Kaswende ni nini?

Kaswende ni maambukizi ya zinaa (STI). Ugonjwa wa zinaa ni maambukizi ambayo huenezwa kutoka kwa mtu hadi mwingine kupitia ngono.

  • Kaswende huenea kwa urahisi kupitia kufanya ngono kwa njia ya tundu la haja kubwa, kinywa, au uke na mtu aliyeambukizwa

  • Mwanamke mjamzito anaweza kumwambukiza kaswende mtoto wake

  • Kaswende ina hatua 3 ambazo huendelea kuwa mbaya zaidi

  • Madaktari hutibu kaswende kwa penisilini

Hatua 3 za kaswende ni zipi?

Hatua ya 1: Kaswende huanza katika sehemu ya mwili wako ambayo iligusana na majimaji ya mwili wa mwenzi wako wa ngono. Kwa mfano, ikiwa ulishiriki ngono ya uke, kaswende inaweza kuanza kwenye uume wako (kama wewe ni mwanamume) au ndani ya au karibu na uke wako (kama wewe ni mwanamke).

Hatua ya 2: Kaswende huenea kwenye damu yako na kuambukiza ngozi yako.

Hatua ya 3: Kaswende huenea katika mwili wako wote. Sehemu yoyote ya mwili inaweza kuambukizwa na kaswende lakini hasa moyo, mishipa ya damu, ubongo na uti wa mgongo.

Mara nyingi kuna muda fulani kati ya hatua ya 2 na hatua ya 3. Muda huu unaitwa kipindi fiche. Katika kipindi fiche, watu hujisikia vizuri na kwa kawaida hawawezi kupitisha kaswende kwa watu wengine. Wakati mwingine kaswende hutoweka baada ya hatua ya 2. Walakini, takribani mtu 1 kati ya 3 aiyetibiwa maambukizi ya kaswende huenda kwenye hatua ya 3.

Dalili za kaswende ni zipi?

Dalili ni tofauti katika kila hatua ya kaswende.

Dalili za kaswende ya hatua ya 1 (ya msingi).

  • Eneo dogo, jekundu, lililochomoza kwenye sehemu ya maambukizi, kama vile uume wako, uke, rektamu (pale ambapo kinyesi huhifadhiwa), au midomo.

  • Eneo dogo jekundu hubadilika na kuwa kidonda kisicho na maumivu, kilicho wazi ambacho ni kigumu na hakitoi damu

  • Huenda usione kidonda kwa sababu hakisababishi dalili nyingi

  • Wiki 3 hadi 12 baadaye, kidonda hupona na utajisikia mzima

Isipotibiwa, kaswende itaendelea hadi kwenye hatua ya 2 kwa sababu maambukizi huenea katika damu yako.

Dalili za kaswende ya hatua ya 2 (ya pili).

  • Upele usiowasha kwenye mwili wako—tofauti na vipele vingine vingi, vipele kutoka kwa kaswende mara nyingi huonekana kwenye viganja vya mikono au kwenye nyayo za miguu.

  • Chunjua zilizoinuka, zenye ncha bapa na laini zinaweza pia kutokea kwenye sehemu zenye unyevunyevu karibu na mdomo, kwapa, viungo vya uzazi na tundu la haja kubwa (ambapo kinyesi hupitishwa)

  • Homa

  • Kujisikia dhaifu na mchovu mwili mzima

  • Kutohisi njaa kama kawaida

  • Vinundu vya limfu vilivyovimba

Vipele vimejaa vijidudu vya kaswende. Vijidudu vinaweza kuenea kwa watu wanaogusa chunjua hizo.

Dalili za hatua ya 2 hutoweka hatimaye. Lakini zinaweza kusababisha matatizo katika sehemu nyingine za mwili na viungo, kama vile ini, figo, na macho yako. Isipotibiwa, huenda ukakosa kuwa na dalili zaidi. Walakini, takriban mtu 1 kati ya 3 anayepata kaswende huendelea hadi hatua ya 3.

Dalili za kaswende ya hatua ya 3 (ya juu).

Dalili zinaweza kuathiri ngozi yako, mishipa ya damu, moyo, ubongo, au uti wa mgongo.

Matatizo ya ngozi yanaweza kujumuisha:

  • Uvimbe laini kama vile mpira kwenye ngozi yako, kama vile ngozi ya kichwa na uso (uvimbe unaweza pia kuwa ndani ya mwili wako, kama vile ini au mifupa)

  • Uvimbe huo hugeuka kuwa vidonda vilivyo wazi na kuua tishu zinazouzunguka

  • Uvimbe hupona polepole na kuacha makovu

Matatizo ya mishipa ya damu kwa kawaida huhusisha ateri kubwa (mkole) inayotoka kwenye moyo na kupeleka damu mwilini. Mkole unaweza kudhoofika na kutanuka. Wakati mwingine mkole dhaifu hupasuka, (kuvunjika) na unaweza kusababisha kifo. Tatizo la mkole husababisha:

  • Maumivu ya kifua

Matatizo ya moyo kwa kawaida husababisha vali za moyo kuvuja na dalili zake ni:

  • Maumivu ya kifua

  • Kupumua kwa shida

  • Shambulio la moyo

Matatizo ya ubongo kwa kawaida hayaonekani kwa miaka 15 hadi 20. Dalili zinajumuisha:

  • Maumivu ya kichwa

  • Shingo iliyokaza

  • Mabadiliko katika hali ya hisia au tabia

  • Kutofikiria vyema

Maambukizi ya uti wa mgongo hufanya iwe vigumu kudhibiti misuli yako. Huenda ukahitaji:

  • Kupoteza hisia kwenye miguu yako

  • Ugumu wa kutembea

  • Maumivu kwenye mgongo, miguu, au mikono

  • Udhaifu wa mikono au miguu yako

Madaktari wanawezaje kujua kama nina kaswende?

Ili kugundua kaswende, madaktari hufanya vipimo vya damu. Iwapo wanafikiri kuwa kaswende imeathiri ubongo wako au uti wa mgongo, madaktari wanaweza kukufanyia taratibu za kufyonza majimaji ya uti wa mgongo.

Madaktari hutibu vipi kaswende?

Madaktari watafanya:

  • Kukudungia dozi ya penisilini kwenye misuli yako, kwa kawaida kwenye makalio

  • Kukupa dozi za ziada za penisilini kulingana na hatua yako na dalili

  • Kukuambia uepuke kushiriki ngono hadi umalize matibabu

  • Kuwapima na kuwatibu kaswende wenzi wako wa ngono

  • Kufanya vipimo vya damu ili kuhakikisha kuwa matibabu yamefaulu

Watu walio na mzio wa penisilini wanaweza kupewa dawa zingine za kuua bakteria.

Wakati mwingine penisilini inapoua vijidudu vya kaswende, mwili wako hupata mwitikio wa vijidudu vilivyokufa na vinavyokufa. Mwitikio huu kwa kawaida hufanyika ndani ya saa 12 za kwanza. Unaweza kupata homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, na upele. Mwitikio huu husababisha usumbufu, lakini si hatari Kwa kawaida, dalili hupotea ndani ya saa 24: Mwitikio huu hautokani na mizio ya penisillini.