mbili (ikiwa una epididimitisi)

Wanawake na wanaume

Ikiwa rektamu yako imeambukizwa, unaweza kuwa na maumivu na kutokwa na uchafu wa manjano kwenye tundu lako la haja kubwa (pale ambapo hupitisha kinyesi).

Ikiwa koo lako limeambukizwa, kwa kawaida hutakuwa na dalili yoyote.

Bado unaweza kumwambukiza mpenzi wako hata kama huna dalili.

Madaktari wanawezaje kujua kama nina klamidia?

  • Madaktari hushuku klamidia kulingana na dalili zako

  • Hakika, watapima mkojo wako au kwa sampuli kutoka kwa uume, uke, koo au rektamu yako.

Huenda daktari wako akapitisha pamba ndogo kwenye uume, koo, au rektamu yako ili kupata sampuli ya majimaji ya kupima. Ikiwa wewe ni mwanamke, daktari wako ataangalia kwenye uke wako kwa kutumia kifaa cha plastiki na kuchukua usaha kutoka kwenye mlango wa uzazi (sehemu ya chini ya mfuko wa uzazi inayofunguka hadi kwenye uke wako).

Ikiwa wewe ni mjamzito au uko katika hatari kubwa ya kuwa na klamidia, daktari wako anaweza kufanya kipimo cha mkojo cha klamidia iwapo huna dalili zozote. Wanawake wako katika hatari kubwa zaidi kwa:

  • Kushiriki ngono wakiwa chini ya miaka 25

  • Umewahi kupata maambukizi ya zinaa

  • Kushiriki katika shughuli hatari za ngono (kama vile kushiriki katika biashara ya ngono, kuwa na mwenzi anayefanya biashara ya ngono, kuwa na wapenzi wengi, au kutotumia kondomu mara kwa mara)

  • Kuwa na mpenzi anayefanya shughuli hatari za ngono

Wanaume wako katika hatari kubwa zaidi kwa:

  • Kushiriki ngono na mwanaume mwenzao ndani ya mwaka mmoja uliopita

Huenda daktari akakupima pia damu au mkojo wako kuchunguza magonjwa mengine ya zinaa kwa sababu watu wengi wana zaidi ya ugonjwa mmoja wa zinaa.

Madaktari hutibu vipi klamidia?

Madaktari watafanya:

  • Watakupa wewe na mwenzi wako wa kingono dawa za kuua bakteria

  • Kukuambia uepuke kujamiiana hadi umalize dawa za kuua bakteria ili kuzuia kueneza klamidia