Pepopunda

(Pepopunda)

Imepitiwa/Imerekebishwa Jul 2023

Je, pepopunda ni nini?

Pepopunda ni ugonjwa unaotishia maisha unaosababishwa na bakteria iitwayo Clostridium tetani.

  • Bakteria ya pepopunda hutoa sumu ambayo huathiri neva na ubongo wako

  • Pepopunda inaweza kutokea baada ya kukatwa, kuwa na jeraha la kutobolewa, kuungua, au jeraha lolote linaloruhusu vijidudu kuingia kwenye ngozi yako

  • Dalili kwa kawaida huanza na mkazo mkali wa misuli wa siku 5 hadi 10 baada ya kupata jeraha

  • Huenda ukawa na tatizo la kumeza na kupumua, ambalo linaweza kuwa mbaya sana

  • Kachannjwa kwa chanjo ya pepopunda kunasaidia kuzuia pepopunda

Muone daktari mara moja ikiwa unafikiri kuwa unaweza kuwa na pepopunda au ikiwa una jeraha la kutobolewa, mkato mkubwa, au jeraha ambalo ni gumu kusafisha vizuri.

Je, ugonjwa wa pepopunda unasababishwa nini?

Bakteria wanaosababisha pepopunda huishi kwenye uchafu na kinyesi cha wanyama. Wanaweza kuingia kwenye mwili wako unapopata:

  • Jeraha la kukatwa au kutobolewa, haswa lililo na kina kirefu au lenye uchafu ndani yake

  • Kuchomwa kwa sindano chafu (kama vile sindano ya tattoo au sindano unayotumia kujidunga dawa za mitaani)

  • Jeraha la ngozi kama vile jeraha la kuungua au linalosababishwa na baridi kali

Katika sehemu za dunia zenye hali duni ya usafi wa mazingira, uchafu unaweza kuingia kwenye kikonyo cha kiunga mwana na kusababisha pepopunda kwa watoto wachanga.

Je, dalili za pepopunda ni zipi?

Dalili huanza siku 5 hadi 10 baada ya jeraha, na wakati mwingine baada ya muda mrefu wa siku 50 baadaye. Zinajumuisha:

  • Maumivu ya misuli ambayo ni chungu na yanafanya misuli yako kuwa imara na ngumu

Maumivu ya misuli kwa kawaida huanza kwenye taya yako. Huwezi kufungua taya yako, ndiyo maana pepopunda wakati mwingine inatwa "kufungana kwa taya." Maumivu ya misuli yanaweza kuathiri koo lako na kupumua, na baadaye shingo yako, mabega, uso, mikono, miguu, mgongo na tumbo. Wakati mwingine watu walio na pepopunda huwa na nyuso zilizoganda kwa tabasamu huku nyusi zikiwa zimeinuka juu. Wanaweza pia kuwa na mgongo uliopinda na tazito wakati wa kukojoa au kupitisha kinyesi (haja kubwa).

Dalili zingine ni pamoja na:

  • Mapigo ya moyo ya haraka

  • Homa na kutokwa na jasho

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina pepopunda?

Madaktari wanaweza kujua kuwa una pepopunda kutokana na dalili zako na kwa kuulizia kuhusu majeraha yoyote ya hivi majuzi ambayo umekuwa nayo. Wanaweza kuchukua sampuli ya tishu zilizojeruhiwa ili kupima ikiwa zina bakteria.

Je, madaktari hutibu vipi pepopunda?

Watu wenye pepopunda hutibiwa hospitalini. Madaktari watasafisha majeraha yoyote na kuondoa tishu za ngozi zilizokufa. Madaktari watatibu pepopunda kwa kutumia:

  • Dawa za kuua bakteria zinazowekwa kwenye mshipa wako wa damu kupitia IV

  • Sindano ya dawa ili kupunguza maumivu ya misuli

  • Chanjo ya pepopunda, ikiwa hujawahi kuipata au hujapata chanjo ya nyongeza katika kipindi cha miaka 10 iliyopita

  • Dawa ya maumivu na wasiwasi

Ikiwa huwezi kupumua, madaktari wataingiza bomba la kupumulia kwenye koo yako na kukuweka kwenye mashine ya kupumulia. Ikiwa huwezi kumeza, madaktari watakupa chakula na vowevu kupitia mishipa yako ya damu kwa kutumia IV.

Je, ninawezaje kuzuia pepopunda?

Unaweza kuzuia pepopunda kwa kupata chanjo ya pepopunda (chanjo). Miongoni watoto wadogo, chanjo ya pepopunda hutolewa pamoja na chanjo ya dondakoo na kifaduro. Madaktari hutoa msururu wa sindano 3 au zaidi kwa watoto wadogo. Watu wazima wanapaswa kupata chanjo ya ziada ya kuimarisha kinga mara moja kila baada ya miaka 10 baada ya hapo.

Ikiwa utakatwa au kujeruhiwa, hakikisha umesafisha jeraha mara moja kwa sabuni na maji. Kisha, mpigie simu au umtembelee daktari wako ili kuona ikiwa unahitaji sindano ya chanjo ya pepopunda. Utahitaji moja ikiwa hujawahi kudungwa chanjo ya pepopunda au hujapata chanjo ya nyongeza katika miaka 10 iliyopita.