Je, unene wa kupindukia ni nini?
Unene wa kupindukia ni kuwa na mafuta mengi mwilini. Unene wa kupindukia husababisha matatizo ya kiafya. Kadri unavyozidi kunenepa zaidi ndivyo hatari yako ya kupata matatizo ya kiafya inavyoongezeka.
Unene wa kupindukia husababishwa na kula kalori zaidi kuliko kiasi ambacho mwili wako unahitaji
Kuwa mnene kupindukia huongeza uwezekano wako wa kupata magonjwa mengi, kama vile kisukari, shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa moyo, na aina zingine za saratani
Kupunguza uzani hata kidogo kunaweza kupunguza uwezekano wako wa kuwa na matatizo ya kiafya
Ili kupunguza uzani, unapaswa kula kidogo na kufanya shughuli zaidi (kufanya mazoezi)
Dawa au upasuaji wakati mwingine unaweza kusaidia kupunguza uzani
Unene wa kupindukia unaweza kusababisha matatizo katika takriban kila kiungo.
Unene wa kupindukia unaendelea kuongezeka duniani kote. Nchini Marekani, takriban mtu 1 kati ya watu wazima 3 ana unene wa kupindukia. Unene wa kupindukia utotoni pia ni tatizo.
Je, unene wa kupindukia husababishwa na nini?
Unene wa kupindukia husababishwa na kula kalori zaidi kuliko ambacho mwili wako unahitaji. Mlo, jeni, mtindo wa maisha, na matumizi ya dawa fulani ni baadhi ya mambo yanayochangia unene wa kupindukia.
Yafuatayo huongeza uwezekano wako wa kuwa na unene wa kupindukia:
Kutoshiriki shughuli za kutosha za kimwili, kama vile spoti au mazoezi, au kukuwa na kazi ambayo unakaa muda mwingi
Kula vyakula vyenye kalori nyingi (kwa mfano, vitafunio vyenye nishati nyingi) au kukula chakula kingi kwa kipindi kirefu
Kuwa na wanafamilia ambao wana unene wa kupindukia (unene wa kupindukia unarithiwa katika familia)
Ulikwisha wahi kuwa na unene wa kupindukia ukiwa mtoto
Kutopunguza uzani utokanao na ujauzito baada ya kupata watoto
Mabadiliko ya homoni kama vile katika ukomo wa hedhi (mwanamke anapoacha kupata hedhi na hawezi tena kuwa mjamzito)
Kuwa na matatizo fulani ya kula, kama vile ugonjwa wa kula kupita kiasi
Kumeza dawa fulani
Kulala chini ya saa 6 kila usiku
Je, dalili za unene wa kupindukia ni zipi?
Unene wa kupindukia unaweza kusababisha dalili zingine kando na kuonekana kuwa na uzani mkubwa kupita kiasi. Unaweza kuwa na:
Kupumua kwa shida
Kukoroma
Matatizo ya ngozi ikiwa ni pamoja na alama za kunyoosheka kwa ngozi
Maumivu ya viungo na mgongo
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina unene wa kupindukia?
Madaktari wanaweza kujua kuwa una unene wa kupindukia kwa:
Kukokotoa BMI yako (kiashiria cha uzito wa mwili)
Kupima unene wa mafuta yaliyo kwenye kiuno chako na sehemu ya nyuma ya mkono wako wa juu
Wakati mwingine kufanya kipimo ambacho hupima kiasi cha mafuta kwenye mwili wako wote (kipimo cha muundo wa mwili)
BMI yako ni uzani wako (katika kilogram) ukigawanywa na urefu wako (katika mita). Una unene wa kupindukia ikiwa BMI yako ni 30 au zaidi. Una uzani kupita kiasi ikiwa BMI yako ni zaidi ya 25.
Daktari anaweza pia:
Chunguza ikiwa una kisukari na lehemu nyingi kwa kutumia vipimo vya damu
Chunguza ikiwa una shinikizo la juu la damu kwa kutumia kifaa cha kupima shinikizo la damu kinachofungwa kwa mkono
Chunguza ikiwa una magonjwa mengine ambayo hutokea mara nyingi zaidi kwa watu walio na unene wa kupindukia, kama vile kupumua kwa shida wakati wa kulala, ini lenye mafuta, na unyogovu
Je, madaktari wanatibu vipi ugonjwa wa unene wa kupindukia?
Ni rahisi sana kuzuia unene wa kupindukia kuliko kutibu. Mara baada ya kuongeza uzani, mwili wako hukataa kupunguza uzani. Kwa mfano, unapopunguza chakula unachokula, unahisi njaa zaidi na unatumia nguvu kidogo unapopumzika.
Madaktari hutibu unene wa kupindukia kwa kukusaidia kubadilisha baadhi ya tabia zako:
Kula vyakula vyenye afya (vilivyo na nyuzinyuzi nyingi, kiwango kidogo cha sukari)
Weka kiasi kidogo kwenye sahani yako ili usijaribiwe kula sana
Epuka vinywaji vyenye kalori nyingi, kama vile soda, juisi au pombe
Fanya mazoezi zaidi na ujihusishe na shughuli zaidi (kwa mfano, panda ngazi badala ya lifti, au tembea badala ya kuendesha gari au kupanda basi)
Kwenda kwenye mikutano ya kikundi cha watu wengine wanaojaribu kupunguza au kudhibiti uzani wao kunaweza kukusaidia kudumisha ulaji wako wenye afya na mazoea ya kufanya mazoezi.
Kwa watu walio na uzani mwingi wanaostahili kupunguza, madaktari wanaweza kuwapa:
Dawa
Upasuaji wa kupunguza uzani (upasuaji wa bariatriki)