Kiasi cha Juu cha Lehemu

Imepitiwa/Imerekebishwa Feb 2023

Lehemu ni nini?

Lehemu ni aina ya mafuta. Mafuta pia huitwa lipid.

Mwili wako hutumia lehemu kujenga sehemu muhimu za seli na kutengeneza majimaji fulani ya usagaji chakula. Mwili wako unahitaji lehemu. Lakini kuwa na lehemu nyingi zaidi kwenye damu yako (lehemu ya juu) kwa muda mrefu kunaweza kusababisha matatizo ya kiafya.

Lehemu hutoka wapi?

Lehemu katika mwili wako hutoka sehemu mbili:

  • Lehemu fulani hutokana na kula vyakula fulani

  • Lehemu fulani hutengenezwa katika mwili wako kutokana na vitu vingine

Je, zipi ni aina tofauti za lehemu?

Kuna aina nyingi za lehemu. Aina mbili muhimu zinaitwa:

  • Lehemu ya LDL (lehemu mbaya)

  • Lehemu ya HDL (lehemu nzuri)

Jumla ya lehemu ni kiasi cha aina zote tofauti za lehemu katika mtiririko wako wa damu.

Lehemu ya juu ni mbaya?

Kuwa na kiwango kikubwa cha lehemu ya LDL kwa muda mrefu husababisha ugumu wa ateri(atherosklerosisi). Ateri zako huzibwa na mrundikano wa lehemu, mafuta na vitu vingine. Damu hutiririka kwa shida inapopitia mishipa iliyozibwa. Wakati mwingine damu huganda katika maeneo yaliyoziba na kuzuia kabisa mtiririko wa damu. Kuzuia mtiririko wa damu kwenye moyo wako husababisha shambulio la moyo. Kuzuia mtiririko wa damu kwenye ubongo husababisha kiharusi.

Kuwa na kiwango cha juu cha lehemu ya HDL hupunguza uwezekano wa kupata atherosklerosisi. Ndiyo maana HDL inaitwa lehemu nzuri.

Ni nini husababisha lehemu ya juu?

Baadhi ya watu hutengeneza lehemu nyingi mwilini, bila kujalisha wanachokula. Aina hii ya tatizo la lehemu ya juu hurithiwa katika familia.

Lehemu ya juu inaweza pia kusababishwa na:

  • Kula vyakula vingi vya mafuta na lehemu

  • Kuwa na kisukari

  • Kutofanya chochote

  • Kunywa pombe kupita kiasi

  • Kumeza dawa fulani

Sio lazima uwe mnene ili uwe na lehemu ya juu.

Dalili za lehemu ya juu ni zipi?

Lehemu ya juu kwa kawaida haisababishi dalili. Walakini, katika hali mbaya, unaweza kupata:

  • Michubuko midogo ya manjano kwenye ngozi yako kutoka kwa mafuta mengi zaidi (santoma)

Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina kiwango cha juu cha lehemu?

Kipimo rahisi cha damu kinaweza kuwajulisha madaktari ikiwa una lehemu ya juu. Madaktari wanapendekeza kupima lehemu kwa:

  • Watoto kati ya umri wa miaka 9 na 11 (mapema ikiwa wana sababu hatarishi za lehemu ya juu kama vile ugonjwa wa kisukari)

  • Watu wazima wanapofika umri wa miaka 20

Watu wazima wanapaswa kupimwa lehemu kila baada ya miaka 4 hadi 6.

Madaktari hutibu vipi lehemu ya juu?

Lehemu ya juu inaweza kutibiwa kwa:

  • Kupunguza ulaji wa mafuta (hasa mafuta mazito) na lehemu

  • Kufanya mazoezi (kwa mfano, kutembea haraka) angalau dakika 30 kwa siku, mara 5 kwa wiki

  • Kuacha kuvuta sigara ikiwa unavuta sigara

  • Kutumia dawa za kupunguza lehemu

Vyakula vilivyo na viwango vya chini vya mafuta mazito na lehemu ni pamoja na:

  • Matunda na mbogamboga (iwe ni mbichi, zimegandishwa, ziko kwenye makopo au zimekaushwa)

  • Nyama isiyonona, kama vile samaki, kuku na bata mzinga bila ngozi, na aina zisizonona za nyama ya ng'ombe, kondoo, nguruwe na ndama

  • Mikate na vyakula vya nafaka isokobolewa, kama vile nga wa shayiri, pumba, ngano, na mseto wa nafaka

  • Bidhaa za maziwa zisizo na mafuta mengi, kama vile maziwa yaliyoondolewa malai au ya 1%, mtindi usio na mafuta mengi, na jibini isiyo na mafuta mengi

  • Mafuta ya mboga ambayo si mazito, kama vile kanola, mizeituni, mahindi, safflower, uto, soya na alizeti.

Vyakula vilivyo na viwango vya juu vya mafuta mazito na lehemu ni pamoja na:

  • Siagi, malai, au mafuta mazito

  • Soseji, nyama baridi, mkate wenye soseji, nyama ya viungo, mbavu, viini vya mayai, na aina ya mafuta ya nyama ya ng'ombe, kondoo na nguruwe.

  • Bidhaa zilizookwa zilizonunuliwa, kama vile pai, keki, donati, biskuti na mikate yenye mafuta mengi.

  • Bidhaa za maziwa yenye mafuta mengi, kama vile maziwa halisi, malai, vinywaji vinavyochanganywa na maziwa, mtindi wa maziwa halisi, jibini nyingi, siagi, na aiskrimu

  • Mafuta ambayo yana mafuta mengi mazito, kama vile mafuta ya nazi, mawese, mafuta ya nguruwe na bakoni.